BoT yatangaza kuungana benki za Twiga na Posta

Muktasari:

Baada ya muungano huo sasa imezaliwa benki ya Tanzania Postal Bank (TPB)


Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza kuungana kwa Benki ya Twiga Bancorp na Benki ya Posta na kuzaliwa Benki ya Tanzania Postal Bank (TPB).

Kuungana kwa benki hizo kunakuja ikiwa imepita takribani miaka miwili tangu Twiga Bancorp kuwekwa chini ya uangalizi na BoT.

Akitangaza kuungana kwa benki hizo leo Jumatano Mei 16, 2018, Naibu Gavana wa BoT, Dk Bernard Kibesse amesema hatua hiyo imetangazwa baada ya mmiliki wa benki hizo ambaye ni Serikali kuwasilisha maombi kwa BoT, kubainisha kuwa lengo ni kuongeza ufanisi wa benki zote mbili na muungano huo unaanza rasmi kesho, Mei 17, 2018.

"Benki Kuu imeidhinisha kuunganishwa benki hizo kama ambavyo mmiliki wake alitaka na kuanzia Mei 17 wateja wa Twiga Bancorp, wafanyakazi, mali na madeni yote yatahamishiwa TPB na Benki Kuu sasa imesitisha kuisimamia benki hiyo," amesema Dk Kibesse.

Amesema benki hiyo iliyokuwa chini ya uangalizi wa BoT tangu Oktoba 28, 2016 baada ya kuona mwenendo wake unahatarisha amana za wateja wake na sekta ya benki kwa ujumla lakini baada ya kuunganishwa na TPB benki hiyo mpya mtaji wake umepimwa na unajitosheleza kwa mujibu wa sheria.

"Benki hii mpya TPB inao mtaji wa kutosha (bila kutaja kiasi) na tunawaomba wateja wa Twiga kuwa watulivu katika kipindi hiki cha kuunganishwa huku wakiendelea kupata huduma kwa kadiri itakavyoelekezwa na benki husika," amesema Dk Kibesse.