Bashe ataka NFRA iongeze uwezo kuhifadhi chakula
Muktasari:
- Waziri Hussein Bashe ameitaka NFRA kuingia mikataba na wakulima ya kununua mazao yao ili wawe na uhakika wa soko na waweze kupata mahitaji muhimu kama mbolea na pembejeo wakati wakiwa shambani.
Dodoma. Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amezindua bodi ya wakurugenzi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) akiipa majukumu mawili likiwemo la kuhakikisha nchi ina chakula cha kujitosheleza kwa kipindi cha miezi sita.
Akizungumza leo Jumanne Aprili 18, 2023 jijini hapa, wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo,Waziri Bashe amesema bodi hiyo inatakiwa ibadilishe mtazamo kwa kuongeza ununuzi wa chakula kutoka tani 500,000 hadi kulenga kufikisha tani milioni tatu.
“Ninachotaka kwa bodi hii na menejiment mhifadhi chakula cha miezi sita. Najua sasa hapa kuna changamoto za mitaji lakini vyote hivi nendeni mkavijadili,” amesema Bashe
Waziri Bashe amewataka kuwa na mipango na kubadilika kifikra sio kusubiri ruzuku ya Serikali kuweza kujiendesha.
Pia,ameitaka kuingia mikataba na wakulima ili wawe na uhakika wa soko na waweze kupata mahitaji muhimu kama mbolea na pembejeo wakati wakiwa shambani.
“Nataka mwende mkanunue chakula mahindi na mpunga mapema. Tangazeni mkulima yoyote mwenye shamba kuanzia ekari 50 aje muingie naye mkataba jinsi ya kuja kununua mazao,”amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi hiyo, John Ulaya amesema watajitahidi kufanya kazi kwa bidii na maarifa kwani nia, sababu na uwezo wa kufanya hivyo wanao.
“Kwa kila ulichosema tunakubaliana nacho. Uturuhusu tuendelee kuja kuchukua miongozo kwako lakini nakuahidi katika kipindi kifupi tutaonesha mabadiliko,” amesema Ulaya.