Boniphace Jacob asema wabadhirifu fedha za umma wachukuliwe hatua, akiichambua ripoti ya CAG

Aliyekuwa Meya wa Ubungo, Boniphace Jacob akifanya uchambuzi wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mwaka 2022/2023.

Muktasari:

  •  Wakati ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ikionyesha kuongezeka kwa hati safi hadi kufikia asilimia 98, Meya mstaafu Boniphace Jacob amesema kuna baadhi ya maeneo upigaji umeongezeka

Dar es Salaam. Aliyekuwa Meya wa Ubungo, Boniphace Jacob amesema kuchukua hatua kali za kinidhamu kwa watakaobainika kushiriki katika ubadhirifu wa fedha za umma katika ripoti ya Mdhibiti Mkuu na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG,) kutasaidia kukomesha vitendo hivyo.

Alitoa kauli hiyo wakati akifanya uchambuzi wa ripoti ya CAG ya Mamlaka za Serikali za mitaa mwaka 2022/2023 huku akifanya mlinganisho na kile kilichokuwapo mwaka 2021/2022.

Jacob amesema anashangaa kuona fedha za miradi zinazotolewa katika halmashauri zinazoshindwa kumalizika zikiongezeka, wakati ambao miundombinu ikiwemo barabara katika maeneo mbalimbali ni mibovu.

Serikali ina utaratibu wa kukamilisha matumizi ya fedha zilizopangwa kila ifikapo Juni 30, wakati ambao Hazina wanaweza kuichukua fedha itakayobakia katika utekelezaji wa miradi, isipokuwa ile iliyoandikiwa barua ya kuombewa kibali maalumu cha kuhamisha fedha kwenda mwaka unaofuata.

Katika ripoti ya CAG aliyoitoa mwaka huu inaonyesha kuwa fedha za miradi ya maendeleo zilizosalia hadi mwisho wa mwaka wa fedha 2022/2023 zilikuwa Sh19.79 bilioni ikiwa ni ongezeko kutoka Sh11.5 bilioni mwaka uliotangulia.

“Wakati mwingine tunalalamika barabara mbovu, mitaro hakuna, watu wanakaa chini kumbe hizi halmashauri zinabaki na fedha ambazo wanaona hawana matumizi yake,” amesema Jacob.

Amesema hela hizo zitakaposahaulika baada ya muda huliwa kwani bajeti mpya ikitoka mambo mengi yanabadilika.

Kwa mujibu wa ripoti hizo, halmashauri ambazo zimesalia kuwa na fedha za miradi ya maendeleo ambazo hazikutumika pia ziliongezeka, kutoka 12 mwaka 2021/2022 hadi halmashauri 27 katika ripoti ya mwaka huu.

Hili linasemwa wakati ambao Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliwahi kueleza kuwa fedha za bakaa kwa sasa zinatumika kama kichaka cha watendaji kujipatia fedha.

Alipokuwa katika wilaya ya Bunda, Majaliwa  alisema halmashauri hiyo imekuwa ikitumia mwanya huo kuziombea kibali fedha, kisha zinahamishiwa kwenye akaunti jumuifu ya amana, halafu zinatolewa na kutumiwa kinyume na utaratibu.

Alisema mchezo huo unafanywa na watu wachache kwenye Halmashauri ya Wilaya kwa kushirikiana na watumishi wasio waaminifu wa kitengo cha akaunti jumuifu ya amana kilichopo Tamisemi na hata Katibu Mkuu hawezi kujua mchezo huo wala madiwani.

“Mara nyingi wanaocheza mchezo huo hapa Bunda ni Mkurugenzi wa Halmashauri, Mweka Hazina na Mkurugenzi wa Mipango wa Halmashauri. Kwa mfano, mwaka wa fedha 2021/2022 waliomba kibali cha kuhamisha Sh871.4 milioni ili ziweze kutumika baada ya muda lakini walihamisha Sh962 milioni na kuzihifadhi huko,” alisema Majaliwa.

Jacob amesema kutoa hatua kali za kinidhamu kwa baadhi ya watu ikiwemo viongozi wa halmashauri wanaotajwa kuhusika inaweza kusaidia kukomesha ubadhirifu.

"Ukitoa mifano michache kwa baadhi ya watu hivi vitu vinakomesheka, mtu atolewe halmashauri atenguliwe, vilevile tumuone akipandishwa kizimbani, kuwajibishwa kwa ufisadi aliofanya kwenye halmashauri yake, wengine watajifunza, wakuu wa wilaya wakiwajibishwa kutokana na kile walichofanya wengine watajifunza," amesema Jacob.

Jacob pia amesema uchambuzi wake umebaini kuwa manunuzi yenye thamani ya Sh14.02 bilioni yalifanyika nje ya mpango wa manunuzi wa halmashauri mwaka 2021/22 kiasi ambacho kimeongezeka hadi kufikia Sh28.87 bilioni ripoti ya mwaka huu.

Pia halmashauri zinazokwenda nje ya mfumo huo zimefikia 22 mwaka huu kutoka 19 mwaka uliotangulia.

Pia ununuzi ambao haukuidhinishwa na bodi za zabuni ulifikia Sh4.79 bilioni katika ripoti ya mwaka 2022/2023 kutoka manunuzi ya aina hiyo yaliyofanyika ya Sh4.34 bilioni.

Jacob ameendelea kwa kueleza kuwa, sehemu nyingine ambayo imeonekana kutotiliwa mkazo ni manunuzi yanayofanywa bila kuzingatia ushindani kwa mujibu wa sheria.

Ripoti iliyotoka 2021/2022, CAG alibainisha kuwa ukaguzi wake alibaini halmashauri 10 zilifanya ununuzi wenye thamani ya Sh2.85 bilioni kwa kutumia mzabuni mmoja au wachache badala ya njia ya ushindani kinyume na matakwa ya sheria.

Hata hivyo, hili liliongezeka kupitia ripoti iliyotolewa mwaka huu ambapo manunuzi ya aina hii yalifikia thamani ya Sh4.65 bilioni uliofanywa na halmashauri 36.

Katika upande wa kuingia mikataba bila kupitiwa na mwanasheria, katika mwaka 2021/2022 halmashauri 20 za Serikali za mitaa zilisaini mikataba yenye thamani Sh6.68 bilioni  kabla mikataba hiyo kupitiwa na mwanasheria.

Hata hivyo, licha ya halmashauri zilizosaini mikataba bila kupitiwa na mwanasheria zikipungua hadi kufikia 14 katika ripoti ya mwaka huu, lakini thamani yake ilifikia Sh9.95 bilioni.