Bei ya mafuta pasua kichwa

Thursday July 08 2021
mafutapic
By Ephrahim Bahemu

Dar es Salaam. Kwa kipindi cha mwaka mmoja bei ya mafuta ya petroli na dizeli nchini imepanda kwa zaidi ya Sh885, sawa na asilimia zaidi ya 50 kutokana na ongezeko la bei katika soko la duniani, kuongezeka kwa gharama za usafirishaji na mabadiliko ya tozo mbalimbali.

Juni mwaka jana, bei ya mafuta mkoani Dar es Salaam ilishuka hadi Sh1,520 kwa lita moja ya petroli, dizeli Sh1,546 na mafuta ya taa Sh1,568, ukilinganisha na zaidi ya Sh2,400 iliyotangazwa mwezi huu

Kuanzia Julai mosi bei ya ukomo iliyotangazwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) petroli imepanda bei kwa Sh156 kwa lita moja, dizeli kwa Sh142 na mafuta ya taa kwa Sh164.

Sababu za kupanda kwa bei ya mafuta, Ewura ilisema ni kuanza kutumika kwa bajeti mpya ya Serikali baada ya kupitishwa bungeni, ikianzisha tozo ya Sh100 kwa kila lita ya petroli, dizeli na mafuta ya taa na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia na kuongezeka kwa gharama za usafirishaji wa bidhaa hiyo.

Kutokana na mabadiliko hayo ya bei, Dar es Salaam ndipo mafuta hayo yanapatikana kwa bei rahisi ambapo bei ya kikomo kwa lita moja ya petroli ni Sh2,405, dizeli Sh2,215 na mafuta ya taa Sh2,121, huku wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma yanakopatikana kwa bei ghali zaidi, ni Sh2,649 kwa petroli, dizeli Sh2,459 na mafuta ya taa Sh2,365.

Wakimbilia nchi jirani

Advertisement

Kutokana na bei iliyopo nchini sasa, baadhi ya watumiaji wa vyombo vya moto, hususan bodaboda mjini wanalazimika kufuata mafuta katika nchi jirani.

Hali hiyo imeonekana katika maeneo ya Kabanga na Rusumo wilayani Ngara ambako watu wanavuka Rwanda na Burundi kufuata mafuta, huku Tunduma wilayani Momba, wakivuka kuyafuata katika eneo la Nakonde, Zambia.

Mmoja wa wamiliki wa gari mjini Tunduma, Elias Mahenge alisema amekuwa ananunua mafuta Zambia kwa Sh1,700.62 kwa lita moja, bei ambayo ni ndogo ukilinganisha na Sh2,526 kwa lita mjini Tunduma.

Richard Simyota, dereva wa bodaboda mjini Tunduma alisema kupanda kwa bei ya mafuta nchini imekuwa fursa kwao kununua bidhaa hiyo na kufanyia biashara mjini Tunduma.

Meneja wa Kituo cha Mafuta cha Ilasi mjini Tunduma, Happy Asajile alisema awali walikuwa na wateja wengi, lakini baada ya bei kupanda wateja wamepungua na inasemekana wanaenda Nakonde kununua mafuta ambako bei ni nafuu, hivyo kuna haja ya Serikali kuingilia kati.

Bei ya mafuta katika baadhi ya nchi jirani Zambia, Rwanda na Burundi inaelezwa kuwa pungufu ya hapa nchini kutokana na kuwa na kiwango kidogo cha tozo na kodi.

Pamoja na ongezeko hilo la bei ya mafuta, kwa nchi nyingine za Afrika mashariki – Kenya na Uganda kwa Tanzania bado yanauzwa nafuu.

Nchini Kenya petroli inauzwa kwa Ksh124.72 (Sh2,619) katika Bandari ya Mombasa, Nairobi Ksh127.14 (Sh2,669).

Nchini Uganda kwa wiki kadhaa zilizopita petroli ilikuwa inauzwa Ush4, 150) sawa na Sh2573.

Kodi na tozo

Kwa mujibu wa taarifa ya Ewura, bei ya mafuta sokoni kwa lita ni Sh1,087.27, dizeli Sh1,050.47 na mafuta ya taa ni Sh945.32 wakati gharama za usafiri, forodha na bima mpaka bandari ya Dar es Salaam, petroli ni Sh75.02, dizeli Sh47.12 na mafuta ya taa ni Sh116.59.

Kwa hesabu hiyo maana yake kabla ya kodi na tozo mbalimbali gharama ya petroli ikiwa bandari ya Dar es Salaam petroli ni Sh1,162.29, dizeli ni Sh1,097.59 na mafuta ya taa Sh1,061.91.

Mbali na Dar es Salaam, kwa taarifa ya sasa ya Ewura bei ya mafuta pamoja na bima kabla ya kodi na tozo nyingine za Serikali mafuta yanayopita katika bandari ya Mtwara gharama yake ni Sh1,179.91 kwa petroli na dizeli Sh1,126.30, huku ya bandari ya Tanga petroli ikiwa ni Sh1,219.67 na dizeli Sh1,143.29.

Kwa kuwa Serikali inahitaji tozo na kodi mbalimbali kwa ajili ya kuhudumia wananchi, kila lita moja ya petroli Serikali imeongeza kodi ya Sh892, dizeli Sh768 na mafuta ya taa Sh715 na kiwango hicho ni tofauti na tozo nyingine ambazo hutozwa na mamlaka mbalimbali za Serikali pamoja na gharama za usafiri, jumla ya tozo ni zaidi ya 20.

Mbali na makato ya kodi na tozo nyingine kupitia mafuta, pia hutozwa gharama za ghala, maendeleo ya reli, gharama za kushughulikia masuala mpakani, vipimo vya uzani, TBS, Tasac, Ewura, gharama za kuchelewa kwa meli, gharama ya uvukizi, upotevu wa mafuta baharini na nyingine kadhaa.

Ongezeko la nauli

Ongezeko hilo la bei ya mafuta limeanza kuchagiza mabadiliko ya nauli kwa kile wasafirishaji wanadai ni kutaka kufidia ongezeko la gharama za uendeshaji.

Gazeti hili jana lilikuwa na habari ya wasafirishaji wa abiria mkoani Arusha wamepandisha nauli za mabasi kati ya Arusha na Moshi kutoka Sh2,500 hadi 3,000, sambamba na nauli za njiani zote kwa wastani wa Sh500.

Mkurugenzi wa habari wa Taboa, Mustafa Mwalongo aliliambia gazeti hili kuwa licha ya bei ya mafuta kupanda kwa kipindi kirefu, mabadiliko ya nauli hayajafanyika tangu mwaka 2011, lakini kutokana na ongezeko la bei ya mafuta baadhi ya wamiliki wa mabasi wameanza kutaka maboresho ya nauli.

“Suala la kuboresha viwango vya nauli limekuwepo, lakini sasa huenda likajadiliwa na kufanyiwa maamuzi katika mkutano wetu mkuu wa Septemba au Novemba, maana kuna wanachama wetu wameanza kulalamika kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta,” alisema Mwalongo.

Mwalongo alisema endapo ajenda hiyo itapita katika mkutano mkuu maamuzi yake ndiyo yatakuwa madai halisi ya wao kuwasilisha serikalini na hapo zitateuliwa kampuni za kuonyesha hesabu za namna mafuta yalivyoathiri faida yao.

Advertisement