Bei ya mafuta Bara yapaa, Zanzibar walia na uhaba

Muktasari:

Jana Jumatano Novemba 7, 2018 bei ya petroli, dizeli na mafuta ya taa imeongezeka kwa asilimia 1.22 hadi asilimia 3.7 ikilinganishwa na Oktoba

Dar/Zanzibar. Wakati petroli, dizeli na mafuta ya taa yakipanda bei upande wa Tanzania Bara, huko Zanzibar yameadimika.

Ongezeko hilo la bei linatokana na kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo katika soko la dunia na gharama za usafirishaji.

Katika ongezeko lililotangazwa jana na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), bei ya rejareja ya mafuta yanayopita katika Bandari ya Dar es Salaam kwa dizeli imeongezeka kwa Sh81 kwa lita (sawa na asilimia 3.52) ikinganishwa na mwezi uliopita, Petroli imeongezeka kwa Sh29 (asilimia 1.22) na mafuta ya taa Sh34 (asilimia 1.5).

Kwa mujibu wa taarifa ya Ewura, bei ya jumla ya bidhaa hiyo imeongezeka kwa asilimia 3.71 (sawa na Sh80.9) kwa dizeli na petroli kwa asilimia 1.28 (sawa na Sh28.74) na mafuta ya taa kwa asilimia 1.50 (sawa na Sh34) kwa lita moja.

Septemba 5, mamlaka hiyo ilitangaza kushuka kwa bei za rejareja za petroli kwa Sh10, dizeli Sh19 na mafuta ya taa kwa Sh24 kwa lita moja.

Hata hivyo, katika bei zilizotangazwa jana, mafuta yanayopita katika Bandari ya Tanga yamezidi kupaa kwa wanunuzi wa rejareja huku ikiendelea kuwa ileile kwa wanunuzi wa jumla kwa kuwa hakuna shehena mpya iliyoingia. Wanunuzi wa rejareja wa mikoa ya Kaskazini ambayo ndio hutumia mafuta yanayopita katika bandari hiyo, watakumbana na ongezeko la Sh87 kwa lita moja ya petroli na Sh111 kwa dizeli.

Zanzibar walia

Wakati hayo yakijiri Tanzania Bara, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (Zura), Haji Kali alisema kuna upungufu mkubwa wa mafuta hayo visiwani humo.

Kali aliliambia Mwananchi kuwa kutokana na hali hiyo, hatua za kurejesha upatikanaji wa mafuta zimeanza.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Maji, Nyumba na Nishati, Ali Halil Mirza alisema meli ya kampuni ya Mafuta ya Zanzibar (ZP), imewasili visiwani na usambazaji umeshaanza.

Alisema tatizo hilo litamalizika kabisa pindi meli ya Mv United Spirit inayosafirisha mafuta kwenda visiwani humo itakapotengamaa. Kwa sasa meli hiyo iko katika hatua za mwisho za matengenezo ikitarajiwa kutengemaa wiki mbili zijazo.

Walaji walizwa na bei

Jijini Dar es Salaam, wananchi wameiomba Serikali kuweka ruzuku au kupunguza kodi katika mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kutokana na kupaa kwa bei ya bidhaa hiyo.

Mkazi wa Tabata, Sam Mshana anayefanya biashara ya duka, alisema mafuta ni bidhaa muhimu kwa maisha ya watu hususan katika usafirishaji wa vyakula, hivyo Serikali ingeangalia namna ya kupunguza kodi au kuweka ruzuku ili yasiathiri maisha ya watu.

Alex Pascal anayeendesha gari la mizigo alisema, “Mafuta yanatugombanisha na mabosi wetu, hapa nimejaza ya Sh40,000 nimepata lita 16 tu, zamani zingefika 20.”

Imeandikwa na Ephrahim Bahemu na Haji Mtumwa