Benki ya Dunia yaahidi neema zaidi utafiti Tanzania
Muktasari:
- Benki ya Dunia imesema itaendelea kutoa ushirikiano wa kifedha na utalaamu Tanzania kwa ajili ya kufanya utafiti baada ya kuridhishwa na mwenendo wa miaka 15 ya ufadhili wake.
Dar es Salaam. Benki ya Dunia (WB) imesema itaendelea kutoa ushirikiano wa kifedha na utalaamu Tanzania kwa ajili ya kufanya tafiti baada ya kuridhishwa na mwenendo wa miaka 15 ya ufadhili wake.
Licha ya kutoeleza imeweka kiasi gani katika kipindi hicho, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), imesema tayari imeshapokea mkopo nafuu wa dola 82 milioni (Sh200 bilioni) za benki hiyo kwa programu ya miaka mitano (2022/23-2026/27) utakaosaidia kuimarisha miundombinu ya huduma za tafiti.
Benki hiyo kupitia Mradi wa Utafiti wa Kupima Hali ya Maisha zinazojumuisha tafiti za Kilimo (LSMS-ISA) imekuwa ikisaidia ufadhili wa kifedha na utalaamu katika ukusanyaji wa taarifa na uwepo wa takwimu za kisekta tangu mwaka 2008.
Katika maadhimisho ya ufadhili huo, kitengo cha takwimu cha benki hiyo jana ilikutanisha watalaamu wa taasisi za tafiti kutoka zaidi ya mataifa 10 ya Afrika na Asia yanayofadhiliwa katika mradi huo kufanya kutathmini ya miaka 15 na kutazama mwelekeo mpya.
Akizungumza katika kongamano hilo, Meneja mwandamizi wa uzalishaji wa takwimu kutoka kitengo hicho cha Benki ya Dunia, Calogero Carletto alisema;
“Tunajisikia faraja kuona ufadhili wa WB katika tafiti umeonyesha matokeo chanya katika miaka 15 sasa, ziko changamoto za ongezeko la joto kutokana na mabadiliko ya tabianchi, lakini muhimu ni kuwa na sera zitakazosaidia kupunguza athari hizo.
“Siwezi kusema kiasi gani tuliwekeza ila ilikuwa ni zaidi ya mamilioni ya dola pamoja na utalaamu. Tunashuhudia sera mbalimbali zimeanzishwa kupitia tafiti hizo, Serikali imefikia maeneo yenye uhitaji. Kwa hiyo tutaendelea kushirikiana zaidi na Tanzania kwenye tafiti miaka ijayo,” amesema.
Kongamano hilo lilihusisha uwasilishaji wa tafiti tatu kati ya 12 zinazogusa usalama wa chakula, hali ya kipato na huduma za lishe bora.
Akieleza changamoto za uchakataji na uwasilishaji wa taarifa, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Repoa Dk Donald Mmari amesema kuna kiwango kidogo cha uchakataji na usambazaji wa taarifa zinazotokana na tafiti hizo kili kufikia walengwa.
“Ni kweli Serikali inatahidi na kumekuwapo na ongezeko la uzalishaji wa takwimu lakini uchambuzi wa takwimu hizo ili kujua maana yake nini katika maendeleo bado uko chini, Serikali haijawekeza kwa taasisi za utafiti ili kuchambua na kuona maeneo gani yanahitaji tafiti ndogo.
“Utafiti mdogo unaweza kuhitajika ili kujibu baadhi ya maswali yanayotokana na uchambuzi huo kabla ya kusambaza kwenye makundi yenye mahitaji tofauti kwa ajii y matumizi, itasaidia sana kuleta tija.”
Akijibu hoja hiyo, Mkurugenzi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dk Albina Chuwa amesema ofisi hiyo imetenga bajeti kwa ajili ya ushirikishaji taasisi za utafiti binafsi kupitia mkopo huo wa dola 82milioni.
“Katika mkopo huo tutaimarisha mifumo ya ukusanyaji takwimu ngazi za wizara, taasisi na sekta binafsi. Pia tutajenga jenga la ofisi za NBS Lindi, Simiyu na Pemba. Kwa hiyo tutahakikisha tunaendelea kuimarisha zaidi huduma za takwimu,”alisema.
Kuhusu usambazaji na uwezo wa walengwa kutafsiri takwimu hizo, Dk Chuwa amesema hali kwa sasa inaridhisha kwa zaidi ya asilimia 70.
“Tathimini ya ufutiliaji wa matumizi ya takwimu Afrika chini ya Benki ya Dunia mwaka 2018/19 inaonyesha Tanzania ilishika nafasi ya pili kwa hiyo ninaamini tafiti zinawafikia na wanazielewa namna ya kuzitumia katika mahitaji yao,” alisema.
Kupitia mradi huo, Tanzania imepata ufadhili wa kifedha na utalaamu katika uandaaji wa tafiti mbili za mapato na matumizi ya kaya binafsi 2022/12 na ule wa 2017/18.