Basata yampongeza Diamond kutajwa tuzo za BET 2021

Thursday June 03 2021
basata pc
By Fortune Francis

Dar es Salaam. Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) limempongeza msanii Nasib Abdul ‘Diamond Platnumz’ kwa kufanikiwa kutajwa kuwania tuzo za Black Entertainment  Television (BET) za mwaka 2021 katika kipengele cha Best International Act (msanii aliyefanya vizuri kimataifa).

Taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Juni 3, 2021 na kaimu katibu mtendaji wa baraza hilo, Matiko Mniko imeeleza hayo ni mafanikio makubwa katika maendeleo ya sanaa na sio kwa Diamond pekee, bali ni kwa tasnia nzima ya mziki wa Tanzani.

“Msanii akishinda tuzo, Taifa zima linapata sifa. Hii ni njia mojawapo ya kuvutia uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi na hatimaye kukuza uchumi wetu,” ameeleza Mniko katika taarifa hiyo.

Kaimu katibu mtendaji huyo ametoa wito kwa wadau wa sanaa na wananchi wote kwa ujumla walio ndani na nje ya nchi kumuunga mkono msanii wetu, ili afanikiwe kutwaa tuzo hiyo.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa washiriki wanaotajwa kuwania tuzo hizo hupatikana kupitia “BET voting members” ambao ni jopo la watu waliopo kwenye sekta ya sanaa na burudani na huangalia mambo yaliyofanywa  katika sanaa na burudani  na msanii husika ndani na nje ya nchi.

Tuzo hizo zinatarajiwa kutolewa Juni 27,2021 huko Los Angeles Marekani.

Advertisement
Advertisement