Bei ya petroli yagonga Sh2,861

Muktasari:

  • Wakati Serikali ikitangaza kurejesha Sh100 katika mafuta, watumiaji wa nishati hiyo watalazimika kufunga mkanda kutokana na bei kuendelea kupaa.

Dodoma. Wakati Serikali ikitangaza kurejesha Sh100 katika mafuta, watumiaji wa nishati hiyo watalazimika kufunga mkanda kutokana na bei kuendelea kupaa.

Bei ya nishati hiyo inapanda wakati wananchi wakilalamika kupaa kwa bei za bidhaa mbalimbali za vyakula hasa wakati huu wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Hata hivyo, vita vya Russia na Ukraine ambavyo vimedumu kwa zaidi ya mwezi sasa navyo vinatajwa kupandisha bei ya nidhati hiyo kwenye soko la dunia. Russia ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa mafuta dunia.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Jumanne Aprili 5, 2022 Mkurugenzi wa Petroli wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Gerald Maganga amesema kuanzia kesho Jumatano, Aprili 6,2022 bei mpya ya petrol kwa mafuta yanayopokelewa kupitia Bandari ya Dar es salaam itakuwa Sh2,861 kutoka Sh 2,540 ikiwa ni ongezeko la Sh321.

Kwa upande wa dizeli bei mpya itakuwa Sh2,692 kutoka Sh2,403 ya sasa ikiwa ni ongezeko la Sh289. Bei ya mafuta ya taa itapanda kutoka Sh2,208 hadi Sh2,682 ikiwa ni wastani wa Sh474.

Maganga amesema mafuta ambayo yatapitia Bandari ya Tanga, bei ya petrol itakuwa Sh2,848 kutoka Sh2,563 ikiwa ni ongezeko la Sh285.

Kwa upande wa dizeli bei itaongezeka kutoka Sh2,484 hadi Sh2,779 ikiwa ni ongezeko la Sh295 kwa lita moja.

Mafuta ambayo yatapokewa kupitia Bandari ya Mtwara bei ya petrol kwa lita moja itakuwa Sh2,678 kutoka Sh2,577 ikiwa ni ongezeko la Sh100.

Bei ya dizeli kwa lita moja itakuwa Sh2,811 kutoka Sh2,530 ikiwa ongezeko la Sh281.

Hata hivyo, Maganga amesema kuwa bei hizo zimejumuisha tozo ya Sh100 ambayo Serikali ilitangaza kuiondoa mwezi Machi, 2022 kabla ya Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza kuirejesha akisema utaribu wa kuindoa haukufuatwa kwa kuwa fedha hiyo ilishapangiwa bajeti.