Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bosi wa Jatu 'amwangukia tena DPP'

Muktasari:

  • Hii ni mara ya tatu kwa Gasaya anayekabiliwa na mashitaka mawili likiwemo la kujipatia Sh5.1 bilioni kwa njia ya udanganyifu, kumwandikia barua DPP ya kuomba kukiri mashitaka.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu  wa Kampuni ya JATU  PLC, Peter Gasaya ( 33) anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, amemwandika barua Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP), akiomba kukiri na apunguziwe adhabu ili aweze kuimaliza kesi yake.

Gusaya anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kujipatia Sh5.1 bilioni kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha kiasi hicho cha fedha.

Hata hivyo, Serikali imeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuwa tayari barua hiyo imeshapokelewa na inafanyiwa kazi.

Hii ni mara ya tatu kwa Gasaya, kumwandikia barua DPP ya kuomba kukiri mashtaka yake na kuomba kupunguziwa adhabu, mara ya kwanza ilikuwa Aprili 24, 2023.

Lakini, Julai 31, 2023 mshtakiwa huyo aliondoa nia yake ya kufanya majadiliano na DPP kwa kile alichodai kuwa barua aliyoandika ya kuomba kukiri mashtaka na kuiwasilisha upande wa mashtaka, haionekani.

Mara ya pili ilikuwa Machi 12, 2024, ambapo alimuandikia DPP barua hiyo, lakini majadiliano hayo hayakufikiwa muafaka kutokana kuwepo kwa sheria mpya inayoelekeza kuwa majadiliano ya kuimaliza kesi yatafanyika baada ya upelelezi wa kesi husika kukamilika.

Leo, Jumatano Juni 11, 2025, Wakili wa Serikali, Erick Kamala ameieleza Mahakama hiyo kuwa barua hiyo imeshapokelewa na inafanyiwa kazi.

Kamala ametoa taarifa hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Amedai Gasaya aliandika barua kwa DPP, Juni 6, 2025 na kuomba kufanya majadiliano ya kuimaliza kesi yake.

"Barua hiyo imeshapokewa, hivyo tunaomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa," amesema Kamala.

Hakimu Mhini baada ya kusikiliza maelezo ya upande wa mashtaka aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 25, 2025 itakapotajwa na mshtakiwa amerudishwa rumande.

Mshtakiwa huyo amerudishwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Ifahamike kuwa Desemba 29, 2022 Gasaya alifikishwa mahakamani hapo na kusomewa kesi ya jinai yenye shtaka moja la kujipatia Sh5.1 bilioni kwa njia ya udanganyifu.

Aprili 11, 2023 mshtakiwa huyo alifutiwa kesi hiyo na DPP chini ya kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), sura ya 20, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022 na kufunguliwa kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka mawili.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, mshtakiwa anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kujipatia kiasi hicho cha fedha pamoja na kutakatisha Sh5.1 bilioni katika kesi ya uhujumu uchumi ya mwaka 2023.

Katika shtaka la kwanza, mshtakiwa anadaiwa kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika jiji la Dar es Salaam, akiwa kama Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo, kwa njia ya udanganyifu alijipatia Sh5,139,865,733 kutoka Saccos ya JATU.

Mshtakiwa anadaiwa kujipatia fedha hizo kwa njia ya udanganyifu kutoka Saccos ya JATU kwa kujipambanua kwamba fedha hiyo ataipanda kwenye kilimo cha mazao, jambo ambalo alijua kuwa sio kweli.

Shtaka la pili ni kutakatisha fedha tukio analodaiwa kulitenda kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika jiji la Dar es salaam.

Siku hiyo ya tukio na eneo hilo, mshtakiwa akiwa Mtendaji Mkuu na mwanzilishi wa JATU Saccos, alijihusisha na muamala wa Sh5,139,865,733 kutoka katika akaunti ya JATU Saccos iliyopo benki ya MNB tawi la Temeke kwenda katika akaunti ya JATU PLC iliyopo katika benki ya NMB tawi la Temeke, wakati akijua fedha hizo zinatokana na kosa tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.