Biteko awataja wanaoruhusiwa kuuza madini ndani ya ukuta wa Mirerani bila leseni

Wednesday January 13 2021
By Filbert Rweyemamu

Simanjiro. Wafanyakazi kwenye migodi ya wachimbaji wadogo wa madini ya Tanzanite iliyopo Mirerani wamepata ahueni baada ya Serikali kuwatambua kuwa wanaweza kuuza madini ndani ya eneo hilo lililozungushiwa ukuta bila kuwa na leseni.

Hayo yameelezwa na waziri wa madini, Dotto Biteko leo Jumatano Januari 13, 2021 wakati akizungumza na wadau wa shughuli za uchimbaji kwenye migodi hiyo.

Amesema wafanyakazi wana haki ya kuuza madini waliyopata bila kuulizwa leseni kwa sababu mfanyakazi wa aina hiyo hawana leseni kisheria.

"Nafahamu imekua changamoto kwenu Wanaapolo (wafanyakazi kwenye migodi ya wachimbaji wadogo)  jambo la msingi mnapofika kwenye ofisi ya uthamini msiulizwe leseni bali tathmini ikishafanyika uzeni madini mpate riziki yenu," amesema Biteko

Biteko alikua akijibu hoja za wadau hao waliotaka ufafanuzi wa namna ya kuendelea na shughuli zao bila kubughudhiwa na vyombo vya dola vilivyopo Mirerani.

Kuhusu Lakiri ambayo wachimbaji na Wanaapolo wameilalamikia amesema haitatumika badala yake watahitaji kupata kibali kinachoonesha kiwango cha madini kinapotoka hadi kwenye soko.

Advertisement

Biteko amesema Serikali imekua ikidhibiti utoroshwaji wa madini kupitia taasisi zake lengo likiwa kuifanya sekta hiyo iwanufaishe wadau walio katika mnyororo wa thamani huku Serikali ikipata mapato yake.

Naye Ambrose Ndege amesema wamekua wakitumia muda na nguvu zao kuchimba madini lakini baada ya madini kupatikana wasimamizi wa migodi wamekua wakiwapekua wasiondoke na madini  na kumshukuru Biteko kwa uamuzi wake huo.

"Kazi ya kudhibiti utoroshwaji wa madini sio ya serikali pekee yake ni wajibu wa kila mtu anayeingia ndani ya ukuta huu, jinsi mnavyoshirikiana na maafisa wetu ndivyo na masharti ya udhibiti yanavyolegezwa lakini ukaguzi utaendelea," amesema Biteko.


Advertisement