Bashungwa: Uwekezaji Bandari ya Dar unaongeza ufanisi
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambeye pia ni Mbunge wa Karagwe, Innocent Bashungwa.
Karagwe. Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambeye pia ni Mbunge wa Karagwe, Innocent Bashungwa amesema uwekezaji na uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam utaongeza ufanisi kiutendaji na kuongeza mapato kwa nchi.
Ameeleza hayo leo Julai 17, 2023 wakati wa mwendelezo wa ziara yake Karagwe ya kuongoza wananchi na kukagua miradi ya maendeleo katika Kata za Chonyonyo, Chanika, Rugera na Kihanga.
“Tanzania tuna bandari ambayo ufanisi wake ulikuwa mdogo katika uendeshaji, ndio maana Serikali ikaamua kutafuta mwekezaji ambaye ataongeza ufanisi ili tuweze kupata mapato zaidi ambayo yataenda kutoa huduma za kijamii kwa Watanzania,” amesema Bashungwa.
Bashungwa amewatoa hofu Wananchi wa Mkoa Kagera kwa kueleza kuwa bandari haiuzwi wala haibinafishwi bali Serikali inaleta mwekezaji ambaye ataiendesha kwa makubaliano yatakayoongeza ufanisi kiutendaji.
“Ndugu zangu Wananchi naomba tuyapuuze yanayosemwa huko mitandaoni, katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi tuliahidi kutengeneza ajira milioni nane ndio maana tumeamua kukaribisha uwekezaji utakaozalisha ajira kwa Watanzania,” amesema.
Aidha, Bashungwa amesema uwekezaji huo ni moja ya mkakati wa kupanua wigo wa vyanzo vya mapato ili kuondoa usumbufu kwa Wananchi kwa kutozwa tozo nyingi ambazo zingelitumika kutekeleza miradi mbalimbali nchini.