Biteko: Hali ngumu yakwamisha utumiaji wa nishati safi

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko akizungumza kwenye hafla ya kuwasilisha ripoti ya mpango wa matumizi ya bayogesi na kuendeleza ushirikano kati ya ubalozi wa Sweden na Tanzania Jijini Dodoma.

Muktasari:

  • Naibu Waziri mkuu na Waziri wa Nishati Dk Doto Biteko amesema kuna changamoto ya upatikanaji wa nishati endelevu nchini na tafiti zinaonyesha asilimia 18 ya kaya Tanzania Bara zinashindwa kutumia nishati safi ya kupikia kutokana na sababu za kiuchumi.

Dodoma. Serikali imekiri kuwa bado kuna changamoto ya upatikanaji wa nishati endelevu nchini licha ya kuwa asilimia 72 ya kaya za Tanzania Bara zinaishi katika mitaa au vijiji vilivyofikiwa na huduma za umeme.

Hata hivyo kutokana na changamoto ya umeme nchini, imeelezwa kuwa hadi kufikia Machi 2024 Serikali inakusudia kuongeza uzalishaji wa umeme kwa takribani megawati 783 ili kukabiliana na upungufu uliopo sasa wa wastani wa megawati 233 kwa siku.

Hayo yameelezwa leo Novemba 10, 2023 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk Doto Biteko wakati akizindua matokeo ya utafiti wa athari za upatikanaji wa nishati endelevu za mwaka 2021/22.

Dk Biteko amesema mwelekeo wa Serikali ni kuzalisha angalau megawati 5,000 za umeme ifikapo mwaka 2025 na kukamilisha mkakati wa kitaifa wa angalau asilimia 80 ya watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2033.

“Kutokana na matokeo hayo na takwimu zilizokusanywa na tafiti zilizofanywa wakati wa sensa ya watu na makazi mwaka jana, pamoja na mafanikio tukiri bado kuna changamoto ya upatikanaji wa nishati endelevu”amesema.

Biteko amesema Serikali imeanza kupeleka umeme kwenye vitongoji vyote Tanzania bara na sasa inapeleka kwenye vitongoji 15 kwa kila jimbo la uchaguzi.

Kwa mujibu wa taarifa ya REA ya mwezi Novemba 2023, inaonesha kuwa jumla ya vijiji vilivyounganishwa na umeme Tanzania bara ni 11,079 sawa na asilimia 90 ya vijiji vyote 12,318 huku vijiji vilivyobaki 1,239 sawa na asilimia 10 vikitarajiwa kuunganishwa na umeme ifikapo Juni 2024.

Dk Biteko amesema kwa mujibu wa matokeo ya Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, yanaonesha kuwa, idadi ya kaya zilizounganishwa na umeme Tanzania bara zilikuwa 5,043,801 kati ya hizo kaya 3,728,287 ziko mijini na kaya 1,315,514 ziko vijijini.

Kuhusu nishati safi ya kupikia Dk Biteko amesema utafiti umebaini kuwa asilimia 18 ya kaya Tanzania Bara zinashindwa  kupata njia za kisasa za kupikia kwa sababu zinagharimu zaidi ya asilimia 5 ya kipato chao.

Amesema utafiti huo umeonyesha asilimia 35 ya kaya zinazoishi Dar es Salaam zinatumia mitungi ya gesi (LPG) kwa kupikia huku maeneo mengine ya mijini ikiwa kwa asilimia 14 na asilimia 82 ya kaya iliyobaki inaweza kumudu kutumia njia za upikaji za kisasa.

“Utafiti umeonyesha kuwa, gesi ni ghali, haipatikani katika vifurushi au vifungashio vidogo zaidi ikilinganishwa na mkaa, utatuzi wa changamoto hii inahitaji muunganiko wa kisera kwa kuwashirikisha wadau wa kuzalisha gesi kulingana na mahitaji ya soko”amesema.

Amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua za kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa kuwapatia wananchi mitungi na vifaa vyake ambapo mwaka 2023/24 Serikali kupitia REA imepanga kutoa mitungi 200,000 ya LPG na vifaa vyake.

Katika mwaka 2023/24, REA imepanga kusambazaa majiko banifu 70,000 katika maneo ya vijijini na mijini (peri urban) yaliyotengenezwa kwa teknolojia yenye ubunifu wa kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.

Ili kukidhi mahitaji ya umeme Biteko amesema Serikali itaendelea kuongeza idadi ya njia za kusafirisha umeme kutoka kilomita 6,110.28 za mwaka 2021/22 hadi kufikia kilomita 10,670.95 mwaka 2025/26.

Pia amesema Serikali imeimarisha usambazaji wa umeme kwa kuongeza njia za kusambaza umeme kutoka kilomita 154,567.75 za mwaka 2021/22 hadi kufikia kilomita 226,302.64 mwaka2025/26.

Kwa upande wake Mtakwimu mkuu wa Serikali Dk Albina Chuwa amesema utafiti huo umefanyika kwa kushirikiana na Taifa la Norway na takwimu hizo zinaonyesha kukua zaidi kwa sekta ya nishati nchini.