Bodaboda watano wafariki dunia kwa kugongwa na lori kijiweni
Wakazi wa Kata ya Dodoma Makulu Jijini Dodoma wakiangalia ajali ya lori iliyosababisha vifo vya madereva bodaboda watano. Picha na Rachel Chibwete
Muktasari:
- Watu watano wamefariki dunia baada ya lori kufeli breki na kugonga waendesha bodaboda waliokuwa wamepaki kwenye kijiwe chao jijini Dodoma.
Dodoma. Watu watano ambao ni madereva bodaboda wamefariki dunia papo hapo baada ya kugongwa na lori lililofeli breki eneo la Dodoma Makulu jijini Dodoma usiku wa kuamkia leo.
Lori lilikuwa linatokea kwenye barabara inayotokea Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) ambapo lilifeli breki na kwenda kuparamia Kijiwe cha Bodaboda cha Amani kilichopo kando ya barabara hiyo na kusababisha maafa.
Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gallus Hyera amesema tukio hilo limetokea jana Desemba 11, 2025 saa 2:30 usiku ambapo katika ajali hiyo mtu mmoja alijeruhiwa ambaye ni utingo wa lori hilo.
Kamanda Hyera amesema athari nyingine iliyosababishwa na ajali hiyo ni uharibifu wa pikipiki za vijana hao pamoja na kuharibiwa kwa ukuta wa uzio wa nyumba iliyokuwa karibu na barabara ambao uligongwa na lori hilo.
“Eneo hilo la barabara lina mteremko mkali hivyo madereva ni lazima waendeshe mwendo wa tahadhari ili inapotokea changamoto yoyote waweze kuepusha maafa yanayoweza kuzuilika,” amesema Kamanda Hyera.
Amesema kutokana na eneo hilo kuwa la hatari kwa waendesha vyombo vya moto na watembea kwa miguu Jeshi la Polisi litaimarisha usalama katika eneo hilo wakati mamlaka nyingine kama Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) wakifanya jitihada za kuepusha ajali zaidi katika eneo hilo.
Akizungumza kwenye eneo la tukio Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Jabir Shekimweri amesema watazungumza na Tanroad ili waweke matuta katika eneo hilo kwa ajili ya kuwawezesha madereva kupunguza mwendo kutokana na eneo hilo kutokea ajali mara kwa mara.
“Inaonekana gari hili lilipata hitilafu kwa hiyo dereva alishindwa kulimudu na ndiyo maana liliacha njia na kwenda kuwaparamia vijana wetu na kusababisha maafa, inabidi tuweke matuta katika eneo hili ili kudhibiti mwendo kwa wanaopandisha na wale wanaoshusha kwa ajili ya usalama wetu,” amesema Shekimweri.
Amesema madereva hao walikuwa wamepaki pikipiki zao nje ya barabara lakini kutokana na lori hilo kufeli breki liliwafuata na kusababisha vifo hivyo.
Mmoja wa mashuhuda James Tusiime amesema alisikia kishindo kikubwa kutokea maeneo ya barabarani ambacho hakikuwa cha kawaida kilichoashiria kuna tatizo na alipofika kujua kinachoendelea alikuta ajali hiyo.
“Wote waliofariki walikuwa ni vijana wetu ambao huwa wanatuwahisha tunapokwenda, leo ajali imekatisha uhai wao kwa kweli tunasikitika sana,” amesema Tusiime.
Naye Happiness Richard amesema lori hilo lilikuwa linapiga honi mfululizo barabarani kuashiria kuna tatizo lakini lilipofika kwenye kona lilishindwa kukata kona hivyo liliacha njia na kwenda kuwagonga maderea hao bodaboda ambao walikuwa wanawasubiri abiria kwenye kijiwe chao.
Hiyo ni ajali ya tatu kutokea katika eneo hilo Makulu ambazo zimegharimu maisha ya watu ikiwemo waendesha vyombo vya moto na watembea kwa miguu.