Bibi anayemnyonyesha mjukuu wake baada ya mwanawe kufariki

Thabita Mgaya (50) akimnyonyesha mjukuu nyumbani kwake  Mtaa wa Chamoto Mamlaka ya Mji mdogo wa Mugumu wilaya ya Serengeti.Picha na Athon Mayunga

Muktasari:

  • “Ni jambo linalonistaajabisha hata mimi kuona maziwa yanatoka na ninaweza kumnyonyesha mjukuu wangu baada ya mama yake kufariki dunia siku moja tu baada ya kujifungua,”

Serengeti. “Ni jambo linalonistaajabisha hata mimi kuona maziwa yanatoka na ninaweza kumnyonyesha mjukuu wangu baada ya mama yake kufariki dunia siku moja tu baada ya kujifungua,”

Hiyo ni kauli ya Tabitha Mgaya (50), mkazi wa mtaa wa Chamoto mjini Mugumu wilayani Serengeti mkoani Mara, aliyejikuta akilazimika kumnyonyesha mjukuu wake baada ya binti yake aliyekuwa na umri wa miaka 13 kufariki dunia siku moja baada ya kujifungua.

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu nyumbani kwake mwishoni mwa wiki iliyopita, Tabitha anasema amelazimika kubeba dhamana siyo tu ya kumlea mjukuu wake, bali pia kumnyonyesha licha ya kuacha kunyonyesha miaka 10 iliyopita.


Tukio lilivyoanza

“Desemba 28, 2020 ni siku iliyobadilisha historia ya maisha ya familia yangu. Hii ndiyo siku mtoto wangu wa kike Sarah alipofariki dunia muda mfupi baada ya kujifungua kwa upasuaji akiwa na miaka 13,” anaanza kusimulia

Anasema kifo cha binti yake kilimwachia jukumu la malezi ya mjukuu wake aliyekuwa na umri wa siku moja huku akitafakari namna ya kumudu kazi hiyo kutokana na uwezo mdogo wa kiuchumi wa familia yake.

“Mkuu wa Wilaya, Nurdin Babu (amehamishiwa wilaya ya Longido) alijitolea kulipia gharama ya maziwa kila mwezi ikiwa ni sehemu ya kusaidia malezi ya mjukuu wangu. Namshukuru Mungu alifanya hivyo kwa miezi minne mfululizo kabla ya kusitisha,” anasema

Anasema baada ya huduma ya maziwa kusitishwa, aliamua kuanza kumnywesha uji mjukuu wake kutokana na familia kutomudu kulipia gharama ya maziwa kila mwezi.

“Nadhani utumbo wa mtoto ulikuwa bado hauko tayari kwa uji kwa sababu alianza kuharisha hadi nikasitisha kwa hofu ya kumpoteza,” anasema Tabitha

Anaongeza; “Nikiwa katikati ya mtanziko wa mawazo ya namna ya kumlea mjukuu wangu; siku moja wazo la kumnyonyesha likaniijia. Siku za mwanzoni mtoto alionekana kutotosheka kwa sababu maziwa yalikuwa yanatoka kidogo kidogo lakini sikukata tamaa nikaendelea tu kumnyonyesha,”

Anasema kadri siku zilivyoendelea, alianza kuhisi maziwa yakijaa na kuwa mengi kiasi cha mtoto kunyonya hadi kutosheka.

“Licha ya mshangao wangu na watu wengine, niliendelea kumnyonyesha mjukuu wangu ka bidii kwa sababu mjukuu wangu hakupata madhara yoyote huku mwili wake ukianza kunawiri kwa kupata lishe ya kutosha…namshukuru Mungu nimemtunza na kumkuza hadi sasa amefikisha miezi 10,” anasema Tabitha huku akiona fahari kwa uamuzi wake iliyookoa maisha ya mjukuu wake

Mmoja wa majirani, Hadija Suleiman anasema “Hili la bibi aliyeacha kunyonyesha miaka 10 iliyopita kupata maziwa na kumnyonyesha mjukuu wake ni tukio la kustajaabisha; kwa akili za kawaida naweza kusema haya ni maajabu ya Mungu,” anasema Hadija


Wataalamu wa afya

Akizungumza na Mwananchi kuhusu mama aliyeacha kunyonyesha miaka 10 iliyopita kupata maziwa na kumnyonyesha mtoto, Dk Daniel Safi kutoka Hospitali ya Wilaya ya Serengeti anasema ni jambo la kawaida kwa homoni za mwili wa mama aliyewahi kunyonyesha kusisimka na kutengeneza maziwa. “Kitendo cha mtoto kunyonya maziwa ya mwanamke aliyewahi kunyonyesha huamsha hisia na kumbukumbu ambazo husisimua homoni zinazohusika na utengenezaji wa maziwa na kustua matiti na kuanza kutoa maziwa,” anasema Dk Safi

Anasema mtoto akiendelea kunyonya maziwa ya mwanamke aliyewahi kunyonyesha huku mama anayenyonywa anapata lishe bora, hasa vyakula byenye vitamin C na Protini, basi mwili hujitengenezea maziwa mengi yanayofaaa kumnyonyesha mtoto bila tatizo lolote.

Mtaalamu wa lishe Mkoa wa Mara, Paulo Makali, anasema ni kawaida kwa mwili wa binadamu kupata msisimko na hisia pale jambo alilowahi kufanya, kuona au kusikia linapotendeka.

“Hali hii ndiyo inayotokea hata katika masuala ya kujamiiana. Kuna wakati mmoja kati ya wanaohusika kwenye tendo la ndoa hayuko tayari; lakini kadri mwenzake anavyomgusa hisia zake huamka. Hivyo kitendo cha mama huyo kunyonywa matiti kiliamsha hisia yake na hivyo kuwezesha mwili kutengeneza maziwa,” anasema Makali

Hata hivyo, mtaalamu huyo anakiri kuwa ni mara yake ya kwanza kukutana na tukio la mwanamke aliyeacha kunyonyesha miaka 10 mwenye umri wa miaka 50 kupata uwezo wa kunyonyesha mtoto.

“Kisayansi matukio ya aina hii yanatupatia fursa ya kufanya utafiti na uchunguzi zaidi,” anasema Makali