Bongo Fleva waliofanya makubwa mwaka 2020

New Content Item (1)
Bongo Fleva waliofanya makubwa mwaka 2020

Muktasari:

Kiwanda cha muziki Tanzania kimeshuhudia mafanikio makubwa mwaka 2020 licha ya kwamba dunia ilikuwa katika nyakati ngumu za kuishi katikati ya janga la corona.

Kiwanda cha muziki Tanzania kimeshuhudia mafanikio makubwa mwaka 2020 licha ya kwamba dunia ilikuwa katika nyakati ngumu za kuishi katikati ya janga la corona.

Ndani ya mwaka huu, wasanii wamewashibisha mashabiki vya kutosha kwa kuachia kazi nyingi huku wanamuziki hasa wa muziki wa kizazi kipya wakivunja rekodi.

Ni kutokana na hilo, Mwananchi inakupa orodha ya wasanii ambao inadhani walikuwa bora zaidi kwa mwaka huu 2020.

Diamond

Ndani ya 2020 mwanamuziki Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz alifanya kufuru kama si kutia fora. Kwanza msanii huyu amechaguliwa kuwania tuzo tatu za kimataifa ambazo ni Afrimma, Aeausa na MTV Mama.

Kati ya hiyo, Diamond ameshashinda tuzo mbili -- msanii Bora Afrika kwenye tuzo za Aeausa na mwanamuziki bora wa kiume kwenye tuzo za Afrimma. Pia Diamond ni kati ya wanamuziki sita kutoka Tanzania ambao wameshirikishwa kwenye nyimbo nyingi kwa mwaka 2020. Ameshirikishwa kwenye nyimbo nane za wanamuziki maarufu, akiwamo msanii wa Marekani, Alicia Keys.

Pia kwa mwaka 2020 Diamond amevunja rekodi kwa wimbo wake wa Waah aliomshirikisha nguli wa muziki kutoka DR Congo, Koffi Olomide baada ya kutimiza watazamaji milioni moja kwa muda wa saa nane, ukiwa muda mfupi zaidi kwenye mtandao wa Youtube na kuvunja rekodi iliyokuwa inashikiliwa na mwanamuziki kutoka Nigeria, Davido na kibao chake cha FEM ambacho kilifikisha idadi hiyo ya watazamaji ndani ya saa tisa.

Isitoshe, msanii huyu alikuwa ni ndiye pekee Mtanzania wa kiume kushiriki kwenye matamasha ya kimataifa kama vile tamasha la Africa Day Benefit ambalo lilifanyika Mei kwa ajili ya kuchangisha fedha za kusaidia familia zilizoathirika na matokeo ya janga la corona barani Afrika na kusababisha achaguliwe kwenye tuzo za MTV Mama, kipengele kipya cha ‘Alone Together’, ambacho kinawatunuku wasanii waliofanya shoo kali kipindi cha corona.

Nandy

Kwa mwaka 2020 msanii huyu ambaye jina lake kamili ni Faustina Mfinanga ameshinda tuzo mbili za kimataifa ikiwemo Afrimma kama msanii bora wa kike Afrika Mashariki, na katika tuzo za Aeusa ameshinda kama msanii bora wa kike Afrika, hii ni sawa na kusema si tu Nandy ni mkali Tanzania, bali Afrika nzima.

Aidha, kwa mwaka huu Nandy ametengeneza ‘hits song’ zaidi ya tatu ikiwemo Acha Lizame aliomshirikisha Harmonize, Do Me aliofanya na mume wake mtarajiwa, Billnass na Nibakishie alioshirikana na mfalme Alikiba na zote zimekusanya ‘view’ zaidi ya milioni 10 Youtube.

Zuchu

Zuchu hazuiliki kuwa katika orodha ya wanamuziki bora mwaka 2020? Kwani akiwa na miezi minane tu tangu atambulishwe kwenye kiwanda cha muziki Tanzania, Zuchu ameshatajwa kwenye tuzo tatu kubwa za kimataifa ikiwemo Afrimma ambapo ameshinda msanii bora chipukizi, na pia ametajwa tuzo za Aeausa na MTV Mama.

Aidha Zuchu ndiye msanii wa kike anayeongoza kwa ngoma zake kutazamwa zaidi kwenye mitandao ya kucheza muziki kwa mwaka 2020 kama vile Youtube na Boom Play. Kwa mwaka huu pia Zuchu ametoa nyimbo zaidi ya 10 na zimepata mapokezi makubwa ikiwemo Cheche na Litawachoma alizofanya na Diamond Platnumz ambazo kwa ujumla zinafikia idadi ya watazamaji milioni 23, idadi kubwa kuliko msanii yeyote wa kike wa Tanzania kwa mwaka huu.

Harmonize

Ndani ya mwaka 2020 Rajabu Abdul ‘Harmonize’ aliwekeza muda mwingi zaidi kwenye kujenga lebo yake ya muziki ya Konde Gang, hata hivyo hilo halijamzuia kuibukia kwenye orodha ya wasanii 10 bora wa mwaka 2020. Kwanini? Harmonize ni moja ya wasanii wachache walioshirikishwa kwenye nyimbo nyingi zaidi mwaka huu, ameshirikishwa kwenye nyimbo zaidi ya tano ikiwa ni pamoja na za wasanii kutoka nje ya Tanzania.

Rayvanny

Ni mmoja wa wasanii waliotoa vibao vingi mwaka 2020 na vingi vilivuma. Rayvanny ametoa zaidi ya nyimbo tisa na nyimbo tano alizoshirikishwa.

Nyimbo hizo ni pamoja an Amaboko na Woza zote akiwa amemshirikisha Diamond. Mwingine ni Number One alioimba na Zuchu na ya Teamo na ndio moja ya sababu zilizofanya achaguliwe na kushinda tuzo za Aueusa kama msanii bora wa kiume Afrika Mashariki, Kusini na Kati.

Alikiba

Miaka ya hivi karibuni Alikiba amerudi kitofauti kwa kuachia ngoma nne. Hata hivyo kinachomwingiza kwenye orodha ya wasanii 10 bora wa mwaka 2020.

Lakini pia ana idadi kubwa ya watazamaji kwenye nyimbo zake katika mtandao wa Youtube na nyimbo za kushirikishwa kwani kwa mwaka huu pekee ameshirikishwa kwenye nyimbo nne ukiwemo Nibakishie alioimba na Nandy, Umukwano alioshirikishwa na Tommy Flovour, Bwahehe alioimba na Baby J na Nakupenda aliouachia wiki hii akishirikishwa na DJ kutoka Afrika Kusini, Dj Sbu.

Mbosso

Tangu asainiwe lebo ya WCB miaka miwili iliyopita, baada ya kundi lao la Yamoto kuvunjika, amekuwa moto wa kuotea mbali. Mbosso ambaye jina lake halisi ni Mbwana Yusufu, ameutawala vema mwaka 2020 kwa kuachia vibao vikali ikiwemo Sina Nyota na ule wa Fall aliouachia mwezi mmoja uliopita.

Marioo

Licha nyimbo zake kuchezwa sana mitaani kwa mwaka huu, pia anaingia kwenye orodha ya wasanii wachache kushirikishwa kwenye ngoma nyingi za wasanii wengine. ambapo sasa anatesa na kibao chake cha Mamama Amina.

Kama hiyo haitoshi, pia kwa mwaka huu 2020 Marioo ameanza kwenda kimataifa kwa kufanya ‘colabo’ na wasanii kutoka nje ya nchi akiwemo Nadia Mukami wa nchini Kenya katika wiombo wake wa Jipe na Sho Madjozi wa Afrika ya Kusini aliyeimba naye wimbo wa Mama Amina kati ya wimbo unaotesa kwa sasa. Marioo anatabiriwa huenda mwakani akafanya vizuri zaidi.

Young Lunya,Rostam

Wengine waliong’ara ni wasanii wa miondoko ya kufokafoka akiwemo Young Lunya na Stamina na Roma kupitia kundi lao la Rostam.

Imeandikwa na KELVIN KAGAMBO