Bunge laonya kurudi kwa watumishi hewa

Muktasari:

  • Kati ya mambo yaliyoyofanywa na Serikali ya awamu ya tano katika sekta ya utumishi wa umma ni kuwaondoa wafanyakazi hewa, kuwafuta kazi watumishi waliokuwa na vyeti feki pamoja na darasa la saba walioonekana waliingia kzini bila kuwa na sifa stahiki kwa nafasi walizonazo.

Kati ya mambo yaliyoyofanywa na Serikali ya awamu ya tano katika sekta ya utumishi wa umma ni kuwaondoa wafanyakazi hewa, kuwafuta kazi watumishi waliokuwa na vyeti feki pamoja na darasa la saba walioonekana waliingia kzini bila kuwa na sifa stahiki kwa nafasi walizonazo.

Katika utekelezaji wa suala hilo, zaidi ya wafanyakazi 16,000 walibainika hivyo kufutwa kwenye mfumo wa malipo (payroll) hivyo kuokoa mabilioni ya shilingi zilizokuwa zinatumika kuwalipa stahiki zao.

Wiki moja kabla ya tarehe ya mwisho ya kuwabaini na kuwaondoa watumishi hao, aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Utumishi na Utawala Bora, Angellah Kairuki alisema kufutwa kwa watu hao zaidi ya 16,000 kumeokoa Sh16.15 bilioni ambazo zingetumika kulipa mishahara yao ya Agosti 2016.

Miaka sita baadaye, juhudi hizo zinaonekana kutokuwa na matunda endelevu kwani Bunge limebaini dalili za kuwapo kwa wafanyakazi hewa.

Taarifa ya mwaka ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 2020 inaonyesha bado kuna viashiria vya watumishi hewa kwnai mishahara inayotolewa na Hazina kwenda halmashauri ni nyingi kuliko watumishi waliopo.

Akisoma ripoti hiyo bungeni wiki iliyopita, Mwenyekiti wa LAAC, Grace Tendega alisema kuna viashiria vya kuibuka tena kwa mishahara hewa serikalini, suala ambalo lilishatafutiwa dawa ya kudumu mwaka 2016 Serikali ilipoondoa majina ya wafanyakazi 16,000 kwenye mfumo wa malipo (payroll).

Mwenyekiti huyo alisema hayo baada ya tahtmini ya kamati yake kujiridhisha kwamba kiasi cha mishahara kinachotolewa na Wizara ya Fedha na Mipango (Hazina) kwenda halmashauri ni kikubwa kuliko kinachostahili.

“Hali hii inaashiria serikalini kuna usimamizi hafifu wa mfumo wa mishahara. Udhaifu huu usipodhibitiwa utaibua upya mishahara hewa serikalini,” alitahadharisha Grace.


Ilichobaini kamati

Kwenye tathmini yake, kamati hiyo ya Bunge imebaini kuzidi kwa mamilioni ya shilingi yaliyotolewa kwenda wilayani kwa ajili ya kulipa mishahara ya watumishi waliopo.

Grace alizitaja halmashauri hizo za Mkoa wa Tabora kuwa ni ya Wilaya ya Urambo ambayo mahitaji yake halisi ni Sh13.16 bilioni lakini Hazina ilipeleka Sh13.3 bilioni hivyo kusababisha ziada ya Sh145.73 milioni.

Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua nayo yenye mahitaji ya Sh17.67 bilioni ilipokea Sh17.88 bilioni hivyo kuwa na ziada ya Sh209.9 milioni katika mwaka huo wa ukaguzi wa hesabu zake za fedha.

“Halmashauri ya Wilaya ya Uyui ina mahitaji ya Sh17.06 bilioni lakini Hazina ilipeleka Sh17.37 bilioni hivyo kuwa na ziada ya Sh309.34 milioni,” alisema Grace.

Kwa kuwa Serikali za Mitaa ndizo zenye kanzidata ya watumishi waliopo katika maeneo yao, kamati imependekeza mambo mawili yatakayosaidia kiwango kinachotolewa na Hazina kwa ajili ya mishahara kilingane na kinachohitajika kwenye halmashauri husika.

Kwanza, kamati imependekeza Serikali ichunguze sababu za kutofautiana kwa kiasi cha mishahara kati ya halmashauri na Wizara ya Fedha na Mipango kisha ichukue hatua kwa mujibu wa sheria kutokana na upotevu wa fedha za walipakodi.

Pili, Grace alisema “Serikali ihuishe mfumo wa mishahara unaotumiwa na Hazina uwa na mawasiliano na mfumo unaotumiwa na mamlaka za Serikali za Mitaa nchini ili kupata kiasi sahihi cha mishahara inayopaswa kulipwa. Pendekezo hili linakusudia kudhibiti kuibuka upya kwa hoja ya mishahara hewa serikalini na kuleta hasara bila sababu za msingi.”


Ripoti ya CAG

Kwenye ripoti yake ya ukaguzi wa Serikali za Mitaa ya mwaka wa fedha 2019/20, CAG Charles Kichere amebainisha mapungufu aliyoyaona na akatoa mapendekezo ya nini cha kufanya kudhibiti hali hiyo.

Kati ya mapungufu hayo, CAG amebaini udhaifu katika usimamizi wa rasilimali watu na mishahara unaoathiri utendaji wa kila siku wa taasisi husika kwani kiasi kikubwa cha fedha za Serikali hutengwa kwa ajili hiyo.

Ili kuwa na ufanisi unaotarajiwa, CAG anasema mifumo ya ulipaji mishahara na usimamizi wa rasilimaliwatu ni muhimu ikatumika. Hata hivyo, kwenye ukaguzi wake amebaini mfumo wa usimamizi wa rasilimaliwatu una changamoto.

Kwenye ukaguzi wa mifumo mwaka uliomalizika Juni 2018, CAG alibaini barua za ajira za kughushi kutoka Sekretarieti ya Ajira ya Watumishi wa Umma.

“Katika ukaguzi wangu, nimeona mapungufu ya kutozingatia sheria, miongozo, na maagizo katika kusimamia mishahara na rasilimali watu. Katika mamlaka 10 nilizokagua kulikuwa na watumishi 46 ambao utumishi wao ulikoma lakini wamelipwa jumla ya Sh138.2 milioni ikiwamo mishahara Sh55.35 milioni,” amesema Kichere.

Ili kudhibiti upotevu wa fedha za umma, CAG amependekeza hatua kali zichukuliwe dhidi ya maofisa wa halmashauri wenye dhamana ya kusimamia rasilimali za umma. “Aidha, natoa wito kwa Takukuru kuzipitia kasoro zilizobainika na kuchukua hatua za kisheria,” ameshauri.

Makosa aliyoyabaini CAG yanatokea kutokana na watendaji kutozingatia miongozo na sheria zinazowaongoza kutekeleza majukumu yao.

Mwongozo wa Uhasibu wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wa mwaka 2019 unaelezea wafanyakazi wanaoondolewa kwenye orodha kwa sababu ya kifo, kustaafu, kufukuzwa kazi au kuhamishwa watafutwa kwenye orodha ya mshahara.

Agizo la 20(3) la Randama ya Fedha za Mamlaka za Serikali za Mitaa ya mwaka 2009 linasema madiwani na maofisa wa Serikali za Mitaa watawajibika kwa kuidhinisha malipo yasiyo halali na kuisababishia Serikali hasara.

Kutokana na ukweli huo, CAG anakumbusha kwamba kuna uwezekano malipo hayo yaliyozidishwa ni ulaghai au uzembe uliofanywa na maofisa wa halmashauri hivyo wanapaswa kuchukuliwa kama makosa ya jinai.


Serikali yafafanua

Akizungumzia tofauti iliyojitokeza kwenye malipo mishahara kama ilivyobainishwa na kamati ya Bunge, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba amesema amezisikia hoja zilizotolewa na kueleza sababu za mishahara iliyotolewa na Hazina kuwa mikubwa kuliko idadi ya watumishi waliopo halimashauri.

“Mishahara huingizwa kwenye akaunti ya kila mtumishi. Kilichotokea hata ikaonekana kiasi kilichopelekwa ni kikubwa ni kuwapo kwa wafanyakazi wapya. Hawa wanaweza kuwa awa waliohamia kutoka sehemu nyingine au wapya walioajiriwa,” amesema Tutuba.

Akizungumzia ukaguzi wa CAG, amesema katika mwaka huo wa fedha kulikuwa na madaktari wapya walioajiriwa lakini hawakuingizwa kwenye mfumo hivyo kutoonekana.

Kwa utaratibu uliopo, amesema mfanyakazi mpya akihamia mahali au akiajiriwa, Serikali inatakiwa kumlipa stahiki zake lakini kuna uzembe hufanywa na kusababisha taarifa hizo kutopatikana pindi zikihitajika.

“Uzembe uliofanywa ni Hazina kutoomba relocation report (taarifa ya wafanyakazi wlaiohama) ya wafanyakazi waliohamia. Nimetuma wataalamu kwenda kufuatilia hilo na kuweka mambo sawa,” amesema Tutuba.

Hata mwaka jana, katibu mkuu huyo amesema kuna walimu na wahudumu wa afya waliajiriwa hivyo taarifa zao zisizpoingizwa kwenye mfumo tatizo hilo linaweza kujitokeza tena ndio maana ni muhimu kulishughulikia mapema.