Bulembo ataka jamii ijitolee kwa watoto mazingira magumu
Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Halima Bulembo
Muktasari:
- Kwa miaka mitatu iliyopita Jerusalem Children’s Centre imewezesha kulea watoto 49, ambao kati yao 14 wamejiunga na familia zao.
Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Halima Bulembo ameitaka jamii kujitolea kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu ili nao wafikie ndoto zao kimaisha kama watoto wengine.
Bulengo ametoa kauli hiyo jana Agosti 5 katika mbio za kuchangisha fedha kwa ajili ya kituo cha kulea watoto walio katika mazingira magumu cha Jerusalem Children’s Centre (JCH) kilichopo Kigamboni.
Katika mbio hizo kulikuwa na makundi matatu yaliyotofautishwa kwa rangi, ambapo rangi ya njano iilikuwa kwa ajili ya bima ya afya, kuhakikisha watoto hawa wanapata huduma za afya, rangi ya kijani inawakilisha elimu na nyekundu inaashiria azma yetu ya kujenga mustakabali bora kwa Jerusalem Children’s Home.
“Leo, tunaposhiriki pamoja katika marathon hii, hatukimbii tu kwa ajili ya afya au burudani; tunakimbia kwa ajili ya kusudi ambalo ni muhimu sana kwetu.
“Kama mkuu wa wilaya, ningependa kuwahakikishia kuwa msaada kutoka kwa jamii, upendo kutoka kwa wafadhili waliojitolea, na moyo usiochoka kutoka kwa wafanyakazi wa JCH utatupeleka kule tunapopataka,” amesema.
Amewashukuru wasamaria wema wa JCH kwa kujitokeza na kutoa misaada yao kwa mikono mikunjufu.
“Upendo wenu umewaangazia maisha yao, na mmekuwa msaada muhimu katika kufanya kesho yao iwe yenye nuru. Niwasihi tuu kuwa mbio hizi zisiwe mwisho wa mioyo yetu kutoa. Bado tuna nafasi ya kuendelea kuwajali watoto hawa kupitia uongozi wa JCH.
“Tuwaonyeshe watoto hawa kuwa hawako peke yao, kwamba ipo jamii inayosimama pamoja nao, ikiwatia moyo na kuwalea,” amesema.
Pia amewatia moyo watoto hao akisema ndoto zao za maisha zina thamani kubwa.
Akizungumza awali katika mbio hizo, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Upendo Nelson Ngoda amesema kwa miaka mitatu iliyopita kituo hicho kimeweza kulea watoto 49, ambao kati yao 14 wamejiunga na familia zao.
“Kwa sasa kituo kinahudumia watoto 35, ambao kati yao 12 wanahudhuria shuleni; wanne wakiwa shule za awali, wawili darasa la kwanza, mmoja darasa la pili, wawili darasa la nne, mmoja darasa la tano na mmoja darasa la saba,” amesema.
Amesema kituo hicho inamiliki eneo Kigamboni lenye thamani ya Sh38 milioni na zimeshalipwa.
Amesema lengo la mbio hizo ni kukusanya fedha kwa ajili ya ujenzi wa majengo yatakayohifadhi watoto 38 na wafanyakazi wanane.
“Mbio hizi zitahusisha mazoezi, michezo na ukarimu. Washiriki wa makundi yote watajiunga na mbio za umbali wa kilometa 5, kilometa 10 na kilometa 21 mtawalio,” amesema.
“Marathoni hii siyo kukimbia tu, bali ni kuunganisha jamii na kuongeza uelewa kuhusu watoto wanaoishi katika mazingira magumu,” amesema Upendo.