Bosi Takukuru mwenye mashtaka saba aitaka kamati ya maridhiano

Muktasari:

Aliyekuwa Mchunguzi Mkuu wa Takukuru, Cosmas Batanyita anayekabiliwa na mashtaka saba, ameiomba mahakama imsaidie kukutana na Kamati ya maridhiano baada ya kuwasilisha kwa DPP maombi yake ya kuomba msamaha.

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mchunguzi Mkuu wa Takukuru, Cosmas Batanyita ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisitu kukutana na Kamati ya maridhiano ili kujua hatua iliyofikiwa katika maombi yake ya kukiri na kuomba msamaha.

Mshtakiwa huyo aliyewasilisha maombi hayo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), anakabiliwa na mashtaka saba likiwemo la kuomba rushwa ya Sh200 milioni na kutakatisha fedha.

Hatua hiyo imekuja shauri hilo lilipokuja kwa ajili ya kutajwa ambapo Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon ameeleza hayo mbele ya Hakimu Mfawidhi, Godfrey Isaya kuwa upelelezi bado haujakamilika.

Akiwasilisha ombi lake mahakamani hapo, Batanyita alidai kuwa amekuwa akizungushwa kupata majibu ya suala hilo kutokana na kutokuwa na ndugu wa karibu anayeweza kufuatilia kujua hatua iliyofikiwa.

"Nilishaandika barua ya kuomba kukiri kwenda kwa DPP lakini tatizo langu sina ndugu wa karibu watakaoweza kukutana na hiyo kamati hivyo naiomba mahakama hii inikutanishe nayo,"alidai mshtakiwa huyo.

Akijibu hoja hiyo, Wakili wa Serikali, Simon alidai kuwa mshtakiwa huyo anaidanganya mahakama kwani suala hilo linafuatiliwa na mke wake hivyo alipaswa kuuliza limefikia hatua gani.

"Ombi la mshtakiwa ninalifanyia kazi ili aweze kukutana na hiyo kamati ya maridhiano,"alidai Simon.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Isaya aliahirisha shauri hilo hadi Machi 6, 2020 litakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

Inadaiwa mshtakiwa akiwa mwajiriwa wa Takukuru,  Februari 9, 2020, maeneo ya Upanga, alishawishi na kuomba rushwa ya Sh200 milioni kwa Hussein Gulamal Hasham ili aweze kuharibu ushahidi katika kesi ya ukwepaji kodi iliyokuwa inamkabili Hasham, wakati akijua kuwa upelelezi wa kesi hiyo ulikuwa unaendelea katika ofisi ya Takukuru.

Februari 10,2020 katika eneo la Sabasaba, mshtakiwa alidaiwa kujipatia dola 20,000 (Sh46 milioni) kutoka kwa Faizal Hasham ikiwa ni ahadi ya kuharibu ushahidi katika kesi ya ukwepaji kodi inayomkabili Hussein Hasham.

Katika shtaka la tatu, Februari 13, 2020 katika ofisi ndogo za Takukuru zilizopo Masaki jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alishawishi rushwa ya dola 50,000 kutoka kwa Thangvelu Vall, ili aharibu ushahidi katika kesi ya kukwepa kodi inayomkabili Vall.

Shtaka la nne, inadaiwa  Februari 14, 2020, katika Barabara ya Haile Selasie karibu na Merry Brown, Batanyita alishawishi rushwa ya dola 20,000 kutoka kwa Thangvelu Vall, kama ahadi ya kuharibu ushahidi katika kesi ya kukwepa kodi inayomkabili Vall, wakati akijua upelelezi wa kesi hiyo ulikuwa unaendelea.

Katika shtaka la tano,  Februari 10, 2020 mshtakiwa akiwa mwajiriwa wa Takukuru alitakatisha dola 20,000 kutoka kwa Hasham, wakati akijua fedha hizo ni zao la kuomba rushwa.

Mshtakiwa huyo anadaiwa kuwa Februari 19, 2020 katika duka la kubadilishia fedha lililopo Village Super Market, Oysterbay jijini Dar es Salaam, mshtakiwa kwa lengo la kuficha chanzo cha fedha kiasi cha dola 7,000, alizopewa, alibadilisha fedha hizo na kupata fedha za Tanzania Sh16 milioni wakati akijua fedha hizo ni zao tangulizi la kosa la kuomba rushwa.

Shtaka la saba, Februari 19, mwaka huu eneo la Chamazi jijini Dar es Salaam, Batanyita akiwa mwajiri wa Takukuru, alitumia fedha alizopewa kwa njia ya rushwa, kununulia kiwanja eneo la Chamazi wakati akijua fedha hizo ni zao tangulizi la kosa la kuomba rushwa.