Basi la Classic laua Songwe

Muktasari:
- Mtu mmoja raia wa Congo ambaye hajatambulika jina lake amefariki dunia katika ajali ya Basi aina ya Classic iliyohusisha malori matatu iliyotokea usiku wa kuamkia leo katika kijiji cha Ilonga kata ya Mahenje wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe na kujeruhi watu 18.
Songwe. Mtu mmoja raia wa Congo ambaye hajatambulika jina lake amefariki dunia katika ajali ya Basi aina ya Classic iliyohusisha malori matatu iliyotokea usiku wa kuamkia leo katika kijiji cha Ilonga kata ya Mahenje wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe na kujeruhi watu 18.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Janeth Magomi amesema leo Desemba 4, 2021 kuwa ajali hiyo imehusisha basi aina ya Man lenye namba 6884 AK05 ambalo limeteketea kwa moto na malori matatu yenye namba za usajili T.242 DPR aina ya DAF iliyokuwa inatokea Sumbawanga ikiwa na shehena ya mzigo wa Mahindi, gari namba T.368 DSW na gari lenye namba T.278 AfP iliyokuwa imebeba saruji kutoka Mbeya kuja Tunduma.
Amesema chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi aliokuwa nao dereva wa basi la Classic Hamis Mvagira (33), ambaye hakuchukua tahadhari wakati anapishana na magari mengine ambayo pia yalikuwa yanalipisha lori moja ambalo lilikuwa limeharibika eneo hilo.
Magomi amewataja majeruhi wa ajali hiyo kuwa ni pamoja na John Tarimo (53), Said Hassan (40), Pichisila Udote(48), Sapwe Ulukele (37), Mwelela Mbuyu (43), Fauta Matango (41), Teo Chibanda (40), Ngoi Kakasi (42) na Katembelela Mkonko (42).
Wengine ni Stewart Edward, Gisilane Kateka (54), Kotemba Mozinga (46), Fabian Kaonga (36), Mary Manyunga (40) na Chantul Nuumbi (31) na kuwa majerihi wanne Kati yao wamekimbizwa katika hospitali ya rufaa kanda ya Mbeya kwa matibabu zaidi.
Naye Mkurugenzi Wa hospitali ya Mkoa wa Songwe Ruhobdzyo Lulandala amesema hali za majeruhi waliobaki zinaendelea vizuri na kuwa baada ya uangalizi wa madaktari wataruhusiwa kurejea majumbani