Bei mpya ya petroli, dizeli hii hapa!

Muktasari:

Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji Tanzania (Ewura) imetangaza bei mpya za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kuanzia leo Jumatano Mei 4, 2022 ambapo bei ya nishati hiyo imeendelea kuongezeka.

Dodoma. Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji Tanzania (Ewura) imetangaza kuanza kutumika kwa bei mpya za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kuanzia leo Jumatano Mei 4, 2022 ambapo bei ya nishati hiyo imeendelea kuongezeka.

Kwa mujibu wa tangazo hilo lililotolewa Jumanne Mei 3, 2022 bei ya mafuta ya petroli katika Jiji la Dar es Salaam itakuwa Sh3, 148 na dizeli Sh3,264 kwa lita.

Mkoa wa Tanga bei ya petroli itakuwa Sh3,161 wakati dizeli itakuwa Sh3,264 huku mkoa wa Mtwara peroli ikiuzwa Sh3,177 na dizeli Sh3,309 kwa lita.

Ewura imesema bei ya mafuta ya taa katika Jiji la Dar es Salaam itakuwa ni Sh3112 kwa lita na kwamba  mabadiliko ya bei za mafuta nchini yanatokana na kuongezeka kwa bei ya nishati hiyo katika soko la dunia.