Mahakama yabariki ushindi urais wa Ruto

Muktasari:

Mahakama ya Juu nchini Kenya imebariki ushindi wa Rais mteule wa nchi hiyo, William Ruto baada ya kutoa uamuzi wa maombi ya kikatiba yalifunguliwa na mgombea urais aliyeshindwa, Raila Odinga aliyekuwa akipinga ushindi huo.

Nairobi. Mahakama ya Juu nchini Kenya imetupilia mbali maombi ya kikatiba yalifunguliwa wiki iliyopita na mgombea aliyeshindwa, Raila Odinga kupinga ushindi wa Rais Mteule, William Ruto.

Jaji Mkuu Martha Koome amesema Raila na waleta maombi wenzake wameshindwa kuthibitisha kuwa kulikuwa na udanganyifu na uchakachuaji wakati wa mchakato wa kuelekea uchaguzi, siku na baada ya kupiga kura.

LIVE: Mahakama ya Juu Kenya ikitoa uamuzi urais wa RUTO

Odinga (77), mwanasiasa mkongwe ambaye aligombea huku akiungwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta amepinga matokeo ya uchaguzi wa Agosti 9, akiyaita ‘upotoshaji.’

Alishindwa na Ruto kwa kura 230,000 tu chini ya asilimia mbili tu alizohitaji

Uamuzi huo unamfanya Ruto kuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Kenya kufuatia uchaguzi uliokuwa na upinzani mkali.

“Uchaguzi ulikuwa halali na ulifanyika kwa namna huru na wa haki. Hakuna ushahidi wa kuonesha Fomu namba 34 ilingiliwa kwa namna yoyote wakati wa kuzipakia kwenye tovuti ya tume ya uchaguzi ,” alisema Jaji Koome katika hukumu aliyoisoma kwa karibu saa mbili.