Bunge lapata wawakilishi wa mabunge mengine

Muktasari:
- Wabunge 20 wamechaguliwa kuwakilisha Bunge la Tanzania katika mabunge mengine duniani huku sita wakiingia katika Tume ya huduma za Bunge.
Dodoma.Wabunge 20 wamechaguliwa kuwakilisha Bunge la Tanzania katika mabunge mengine duniani huku sita wakiingia katika Tume ya huduma za Bunge.
Wabunge hao wamechaguliwa baada ya majina yao kupitishwa kwenye Kamati za vyama vyao lakini hawakupigiwa kura kutokana na idadi yao kulingana na nafasi zilizokuwa zikitakiwa.
Spika wa Bunge Job Ndugai, ametangaza majina ya wabunge ha oleo Ijumaa, Juni 25, 2021 ambapo amesema uchaguzi huo umefanyika kutokana na kuanza kwa Bunge jipya la 12 baada ya waliokuwa wawakilishi kumaliza muda wake.
Waliochaguliwa kwa kura ya ndiyo katika Bunge la dunia (APU) Esther Matiko, Mwanaisha Ulenge, Ramadhan Suleiman Ramadhan, Joseph Mhagama na Elibarick Kingu.

Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Matiku akiwa mwenye furaha baada ya wabunge kumchaguwa kuwa miongoni mwa wajumbe katika Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi
Kwa Bunge la SADC wamechaguliwa Shari Raymond, Kassim Hassan Haji, Seleman Zedi, Dk Afred Kimea na Hawa Mwaifunga wakati Bunge la Afrika wameingia Ngh'wasu Kamani, Turfik Salim Turik, Jelly Silaa, Nape Nnauye na Anatropia Theonest.

Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye ni miongoni mwa wabunge watano waliochaguliwa bungeni jijini Dodoma leo, kuwa wawakilishi katika Bunge la Afrika. Picha na Edwin Mjwahuzi
Katika orodha hiyo wapo wabunge waliochaguliwa kwenda Bunge la Umoja wa nchi za Maziwa Makuu ambao ni Dk Christina Ishengoma, Najma Giga, Ezra Chiwelesa, Deus Sangu na Shamsia Mtamba.
Waliochaguliwa katika Tume ya huduma za Bunge ambao wataungana na Spika, Naibu Spika na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu ni Aesh Hillary, Rashid Shangazi na Halima Mdee.
Wengine kwenye Kamati hiyo ni Fakharia Shomari, Janejelly Ntate, Zahoro Mohamed na Khalifa Mohamed Issa.