Bosi wa Bawacha aibua jambo ripoti za CAG

Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), CPA Catherine Ruge.

Moshi. Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), CPA Catherine Ruge amesema asilimia 99 za hoja za ukaguzi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), zimetokana na fedha zilizokusanywa kwa fedha taslimu.

Ruge aliyasema hayo leo Jumatano Aprili 12, 2023 wakati akichangia mjadala wa Twitter Space wa Mwananchi unaohusu mada ya ‘nini kifanyike ili ripoti za CAG ziweze kuwa na tija kwa Taifa’ unaoendeshwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL).

Mjadala huo unafanyika siku chache kupita tangu ripoti za CAG za mwaka 2021/22 kuwasilishwa bungeni jijini Dodoma na kuibua kasoro kwenye maeneo mbalimbali huku wadau mbalimbali wakiwemo wabunge wakitaka hatua zichukuliwe kwa watakaobainika kuhusika na ubadhirifu huo.

Katika mchango wake, Ruge amesema mabilioni ya fedha ambazo zimeleta hoja za ukaguzi yalikusanywa na kutumiwa nje ya mfumo wa Tehama wa Serikali akisema Serikali haiko makini kuhakikisha mifumo yake inafanya kazi.

Mbali na mapendekezo mengi, Ruge alitaka idara ya ukaguzi wa ndani iboreshwe na Bunge linapaswa kuwa na meno katika kusimamia na kuishauri Serikali.

Ruge aliyewahi kuwa mbunge wa viti maalum amesema ili kudhibiti matumizi mabaya ya fedha na kupunguza mianya ya ubadhirifu ni lazima Serikali iweke mifumo mizuri ya tehama.

"Ni lazima mifumo ya tehama iimarishwe, iboreshwe na kila Taasisi ya Serikali iwekewe miundombinu ya tehama kuhakikisha mapato na matumzi yanapita kwenye mifumo sahahihi, hii itasaidia kudhibiti matumizi mabaya ya fedha lakini pia kupunguza mianya ya ubadirifu," amesema

Pamoja na mambo mengine amesema,"suala la uwajibikaji ni changamoto kubwa sana kwenye nchi yetu, kwa hiyo ni muhimu hizi taasisi ambazo zipo ofisi ya Rais, Rais ana mamlaka kikatiba ya kuchukua hatua na kumfanya mtu yeyote au mteule wake awajibike."

Ameongeza,"lakini pia tunalo Bunge ambalo limepewa hayo mamlaka kusimamia, kuishauri Serikali. Bunge bado halijatimiza hili jukumu lake vizuri, wahakikishe wanatimiza wajibu wao ambao wamepewa na wananchi."