Bei ya mafuta yazidi kupaa Tanzania

Muktasari:

Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) imetoa bei mpya za mafuta zitakazoanza kutumika Jumatano ya Agosti 3,2022.

Dar es Salaam. Bei ya mafuta nchini Tanzania, imepanda tena mwezi huu na kuivuka ile ya Julai 2022 ambapo petroli imepanda kwa Sh190 kwa kila lita na Sh179 kwa kila lita ya dizeli huku mafuta ya taa yakipanda kwa Sh323 kwa kila lita kwa Jiji la Dar es Salaam.

 Katika taarifa iliyotolewa leo Jumanne Agosti 2, 2022 na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), bei ya rejareja jijini Dar es Salaam itakuwa Sh 3,410 kwa lita moja ya petroli na Sh3,322 kwa dizeli huku mafuta ya taa yakifika Sh3,765.

Kutokana na bei hiyo mpya ambayo itaanza kutumika kesho, petroli imepanda kwa Sh190 kwa kila lita ambapo mwezi uliopita iliuzwa Sh3,220 na Sh179 kwa kila lita ya dizeli ambayo mwezi uliopita iliuzwa Sh3,143 huku mafuta ya taa yakipanda kwa Sh323 kwa kila lita ambako mwezi uliopita yaliuzwa Sh3,442.

Ewura imesema bei hizo mpya ambazo zitaanza kutumika kesho Jumatano Agosti 3, 2022 zimejumuisha ruzuku ya Sh100 bilioni iliyotolewa na Serikali vinginevyo, lita ya petroli ngeuzwa Sh3,630 na dizeli Sh3,734 jijini Dar es Salaam.

“Bei za Mafuta katika soko la dunia zimeendelea kuongezeka na kusababisha bei za mafuta katika soko la ndani kuongezeka pia."

"Ili kupunguza madhara ya ongezeko hilo katika soko la ndani, Serikali imetoa ruzuku ya bilioni 100 kwa ajili ya bei za mafuta hapa nchini kwa Agosti 2022. Serikali kwa kutoa ruzuku hiyo, imepunguza bei za bidhaa za mafuta kwa Agosti 2022," imeeleza taarifa