Bunge lapiga kura kutokuwa na imani na Trump

Thursday January 14 2021
trumpypic

Donald Trump

By Mwandishi Wetu

Washington. Bunge la uwakilishi nchini Marekani limepiga kura ya kutokuwa na imani na rais wa Marekani anayemaliza muda wake, Donald Trump kwa madai kuwa alichochea ghasia zilizosababisha uvamizi wa jumba la bunge la Capitol huku watu wanne wakifariki.

Wabunge 10 wa chama cha Republican walishirikiana na wenzao wa chama cha Democratic kupiga kura hiyo ya kumshtaki rais.

Trump ni rais wa kwanza katika historia ya Marekani kupigiwa kura ya kutokuwa na imani mara mbili ama kushtakiwa kwa makosa ya uhalifu na bunge hilo la Congress.

Rais Trump ambaye ni mwanachama wa Republican sasa atakabiliwa na kesi katika bunge la seneti ambapo iwapo atapatikana na hatia huenda akapigwa marufuku kushikilia wadhifa wowote wa ofisi ya umma.

Trump anaachia madaraka Januari 20, 2021 baada ya kushindwa katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo na mgombea wa Democratic, Joe Biden.

Bunge hilo linalodhibitiwa na wabunge wengi wa Democratic lilipiga kura jana Jumatano saa kadhaa baada ya mjadala mkali huku walinzi wa kitaifa wakiimarisha usalama ndani na nje ya jumba la bunge hilo.

Advertisement

Shirika la kijasusi nchini Marekani FBI limeonya kwamba kuna uwezekano wa kuzuka kwa maandamano katika majimbo yote 50 kabla ya kuapishwa kwa Biden wiki ijayo.

Katika kanda ya video iliotolewa baada ya kura hiyo kupigwa, Trump aliwataka wafuasi wake kuwa watulivu lakini hakuzungumzia kwamba alikuwa amepigiwa kura ya kutokuwa na imani naye bungeni.

“Ghasia na uharibifu hauna nafasi katika taifa letu…, hakuna mfuasi wangu ambaye angependelea kufanyika kwa ghasia za kisiasa” alisema Trump.

Rais huyo alituhumiwa na bunge la Congress kuchochea ghasia zilizosababisha uvamizi wa Bunge  kufuatia hotuba yake aliyotoa Januari 6, 2021 katika mkutano wa hadhara nje ya Ikulu ya Whitehouse.

Aliwataka wafuasi wake kuandamana kwa amani na uzalendo ili sauti zao zisikike, lakini pia kulalamikia uchaguzi wakidai ulikumbwa na udanganyifu mkubwa.


Advertisement