Bunge laahirishwa kwa muda, chanzo hitilafu ya vipaza sauti

Dodoma. Bunge limeahirishwa kwa dakika 15 ili kupisha ukaguzi wa mitambo iliyopelekea hitilafu ya vipaza sauti.

Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson ameahirisha Bunge leo Oktoba 31, 2023 saa 4.03 asubuhi ili kuruhusu mafundi wafanye ukaguzi.

Hali hiyo ilianzia wakati Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Balozi Nasoro Mbarouk Nasoro alipokuwa akijibu swali.

Baada ya kufika mbele ya mimbari ya kujibia kipaza sauti kiliwaka lakini hakuwa akisikika alichokuwa anazungumza.

Mbarouk alibadirisha maeneo matatu lakini hali haikuwa nzuri licha ya upande mmoja kuwa unasikika lakini kwa shida.

"Naona hata hii haisikiki, hebu mheshiwa hamia eneo lingine pale, au kutakuwa na shida naona maeneo yote ni hivi," amesema Dk Tulia wakati akijaribu kipaza sauti chake.

Awali Naibu Mawazi Patrobas Katambi na Dk Festo Dugange walikuwa wamejibu maswali ya Wabunge bila shida.