Bashe aagiza viongozi wa ushirika wakamatwe kwa kutowalipa wakulima

Muktasari:

  • Wakulima wa kijiji cha Isansa wilayani Mbozi mkoani Mbeya wamesimamisha msafara wa Waziri Kilimo, Hussein Bashe na kumweleza changamoto ya kutopewa fedha zao na Amcos yao wakati kahawa zao zimeuzwa.

Songwe. Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ameagiza kukamatwa kwa viongozi chama cha msingi cha ushirika cha zao la kahawa cha Isaso baada wakulima kulalamika kutolipwa fedha zao licha ya kahawa yao kuuzwa.

  

Bashe aliyekuwa akiendelea na ziara katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, msafara wake ulisimamishwa na wakulima wa kijiji cha Isansa wilayani Mbozi ambao walimueleza changamoto hiyo ya kutopewa fedha zao.

Mbunge wa Mbozi, George Mwenisongole alianza kwa kumweleza Bashe kuwa Amcos hiyo imekuwa ni mateso kwa wakulima kwa kushindwa kuwalipa fedha zao kwa wakati.

“Nikuombe Waziri Bashe, hawa wakulima ni masikini hawana lolote la kufanya, wamepima kahawa yao, imeuzwa hadi sasa hawajalipwa hawajui wataishi vipi, hebu tusaidie,” alisema Mwenisongole.

Katibu wa chama hicho cha ushirika, Sued Mgalla alipohojiwa na Waziri Bashe kama kahawa ya wakulima hao imeuzwa alijibu imeuzwa na fedha zipo benki.

Sued alisema fedha walizopata kwa kuuza kahawa ya wakulima hao zilikuwa benki kwa sababu bado walikuwa wanafanya mahesabu na ukaguzi wa madeni ya wakulima.

Bashe aliagiza polisi wamkamate kiongozi huyo pamoja na wenzake ili waweze kwenda kutoa fedha za wakulima walizodai zipo benki.

“Naomba hawa viongozi wasitoke ndani mpaka fedha za wakulima hawa zilipwe, na watafutwe viongozi wote wa ushirika, aiwezekani mkulima akope kwenye chama cha ushirika mifuko miwili ya mbolea auze kahawa yenye thamani Sh1.4 milioni halafu hela yake asipewe,” amesema Bashe.

Bashe amesema vitendo kama hivyo vimekuwa vikisababisha wakulima kuchukia ushiriki kwa makosa ya watu wachache wenye nia ovu.