Bei ya mbolea yashuka

Rais Samia Suluhu Hassan akizindua Mpango wa Ruzuku ya Mbolea utakaowawezesha wakulima kupata nafuu ya bei za mbolea katika msimu wa kilimo 2022/2023.

Muktasari:

  • Mpango wa ruzuku ya mbolea msimu wa kilimo 2022/2023 wazinduliwa, waelezwa kuleta nafuu kubwa kwa wakulima

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amezindua Mpango wa Ruzuku ya Mbolea utakaowawezesha wakulima kupata nafuu ya bei za mbolea katika msimu wa kilimo 2022/2023.

Mkuu huyo wa nchi amefanya uzinduzi huo leo Jumatatu Agosti 8, 2022 wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya wakulima Nanenane inayoadhimishwa kitaifa mkoani Mbeya.

Akizungungumza wakati wa uzinduzi huo, Waziri wa Kilimo Hussen Bashe amesema mpango huo unalenga kuwaondolea mzigo wakulima ambao wamekuwa wakikutana nao kwa muda mrefu kutokana na changamoto za bei za mbolea.

Mpango huo wa rukuzu unafanya bei ya mbolea ya DAP kuuzwa Sh70, 000 kutoka Sh131,000 ya awali huku mbolea ya urea ikiuzwa Sh70,000 kutoka Sh124,734.

“Kupitia mpango huo mbolea zote za kupandia zinazofahamika kama NPK zilizokuwa zikiuzwa kwa Sh122, 695 zitauzwa kwa Sh70000 huku ruzuku ya Serikali ikiwa Sh52,695,” amesema Bashe.