Binti anayedaiwa kuzaa na baba yake akana madai

Muktasari:

  • Kashfa ya baba anayedaiwa kumpa mimba na kimzalisha watoto watatu  binti yake wa kumzaa, Mabula Masunga Jiumbi inaonekana kuchukua sura mpya baada ya binti yake huyo, kudaiwa kugeuka mahakamani na kukana madai hayo.

Rufiji Pwani. Kashfa ya baba anayedaiwa kumpa mimba na kimzalisha watoto watatu  binti yake wa kumzaa, Mabula Masunga Jiumbi inaonekana kuchukua sura mpya baada ya binti yake huyo, kudaiwa kugeuka mahakamani na kukana madai hayo.

Binti huyo, Mwashi Mabula Masunga alikana madai hayo kinyume na maelezo yake aliyoyatoa polisi akikiri kuzaa na baba yake, wakati akitoa ushahidi baada yake kupandishwa kizimbani na kusomewa shtaka moja la kufanya ngono na binti yake kinyume cha sheria.

Msimamo huo wa binti huyo ulionekana kumvuruga mwendesha mashtaka wa Serikali, Mkaguzi wa Polisi (Inspekta), Justine Sanga na kumuuliza iwapo yuko tayari kuwajibika kwa kuidanganya Mahakama, iwapo vitafanyika vipimo vya Kisayansi na kuthibitisha  kuwa amezaa na baba yake; naye akakubali kuwa yuko tayari.

Jinsi ilivyokuwa hatua kwa hatua kwa hatua

Mabula ambaye ni mkazi wa Kitongoji cha Mbambe, Kijiji cha Mbunju-Mvuleni, Kata ya Mkongo, Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani, alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Rufiji na kusomewa shtaka linalomkabili juzi Jumatatu saa 9:30 alasiri.

Awali, amefikishwa mahakamani hapo saa 4:09 asubuhi akiwa ndani ya gari ya Polisi aina ya Toyota Land Cruiser Pickup, rangi ya Samawati akiwa pamoja na watuhumiwa wengine.

Baada ya kufikishwa mahakamani hapo yeye pamoja na watuhumiwa wenzake wengine walishushwa wakiwa wamefungwa pingu wawili wawili wakaingizwa katika mahabusu ya mahakama hiyo,  kusubiri taratibu za kusajiliwa kwa kesi zao kisha wapandishwe kizimbani kusomewa mashtaka yanayomkabili.

Baada ya dakika 51, yaani saa 11:00 jioni mtuhumiwa huyo na wenzake hao walichukuliwa na askari Polisi kutoka mahabusu na kupakizwa ndani ya gari hilo la Polisi lililowafikisha mahakamani hapo na kisha kuondoka nao kwenda Kituo cha Polisi Utete.

Hata hivyo baadaye Mabula  alirudishwa mahakamani akiwa na mwenzake mmoja huku wakiwa wamefungwa pingu kwa pamoja na kupelekwa tena mahabusu ya mahakani hapo alipopandishwa kizimbani na kisha kusomewa shtaka hilo.

Shtaka na maelezo ya awali ya kesi

Mahakamani, Mabula ambaye hakuwa na Wakili wa kumwakilisha, aliieleza mahakama kuwa lugha ya Kiswahili haimudu vizuri isipokuwa lugha yake ya asili ya Kisukuma.

Hivyo, wakati akisomewa shtaka lake na kisha maelezo ya awali ya kesi, mwendesha mashtaka na Hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Flora Mujaya mara kadhaa walikuwa wakilazimika kurudiarudia maelezo au swali ili aelewe na waweze kuelewa majibu yake.

Hata hivyo, ingawa hajui lugha ya Kiswahili kuizungumzia vizuri wala kuiosoma, lakini kabla ya kusomewa shtaka, Hakimu alielekeza upande wa mashtaka kumpatia mshtakiwa hati ya mashtaka japo iliandikwa kwa Lugha ya Kiingereza (kwa sababu ni haki yake kupewa nakala).

"Mshtakiwa umepewa hiyo nakala japo imeandikwa kwa Kiingereza lakini kilichoandikwa humo ndicho mwendesha mashtaka anachokisoma kwa Kiswahili," amesema Hakimu Mujaya baada ya Inspekta Sanga kumpatia mshtakiwa huyo nakala ya hati ya mashtaka.

Inspekta Sanga alianza kumsomea shtaka na maelezo na majibu ya mshtakiwa baada ya kuwa amefafanuliwa kila pale ilipobidi na maswali ya mwendesha mashtaka na Hakimu Mujaya kupata ufafanuzi kuelewa majibu yake yalikuwa kama ifuatavyo:

Inspekta  Sanga: Kosa, kufanya ngono na maharimu (ndugu ambaye mtu hawezi kumuoa au kuolewa naye kwa sababu ya unasaba wao) kinyume cha kifungu cha 158 (1) (b) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code -PC).

Maelezo ya kosa: Kwamba wewe Mabula Masunga Jiumbi ulifanya ngono na binti yako Mwashi Mabula Masunga, kinyume cha sheria, kuanzia mwaka 2019 mpaka 2023.

Mabula: Siyo kweli (haya ni majibu baada ya kufafanuliwa taratibu na kuelewa pale ilipobidi).

Insp Sanga: Kwamba kwa muda wote huo uliweza kumpa ujauzito mara tatu na kuzaa naye watoto watatu.

Mabula: Siyo kweli

Insp Sanga: Mheshimiwa upelelezi wa kesi hii umeshakamilika na tunaomba kuendelea na hatua inayofuata ya usikilizwaji wa awali yaani kumsomea mshtakiwa hoja za awali (maelezo ya muhtasari wa kesi).

Hakimu Mujaya: Haya msomeeni mshtakiwa maelezo hayo ya awali. Mshtakiwa utasomewa maelezo ya kesi kisha yale unayoyakubali utajibu kuwa ni kweli  na yale unayoyakataa utajibu kuwa si kweli.

Insp. Sanga: Mshtakiwa inaitwa Mabula Masunga Jiumbi, una umri wa miaka 45, mpagani na mkulima mkazi wa mkongo na kwamba alimuoa Holo Seleli Rupile na kuzaa naye  watoto 6 wavulana wanne wa wasichana wawili.

Mabula: Samahani, Kiswahili mimi cha shida (alisema Mabula akirejea na kukumbushwa tatizo lake kuhusu lugha ya Kiswali na Hakimu Mujaya akaridia kumuelezea tena maelezo hayo taratibu) ndipo akajibu kuwa ni ya kweli.

Insp. Sanga: Kuanzia mwaka 2019 ulianza kufanya tendo la ngono na binti yako aitwaye Mwashi Mabula Masunga.

Mabula: Hamna, si kweli.

Insp. Sanga: Kwamba uliweza kumpa ujauzito mara tatu na kumzalisha watoto watatu.

Mabula: Siyo kweli.

Insp Sanga: Baada ya taarifa kufika kituo CA Polisi Ikwiriri ulikamatwa na kuhojiwa na upelelezi ukafanyika.

Mabula: Ni kweli.

Insp. Sanga: Baada ya upelelezi kukamilika umeletwa leo mahakamani kwa ajili ya mashtaka.

Mabula: Ni kweli.

Insp. Sanga: Mheshimiwa tutakuwa na mashahidi 6 na kielelezo kimoja na kwa leo tuna shahidi mmoja, tunaomba kuendelea.

Hakimu Mujaya alikubaliana na hoja ya upande wa mashtaka kuanza usikilizwaji wa ushahidi moja kwa moja na akaelekezwa shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka, ndipo akaitwa binti huyo anayedaiwa kuzalishwa na baba yake.

Baada ya Binti huyo (shahidi wa upande wa mashtaka) kuingia mahakamani kuanza kutoa ushahidi wake, Hakimu Mujaya alimuuliza maswali ya awali kuhusu utambulisho wake na kisha aapishwe. Mahojiano yalikuwa kama ifuatavyo:

Hakimu: Unaitwa nani?

Shahidi: Mwashi

Hakimu: Mwashi nani? Taja majina ya baba yako.

Shahidi: Mabula Masunga Jiumbi.

Hakimu: Una miaka mingapi?

Shahidi: Sijui

Hakimu: Dini yako? (Huwa unakwenda kanisani au msikitini? Alihoji Hakimu Mujaya kumfafanulia shahidi huyo baada ya kuona anababaika kujibu swali hilo)

Shahidi: Sina (dini, alijibu shahidi huyo baada ya kuelewa vyema alichokuwa ameulizwa na Hakimu).

Hakimu: Kwa hiyo ni mpagani, haya kwa kuwa huna dini hutaapishwa, bali utathibitisha tu (kuwa ushahidi atakaoutoa ni wa kweli na kweli tupu), karani (wa Mahakama) muongeze, kuthibitisha.

Hivyo bila kushika kitabu chochote cha imani kubwa mbili yaani Biblia Takatifu kwa Wakristo au Kuran Tukufu kwa Waislamu) kama ambavyo mashahidi wa imani hizo huwa wanafanya kuwapa (Wakristo) au kuthibitisha (Waislamu) wakiwa wamekiinua juu kitabu hicho, karani alimwambia shahidi huyo kuinua mkono wake mtupu juu.

Kisha alimtaka afuatishe maneno ambayo atakuwa anayasema na hali ilikuwa kama ifuatavyo:

Karani: Mimi Mwashi Mabula Masunga...

Shahidi: Mimi Mwashi Mabula Masunga...

Karani: Nathibitisha kwamba...

Shahidi: Eeh...

Karani: Rudia maneno ninayoyatamka Mimi; Nathibitisha kwamba...

Shahidi: Nathibitisha kwamba...

Karani: Ushahidi nitakaoutoa...

Shahidi: Ushahidi nitakaoutoa...

Karani: Ni wa kweli...

Shahidi: Ni kweli...

Karani: Kweli tupu...

Shahidi: Kweli tu (tupu)..


Karani: Mungu nisaidie.

Shahidi: Mungu atanisaidia.

Baada ya shahidi huyo kumaliza kuthibisha  kusema ukweli mtupu, Inspekta Sanga aliieleza mahakama kuwa binti huyo Kiswahili hawezi na kwamba naye anajua zaidi lugha ya Kisukuma.

Hivyo Inspekta Sanga alipendekeza aitwe mkalimani kwa ajili kuitafsiri kutoka lugha ya Kiswahili kwenda Kisukuma na kutoka Kisukuma kwenda Kiswahili na akapendekeza aitwe Afande Ezekiel aapisbwe kwa ajili ya jukumu hilo.

Hivyo Hakimu Mujaya alielekeza mkalimani huyo akaitwa, akajitambulisha kwa jina la H1873 Ditektivu Koplo Ezekiel, Msukuma (kabila lake) mkazi wa Ikwiriri Kaskazini na kazi yake askari Polisi. Kisha aliapa kufanya kazi ya kuitafsiri ku kati ya lugha ya Kiswahili na Kisukuma kwa ukweli wa kike atakachokisema shahidi huyo.

Kisha Insp. Sanga alianza kumuongoza shahidi huyo kutoa ushahidi wake kupitia kwa mkalimani huyo, aliyekuwa kiungo kati ya mwendesha mashtaka, shahidi na pia Mahakama.

Insp Sanga: Shahidi hebu ikumbushe Mahakama majina yako, umesema Unaitwa nani?

Shahidi: Mwashi Mabula Sanga Jiumbi

Insp Sanga: Umri wako?

Shahidi: Miaka sijui

Insp Sanga: Unaishi wapi?

Shahidi: Pambe (Kitongoji, Kata ya Mkongo).

Insp Sanga: dini yako?

Shahidi: Sina dini

Insp. Sanga: Kazi yako?

Shahidi: Mkulima.

Insp. Sanga: Huko Pambe unaishi na nani?

Shahidi: Naishi kwa baba yangu, Mabula Masunga Jiumbi

Pia tunaishi na ndugu zangu na mama yangu.

Insp. Sanga: Wewe umewahi kuolewa?

Shahidi: Nimeolewa ila mwanaume hajanichukua kwa baba.

Insp.Sanga: Mume wako anaitwa nani?

Shahidi: Namfahamu kwa jina moja la Maganga.

Insp Sanga: Una watoto?

Shahidi: Ndio, nina watoto watatu.

Insp. Sanga: Majina yao wanaitwa nani na nani?

Shahidi: Wa kwanza anaitwa Willy Mabula Masunga, wa pili ni Holo Mabula Masunga na wa  tatu ni Mabula Mabula Masunga.

Insp.Sanga: Umewahi kuwa na mahusiano na baba yako?

Shahidi: Sijawahi kuwa na mahusiano na baba yangu Mabula Masunga.

Insp: Lakini watoto hao ni wa baba yako?

Shahidi: Watoto hao sio wa baba yangu.

Insp. Sanga: Kwa nini kituo cha Polisi ulieleza kuwa ulizaa na baba yako?

Shahidi: Kwa kuwa walikuwa wananipiga (Polisi).

Insp Sanga: Ulikuwa unapigwa na Polisi yupi?

Shahidi: Nilikuwa napigwa na askari wote.

Insp Sanga: Kwa nini Polisi walikupiga wakati ulifika kulalamika kuwa ulizaa na baba yako?

Shahidi: Walikuwa wananipiga hata kabla ya kujua swali nililoulizwa na wala kosa.

Insp Sanga: Shahidi lakini tuna maelezo yako uliyoyasaini yako hapa mahakamani, kwa nini unakwenda kinyume?

Shahidi: Kwa kuwa walikuwa wananipiga niliamua kujibu tu hivyo.

Insp. Sanga: Ikitokea uthibitisho wa kisayansi kuwa watoto ni wa baba yako uko tayari kuhusika kama ulivyoeleza hapa,  kuwa umeidanganya Mahakama?

Shahidi: Niko tayari kushtakiwa sababu sijazaa na baba yangu.

Insp Sanga: Kwa sasa baba yako yuko wapi?

Shahidi: Huyu hapa (huku akimgeukia mshtakiwa aliyekuwa amekaa nyuma yake (shahidi) kwenye benchi.

Baada ya mwendesha mashtaka kumaliza kumuongoza shahidi huyo aliyedai amegeuka, Hakimu Mujaya alimuuliza mshtakiwa kama ana swali la kumuuliza shahidi huyo, naye akajibu kuwa anayo na Hakimu akampa nafasi ya kumuuliza.

Mshtakiwa: Mwashi, kwa nini umetaja majina ya watoto bila ubini wa baba wa watoto bali majina yangu?

Shahidi: Nimetaja majina ya baba na babu upande wangu mimi.

Mshtakiwa: Kwa nini ulitumia majina ya ubini wangu?

Shahidi: Nimetaja majina hayo upande wa ubini kwa sababu hajatolewa mahari.

Baada ya mshtakiwa kumaliza maswali yake kwa mshtakiwa, Hakimu Mujaya alimuuliza mwendesha mashtaka kama alikuwa na maswali kwa shahidi ya ufafanuzi wa majibu ya maswali aliyoulizwa na mshtakiwa lakini mwendesha mashtaka akajibu kuwa hakuwa nayo.

Hakimu Mujaya kabla ya kuahirisha kesi hiyo alimueleza mshtakiwa kuwa dhamana yake iko wazi na kwamba anatakiwa kutimiza masharti ya kuwa na wadhamjnj wawili wenye barua ya utambulisho kutoka ofisi inayotambulika na kitambulisho cha Nida na watasaini bondi ya Sh2 milioni.

Mshtakiwa Mabula alijibu kuwa anao wadhamini, lakini wadhamini wake walipoitwa na askari huko nje hakutokea hata mmoja.

Hivyo Hakimu Mujaya alipanga kuendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo Novemba 8, 2023, na akiahirisha hadi tarehe hiyo huku aliamuru mshtakiwa huyo apelekwe mahabusu kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.