Bima ya afya kwa wote kuteka mjadala bungeni kesho
Muktasari:
- Wizara ambazo zitasoma bajeti yake wiki hii ni Afya, Uchukuzi, Mifugo na Uvuvi, na watamalizia na Wizara ya Maliasili na Utalii ambayo bajeti yake itavuka hadi wiki iijayo.
Dodoma/Dar. Wakati Mkutano wa Tatu wa Bunge la Bajeti ukitarajiwa kuendelea kesho, wiki hii inatarajiwa kuwa ya moto kutokana na wizara zinazowasilisha bajeti zao kuwa na mguso wa moja kwa moja kwa wananchi.
Wizara ambazo zitasoma bajeti yake wiki hii ni Wizara ya Afya, Uchukuzi, Mifugo na Uvuvi, huku mwendelezo ukimalizika na Wizara ya Maliasili na Utalii, ambayo bajeti yake inatarajiwa kuendelea hadi wiki ijayo.
Hadi sasa, wizara 15 zimeshapitisha bajeti zake, zikiwamo za Maji, ambayo iliibua mijadala mikali, ikifuatiwa na Wizara ya Elimu, ambayo licha ya kuwa na wachangiaji wengi, hoja zake zilijikita kwenye ushindani na maboresho ya utoaji wa elimu.
Kutokana na maswali yanayojitokeza katika vikao vinavyoendelea, mara nyingi ni suala la Bima ya Afya kwa Wote, uhaba wa watumishi wa afya, ujenzi na upanuzi wa viwanja vya ndege, ulipaji wa fidia, kwa mfano wa eneo la Kipunguni, Dar es Salaam, maeneo ya malisho, migogoro kati ya wakulima na wafugaji, pamoja na vifo vinavyotokana na tembo na mamba.
Maswali hayo ndiyo yanayoonesha kuwa katika mijadala ya bajeti za wizara hizo huenda ikawa mikali zaidi.
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko, akizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Mei 10, 2026, amesema matarajio katika sekta ya afya kwa bajeti ya mwaka 2026/27 ni kuona Serikali ikija na suluhisho la mambo manne muhimu ili Watanzania wawe na uhakika wa huduma za afya pindi wanapohitaji.
Amefafanua kuwa mambo hayo ni ajira za watumishi wa afya, Bima ya Afya kwa Wote, ununuzi wa vifaa vya kisasa hasa kwa hospitali za ngazi ya msingi, na maboresho katika tiba za saratani.
“Tumeona bajeti ya mwaka 2025/26 ilivurugika kutokana na Marekani kuondoa baadhi ya misaada, jambo lililosababisha watumishi 1,800 kupoteza ajira. Aidha, uchaguzi na vurugu zilizofuata pia zilisababisha baadhi ya mambo kutotekelezwa kwa ukamilifu,” amesema Dk Nkoronko.
Amesema kuongeza idadi ya watumishi wa afya ni jambo la msingi, kwa sababu vituo vingi vya afya vimejengwa lakini havina watumishi. Tanzania ina upungufu wa watumishi wa sekta ya afya unaofikia wastani wa asilimia 56 hadi 65, jambo linalosababisha huduma kuwa duni katika baadhi ya maeneo.
“Natamani bajeti ijielekeze pia kwenye ununuzi wa vifaa kwa ajili ya wagonjwa wa dharura, hasa majeruhi katika hospitali za vijijini. Vilevile, maboresho ya tiba za saratani ni muhimu ili huduma za afya zipatikane hadi ngazi za wilaya, lengo likiwa kuwahudumia Watanzania kwa viwango na ubora,” amesema.
Wakati wa mkutano mmoja, Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, aliwahi kusema bajeti ya wizara yake itazingatia kuboresha huduma za afya ya msingi, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, pamoja na kuimarisha miundombinu ya hospitali za rufaa na vituo vya afya nchini.
Pia, itazingatia kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya magonjwa ya mlipuko na yasiyoambukiza, kuboresha huduma za afya kupitia mifumo ya kidijitali, na kuongeza huduma za kitaalamu na ubingwa bobezi.
Wizara ya Uchukuzi yatazamwa kwa fidia
Kwa upande wa Wizara ya Uchukuzi, ambayo imepangiwa siku moja ya mjadala, masuala ya fidia kwa waliopisha upanuzi na ujenzi wa viwanja vya ndege yanatarajiwa kutawala mjadala.
Mbunge wa Segerea (Chaumma), Agnesta Kaiza, mwishoni mwa wiki aliuliza swali kwa Waziri Mkuu kuhusu lini wananchi wa Mtaa wa Kipunguni watapewa fidia baada ya nyumba zao kutathminiwa kwa muda mrefu.
Akijibu, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, alikiri kuwa madai hayo yamekuwa ya muda mrefu na kueleza kuwa Serikali inajitahidi kulipa kadri ya upatikanaji wa fedha.
Wabunge wengine wa Mkoa wa Njombe pia wanashirikiana kushinikiza ujenzi wa uwanja wa ndege na kuhakikisha maeneo mengi yasiyo na viwanja vya ndege yanapata miundombinu hiyo muhimu.
Matarajio ya sekta ya mifugo
Katibu wa Chama cha Wafugaji Tanzania, Joshua Lugaso, ametoa matarajio manne katika bajeti ijayo, mkakati wa kupata madume bora, upatikanaji wa maji kwa mifugo, kuongeza maeneo ya malisho, na ruhusa kwa Serikali kurejesha mapori yaliyopoteza sifa ili yawe malisho.
Lugaso amesema hatua hizo zitasaidia kuondoa migogoro ya muda mrefu kati ya wafugaji na wakulima.
Malalamiko Wizara ya Maliasili na Utalii
Kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii, wabunge wameeleza malalamiko kuhusu vifo vya ndugu zao kutokana na wanyama pori na uharibifu wa mazao kutokana na tembo.
Wakiuliza maswali bungeni kwa nyakati tofauti, baadhi walisikika wakisema wanamsubiri Waziri aje ajibu hoja zao atakapowasilisha bajeti yake bungeni.
Baadhi wamesisitiza mara kadhaa umuhimu wa Serikali kuunda mkakati wa kushughulikia wanyama pori kama tembo na mamba, ingawa Serikali haijaweka wazi suluhisho la kudumu, bali imesema askari wa wanyama pori wanaendelea kupambana na wanyama hao na kutoa tahadhari kwa wananchi.