Barabara ya Mto wa Mbu-Loliondo yaanza kujengwa

Muktasari:

Ujenzi huo utakamilika ndani ya miezi 24.


Dodoma. Serikali imeanza utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya Mto wa Mbu-Loliondo mkoani Arusha kwa kiwango cha lami.

Akizungumza leo Februari 7, 2018 bungeni mjini Dodoma, Naibu  Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa ameliambia Bunge kuwa mkataba wa awamu ya kwanza ya ujenzi huo unahusisha kilomita 49 kutoka Loliondo (Waso) hadi njiapanda ya Sale ambapo utekelezaji ulianza Oktoba, 2017.

Kwandikwa ametoa kauli hiyo wakati akijibu swali la msingi la mbunge wa viti maalum (CCM), Catherine Magige aliyetaka kujua mchakato wa ujenzi wa barabara hiyo umefika wapi.

Katika majibu yake, Kwandikwa amesema ujenzi wa sehemu hiyo ya barabara unatekelezwa na mhandisi wa Ms China Wu Yi Co Ltd kwa gharama ya Sh87.1 bilioni na unasimamiwa na Wakala wa Barabara kupitia Kitengo cha Wahandisi Washauri Wazawa (TECU).

Amesema mradi huo unagharimiwa na Tanzania kwa asilimia 100 na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 24.