Benki ya Dunia yachunguza madai ya mauaji Ruaha

Muktasari:

Benki ya Dunia (WB) inachunguza madai ya mauaji, ubakaji na kuhamishwa kwa wanavijiji wanaoishi maeneo yenye vivutio vya utalii yanayofadhiliwa na benki hiyo nchini, Mwananchi limebaini.


Dar es Salaam. Benki ya Dunia (WB) inachunguza madai ya mauaji, ubakaji na kuhamishwa kwa wanavijiji wanaoishi maeneo yenye vivutio vya utalii yanayofadhiliwa na benki hiyo nchini, Mwananchi limebaini.


Uchunguzi huo unatokana na tuhuma zilizotolewa na taasisi ya Oakland Institute, iliyofanya uchunguzi wa maeneo unakotekelezwa Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (Regrow), ambao Benki ya Dunia imetoa ufadhili wa Dola za Marekeni 150 milioni (Sh375.75 bilioni).


Mradi huo ulilenga kuongeza maradufu ukubwa wa hifadhi hiyo iliyo umbali wa kilomita 130 kutoka Iringa mjini. “Tunachukulia madai haya kwa uzito mkubwa na tunaangalia, tunafanyia kazi jopo la mkopaji na benki. Ujumbe uliochaguliwa ulikwenda nchini Tanzania kuitikia malalamiko yaliyopokewa, kupata taarifa za awali.


“Kama mkopaji hatekelezi mradi kulingana na viwango vya kimazingira na kijamii, tunataka kujua na zaidi sana tunataka kufanyia kazi suala hili haraka,” alisema msemaji wa Benki ya Dunia alipowasiliana kwa barua pepe na gazeti la The Citizen.


Juhudi za kuipata Serikali kuzungumzia taarifa hiyo jana hazikufanikiwa, baada ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki kumtaka mwandishi kumtafuta Msemaji wa Wizara, John Mapepele ambaye naye alimtaka mwandishi amwandikie maswali kwa barua pepe kwanza.


Taarifa iliyochapishwa kwenye gazeti la mtandao la The Guardian Septemba 28, 2023 imeeleza kuwa, wanavijiji wa vijiji vilivyopo karibu na hifadhi ya Ruaha waliwaambia watafiti wa taasisi ya Oakland kuwa, askari waliua, kupiga wafugaji na wavuvi, huku pia kukiwa na madai ya kubaka wanawake walioingia katika hifadhi hiyo.


Hata hivyo, gazeti hili toleo la Mei 18, 2021 liliripoti kuhusu sakata la madai ya kuuawa kwa wananchi watatu waliodaiwa kwenda kuvua samaki ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, kukiwa na taarifa zenye kukinzana kati ya Jeshi la Polisi na Serikali ya mkoa.


Aliyekuwa mbunge wa Mbarali, Francis Mtega alidai bungeni kuwa, watu hao William Estoberi Nundu (38), Sandu Masanja (28) na Ngusa Salawa (14) waliuawa na askari wa wanyamapori.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya (RPC) wakati huo, Ulrich Matei, alisema watu hao wanaodaiwa kuingia kwenye hifadhi Aprili 23, mwaka huu, kufanya ujangili wa kuvua samaki, waliuawa na wanyama wakali na si askari kama inavyodaiwa.


Wakati Kamanda Matei akisema hivyo, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, ambaye kwa sasa amehamishiwa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alisema askari wawili wa hifadhi hiyo wanashikiliwa na polisi kwa uchunguzi zaidi kuhusu tukio hilo.


Kamanda Matei alisema Nundu alikutwa amebaki kichwa kilichokuwa na majeraha kadhaa, kiwiliwili chake kililiwa na mamba ambao kwa taarifa za awali kutoka kwa wananchi zinadai kuwa, eneo hilo lina mamba na viboko wengi.


Pia, alisema Masanja alikutwa amelala kifudifudi kwenye korongo la maji, huku shingo ikiwa inachezacheza wakati Ngusa alikutwa kwenye dimbwi la maji.


Kamanda Matei aliwaambia waandishi wa habari kuwa vifo vya watu hao ambao miili yao ilikutwa ndani ya hifadhi vilitokana na kushambuliwa na wanyama wakali.


Kwa mujibu wa ripoti ya uchunguzi ya Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Mbarali, Telesphor Sambi, Ngusa na Masanja walikufa kwa kuzamishwa kwenye maji, hivyo kukosa hewa na kushindwa kupumua hadi wakapoteza maisha. “Kichwa chake kilikuwa na matundu manne (yanayoaminiwa kuwa ya meno ya mamba) katika pande zote mbili za kichwa. Matundu mengine manne yalikutwa kwenye ngozi na matundu matatu kwenye fuvu, yaliyotoboa hadi ubongo,” alisema Dk Sambi.


huku akisisitiza kuwa wananchi hao wameuawa kwenye Kijiji cha Nyeregete wilayani Rujewa.


“Kumetokea mauaji ya wananchi yaliyotekelezwa na wanaodhaniwa kuwa ni askari wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha,” alisema na kuongeza kuwa kuna wananchi wengine watatu waliokuwa pamoja waliokufa, hawafahamiki mahali walipo.