Bei ya mafuta yazidi kupaa

Muktasari:

Wakazi wa Dar es Salaam sasa wataanza kulipa Sh3,220 kwa lita ya petroli na 3,143 kwa dizeli huku wale wa wilayani Kyerwa mkoani Kagera wakinunua lita moja ya petroli kwa Sh3,458 na dizeli kwa 3,381.

Dar es Salaam. Bei ya mafuta imepanda tena mwezi huu na kuivuka ile ya Mei, iliyokuwa kubwa zaidi katika historia ya Tanzania kiasi cha kuilazimu Serikali kutoa ruzuku.

Mei, bei ya petroli ilifika Sh3,148 jijini Dar es Salaam ikipanda kwa Sh287 kutoka Aprili kwa kila lita moja huku dizeli ikipanda kwa Sh566 kutoka Sh2,692 hadi Sh3,258 katika kipindi hicho.

Katika taarifa iliyotolewa leo Jumanne Julai 5, 2022 na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), bei ya rejareja jijini Dar es Salaam itakuwa Sh3,220 kwa lita moja ya petroli na Sh3,143 kwa dizeli huku mafuta ya taa yakifika Sh3,442.

Maumivu yatakuwa makali mkoani Kagera hasa katika Wilaya ya Kyerwa ambako lita moja ya petroli itauzwa Sh3,458 na dizeli Sh3,381 na mafuta ya taa ni Sh3,679.

Ewura imesema bei hizo mpya ambazo zitaanza kutumika kesho Jumatano zimejumuisha ruzuku ya Sh100 bilioni iliyotolewa na Serikali vinginevyo, lita ya petroliingeuzwa Sh3,497 na dizeli Sh3,510 jijini Dar es Salaam wakati Kyerwa ingekuwa Sh3,735 kwa petrol na Sh3,748 kwa dizeli. Mafuta ya taa hayana ruzuku.

"Katika kukabiliana na ongezeko la bei ya mafuta hapa nchini Serikali imetoa ruzuku nyingi ya Sh100bilioni kwa mwezi Julai. Ruzuku hiyo imeelekezwa katika mafuta ya petroli na dizeli na kiasi kikubwa kimeelekezwa katika dizeli kwa lengo la kudhibiti mfumko wa bei," imeeleza taarifa ya Ewura.

Mwezi uliopita, lita ya petrol iliuzwa Sh2,994 na dizeli Sh3,131 mkoani Dar es Salaam huku Kyerwa ikiwa Sh3,539 kwa petroli na Sh3,232 kwa lita ya dizeli.