Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bunge la Afrika Mashariki lavunjika

Hoja ya kumng’oa Spika Zziwa ilianza kuzungumzwa kwenye vyombo vya habari vya Afrika Mashariki kwa wiki kadhaa sasa na hatimaye kuwasilishwa jana na Mbunge Peter Mathuki kutoka Kenya kwa niaba ya wenzake Shy-Rose Bhanji wa Tanzania, Nyiranilimo Odette wa Rwanda na Hafsa Mossi kutoka Burundi.PICHA|MAKTABA

Muktasari:

Ni baada ya wabunge kupinga Spika Zziwa kuahirisha kikao kilichotokana na hoja ya kumng’oa.

Arusha. Bunge la Afrika Mashariki (Eala) limeanza kuonekana kufanana na Bunge la Katiba linaloendelea mjini Dodoma.

Bunge hilo jana limevunjika bila kujulikana litakutana tena lini baada ya kuibuka mabishano ya kisheria kuhusu hoja ya kutokuwa na imani na Spika, Margret Zziwa.

Hoja ya kumng’oa Spika Zziwa ilianza kuzungumzwa kwenye vyombo vya habari vya Afrika Mashariki kwa wiki kadhaa sasa na hatimaye kuwasilishwa jana na Mbunge Peter Mathuki kutoka Kenya kwa niaba ya wenzake Shy-Rose Bhanji wa Tanzania, Nyiranilimo Odette wa Rwanda na Hafsa Mossi kutoka Burundi.

Awali Bunge hilo linalopaswa kuanza vikao vyake saa 8:00 mchana lilichelewa kuanza hadi Saa 9:44 alasiri baada ya wabunge kugoma kuingia ukumbini walipobaini kuwa hoja ya kumng’oa Spika haikuwa miongoni mwa shughuli za Bunge kwenye kikao cha jana.

Baada ya mashauriano ya muda mrefu kati ya ofisi ya spika, Mwanasheria wa EAC, Wakili Wilbert Kaahwa na Katibu wa Bunge, Kenneth Madete, Spika Zziwa alikubali hoja ya kumng’oa iongezwe kwenye orodha ya shughuli za Bunge ndipo Mbunge Mathuki alipopewa fursa ya kuwasilisha hoja.

Hata hivyo dakika moja tangu Mathuki alipoanza kusoma maelezo ya hoja hiyo, Mbunge Fred Mukassa Mbidde aliinuka na kuomba mwongozo wa Spika na alipopewa nafasi, alipinga hoja hiyo kuwasilishwa na kujadiliwa kwa madai kuwa kuna kesi katika Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) inayohusiana na hoja hiyo.

Akifafanua Mbidde alisema kesi hiyo inaomba mwongozo na ufafanuzi wa kisheria kuhusu kanuni ya 9 ya Bunge la EAC inayoelekeza utaratibu wa kumwondoa madarakani Spika wa Eala iwapo kutatokea haja ya kufanya hivyo.

Wakati Mbunge Mbidde akiwa bado amesimama huku akiendelea kutoa hoja yake, Mbunge Joseph Ombasa kutoka Kenya aliinuka na kumpinga mbunge mwenzake akisema anataka kulipotosha Bunge kwani kifungu 38 (3) kinaruhusu Bunge hilo kujadili hoja yoyote yenye masilahi ya umma wa EAC ikiwamo hilo la kumng’oa Spika.

Baada ya hoja ya Ombassa, Mwanasheria wa EAC, Kaahwa alisimama kutoa ufafanuzi wa kisheria licha ya kukiri kuwapo kesi mahakamani alisema tayari mahakama hiyo imetoa uamuzi mdogo kuwa shauri hilo haliwezi kuzuia shughuli na mjadala wowote wenye nia ya kumwondoa Spika madarakani

Hoja hiyo ya Mwanasheria ilimwibua tena Mbunge Mbidde aliyehoji kwanini maelezo na ufafanuzi wa mwanasheria huyo yanatoa mwelekeo wa ulipo msimamo wake kuhusu hoja iliyokuwa mbele ya Bunge.

Katika hali iliyoashiria uwapo wa kimkakati kati ya kiti cha Spika na Mbunge Mbidde, Spika Zziwa naye aliunga mkono hoja ya mwanasheria kuonekana anaelemea upande unaotaka ang’olewe.

Kauli hiyo ilimwamsha kitini Mwanasheria Kaahwa aliyemhakikishia Spika kuwa hoja yake inalenga kusaidia uendeshaji bora wa Bunge na siyo kuegemea upande unaotaka kumng’oa.

Baada ya malumbano hayo, Mathuki alinyanyuka kwa nia ya kuendelea na hoja yake lakini Spika hakumpa nafasi na badala yake akatoa ushauri wa hoja hiyo kuondolewa kwenye shughuli za Bunge lakini wabunge wengi wakapinga kwa kupaza sauti za hapana.

Hivyo, ghafla Spika Zziwa alisimama na kutangaza kuliahirisha bunge kwa muda usiojulikana akitumia kifungu cha 82 cha kanuni za bunge hilo kinachotoa mamlaka kwa Spika kufanya hivyo pale panapotokea hali ya kutoelewana ndani ya bunge.

Akitoa msimamo wa nchi ya Uganda anakotoka Spika Zziwa, Waziri wa Afrika Mashariki kutoka Uganda, Shem Bagaine alisema, Serikali ya nchi hiyo haitaki kuingilia mchakato wa vikao na uamuzi wa Bunge la EAC, bali inasubiri kuona hatima ya hoja hiyo.

“ Kama nchi hatutaki kuingilia mchakato wa vikao vya bunge. Kama hoja ya kumng’oa Spika itafanikiwa basi tutapendekeza jina la mgombea mwingine wa nafasi hiyo kwa sababu bado ni zamu ya Uganda kushika wadhifa huo,” alisema

Wakati hali ikiwa hivyo, taarifa za uhakika zilizopatikana kutoka miongoni mwa wabunge zinaeleza kuwa, Rais Yoweri Mseveni wa Uganda aliwataka wabunge wa Eala kuahirisha hoja hiyo ili kumpa fursa ya kuwasiliana na marais wenzake wa EAC.

Rais Museveni alikutana na baadhi ya wabunge kutoka Uganda mwishoni mwa wiki iliyopita.