BoT yadai uchumi haupimwi kwa fedha za mfukoni

Muktasari:

  • Dk Kibese amesema uchumi haupimwi kwa kuangalia kiasi cha fedha kilichopo kwenye mifuko ya watu na kwamba, unaangaliwa kwa dhana pana ya ukuaji wa sekta.

Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dk Benard Kibese ametoa ufafanuzi juu ya hali ya ukuaji wa uchumi wa Taifa unaodaiwa kutoakisi hali ya maisha akieleza kuwa unakua kutokana na maendeleo ya sekta na si mifukoni mwa watu.

Dk Kibese amesema uchumi haupimwi kwa kuangalia kiasi cha fedha kilichopo kwenye mifuko ya watu na kwamba, unaangaliwa kwa dhana pana ya ukuaji wa sekta.

Msaidizi huyo wa gavana aliyasema hayo jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Dawati la Muhasibu yaliyofanywa na Chama Cha Wahasibu Tanzania (Taa), yakilenga kutoa elimu kwa wajasiriamali katika masuala ya usimamizi wa fedha.

Ripoti ya BoT ya mwaka jana inaeleza kuwa uchumi wa nchi ulikua kwa asilimia 6.9 huku wananchi wakilia ukata, hali iliyoelezwa kuwa ukuaji huo hauna tija kwa maisha ya Watanzania.

“Tumekuwa tukiulizwa kwamba uchumi unakua lakini hamuoni.Wengi wanalalamika hawauoni huo uchumi mfukoni lakini inategemea ni sekta gani inachangia kwenye ukuaji huo wa uchumi,” alisema msimamizi huyo wa uthabiti na usimamizi wa sekta ya fedha.

“Ukiangalia sekta mbalimbali kama elimu, miundombinu na mawasiliano zimepiga hatua sana tofauti na miaka ya nyuma. Vyuo vimekuwa vingi, barabara nazo zimeongezeka.”

Dk Kibese alisema ili watu wauone ukuaji huo ni lazima washiriki kikamilifu kwa kuzitumia fursa zilizopo kwenye sekta hizo kwa ajili ya kujiingizia kipato. Alishauri kuwapo kwa sera imara kwenye sekta hizo kwa ajili ya kuwanufaisha wananchi ikiwamo kutoa ajira.

Kadhalika alisema biashara zisizo rasmi nchini zimekuwa moja ya vikwazo kwenye ukuaji wa uchumi wa Taifa kutokana na kutofanyika kwa uwazi.

Dk Kibese aliwataka wajasiriamali kurasimisha biashara zao ili Serikali izitambue na kuzijengea mazingira bora zaidi ya kuzifanya.

Pia, alisema biashara zisizo rasmi husababisha Serikali kukosa mapato ambayo yangeweza kuongeza tija kwenye ukuaji wa uchumi wa Taifa.

“Huwezi kutenganisha biashara na uchumi. Mzunguko unavyokuwa mkubwa ndivyo uchumi nao unakua kwa kasi,” alisema na kuongeza kuwa;

“Biashara nyingi zinakufa kwa kukosa kumbukumbu za fedha na pia inasababisha kutopata makadirio sahihi ya kodi.”

Mwenyekiti wa Taa, Dk Fred Msemwa alisema elimu hiyo itakuwa chachu kwenye ukuaji na uboreshaji wa mazingira ya biashara nchini.

Alisema ili kuboresha mazingira ya ulipaji kodi ni vyema wafanyabiashara wakaanza kuwatumia wahasibu ili kuwapa tathmini ya kiasi cha kodi wanachotakiwa kulipa.

“Wafanyabiashara wengi wanakosa kumbukumbu za matumizi ya fedha hali inayowafanya kutojua ni kiasi gani cha kodi wanatakiwa kulipa,” alisema.

Dk Msemwa alisema baada ya kuwapo kwa mwitiko mkubwa, chama hicho kimepanga kupeleka elimu hiyo sehemu mbalimbali hasa vijijini.

Mwanachama wa Taa, Ezekiel Maige alisema elimu hiyo imekuja wakati mwafaka kutokana mkazo wa kisheria hasa ulipaji kodi, hivyo kuna haja ya kuwapa ujuzi wajasiriamali juu ya namna wanavyoweza kunufaika na kazi zao. “Ulipaji wa kodi kwa kipindi kirefu umekuwa ni wa upande mmoja, unategemea uamuzi unaotolewa na Mamlaka ya Mapato (TRA), lakini wafanyabiashara wanatakiwa kutoa uamuzi,” alisema.