Bunge libainishe mapato ya mbunge na kodi anazolipa

Friday September 03 2021
bungepicc
By Julius Mnganga

Bunge ni mhimili muhimu wa Serikali, ambalo hukutanisha wawakilishi wa wananchi kutoka Tanzania nzima. Ni sehemu pekee ambayo wajumbe wake wanawakilisha maoni ya Watanzania zaidi ya milioni 60.

Si tu uchumi, demokrasia na maendeleo ya nchini hujadiliwa ndani ya mhimili huu. Inaaminika wabunge wanalipwa vizuri zaidi kuliko watumishi serikalini, hata wafanyakazi wa sekta binafsi. Tofauti na kwingineko, bungeni hakuna madaraja, wote wanalipwa sawa, kwani majukumu yao yanafanana.

Pamoja na umuhimu wake kwa jamii na Taifa, Bunge halijaweka wazi kiasi cha mshahara na marupurupu anayolipwa kila mbunge kumwezesha kutimiza wajibu wake. Ni kutokana na usiri huu, ndio maana inakuwa ngumu kuwatetea au kuwapinga wanapodai nyongeza ya masilahi.

Hata madai yaliyoibuliwa hivi karibuni na Mbunge wa Ukonga, Jerry Silaa kisha kamati ya Maadili ikasema mbunge huyo amepotoka, kwa kauli yake kwamba wabunge walipe kodi kama watu wengine, halijadiliki sana kwa sababu wananchi hawayajui malipo anayopokea mbunge. Na Bunge lenyewe limenyamaza, halifunguki.

Kwa nini Spika Job Ndugai na wote wanaomsaidia wanashindwa kuujulisha umma stahiki za wabunge zinazotokana na kodi za wananchi, badala yake wanaacha mjadala usiokuwa na msingi utamalaki?

Wafanyakazi wa Serikali wanapoomba kuongezewa mshahara, mjadala huwa wazi wanataka mshahara huo utoke wapi mpaka wapi, hata sekta binafsi hali ni hiyo.

Advertisement

Jerry aliliomba Bunge kuweka utaratibu utakaowafanya wabunge wote walipe kodi ili wawe na uwezo wa kuwaambia wananchi wao, lakini ambacho umma unakifahamu mpaka sasa ni kwamba mbunge huyo amesema uongo, kwani wabunge wanalipa kodi. Hapa hapaeleweki zaidi.

Kwenye mjadala wa Bunge juzi ilielezwa kwamba wabunge wote wanakatwa kodi kwenye mshahara wao. Hii si hoja kubwa kwa sababu inafahamika kuna kitu wabunge wanalipwa zaidi ya mshahara na hicho ndicho jamii inachotaka kujua.

Bunge linaweza kuueleza umma kwamba mshahara wa mbunge ni kiasi fulani halafu analipwa posho ya kila kikao anachohudhuria, posho ya mafuta ya gari lake, wasaidizi alionao hata dereva anayemwendesha. Jumla ya posho hizo ziangaliwe na Bunge litaje kodi zinazotozwa kwenye kiasi hicho ukiacha ile ya mshahara (Paye).

Wananchi tunatakiwa kujenga uchumi wa Taifa letu, jukumu linalotekelezeka iwapo taarifa zitawekwa wazi. Watu wakijua mbunge analipa kodi kiasi fulani kila mwezi, wakihamasishwa kulipa nao wataelewa.

Usiri uliopo unawafunga midomo wabunge wetu kusema. Hata sasa, baada ya Jerry kuadhibiwa, hakuna mwenye uhakika wa kodi anayolipa mbunge wake kutokana na kumwakilisha bungeni.

Kuna umuhimu kwa Bunge kuweka wazi mchango wake kwenye mapato ya Serikali kutokana na kodi inayolipwa na wabunge ili kuwajumuisha wawakilishi hao wa wananchi kutoa elimu na hamasa kwa wananchi kulipa kodi. Hilo lisipofanyika, sidhani kama kauli ya Jerry itabadilika.

Tungependa kuwaona wabunge kwenye mabaraza ya wafanyabiashara, klabu za wanafunzi na makundi mengine wakijivunia kulipa kodi. Wafanye hivyo kwa taarifa zilizo wazi kuwahamasisha wananchi.

Wabunge wakishiriki katika hili, kazi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) itakuwa ndogo tu, kama kumsukuma mlevi, tofauti na sasa wanapohangaika kuzunguka madukani, sokoni na kwingineko kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kulipa kodi.

Iwapo jamii itafahamu kodi anazolipa mbunge, itakuwa rahisi kwa kila mbunge kuitisha mkutano wa hadhara na kutoa elimu kwa wananchi anaowawakilisha walipe kodi, jambo ambalo maofisa wa TRA hawawezi kulifanya na wananchi wakajitokeza kuwasikiliza.

Kwa hapa tulipo, naamini busara za Spika Ndugai zinahitajika kuruhusu taarifa hizi muhimu zifike kwa wananchi na mhimili huo uwahamasishe kulipa kodi kama wanavyofanya wao. Hilo lisipowekwa wazi, hata Spika mwenyewe hatakuwa na uhuru wa kuwakemea wakwepa kodi au wale wasiotaka kulipa kodi kwa hiari.

Uwazi huu unahitajika zaidi kipindi hiki ambacho Serikali imelazimika kupunguza kodi kwenye miamala ya simu kwa asilimia 30. Uamuzi huu umefanywa baada ya malalamiko ya wananchi kuwa mengi mtaani.

Bunge lina wajibu wa kuwaelimisha wananchi kuhusu kodi na umuhimu wake, likitoa mfano wake lenyewe ili iwe rahisi kueleweka mtaani. Elimu hii inapaswa kutolewa kwa uhalisia ili kila Mtanzania ahamasike kulipa kodi kwa maendeleo ya Taifa.

Julius ni mwandishi wa gazeti hili jijini Dar es Salaam. Kwa maoni, anapatikana kwa 0759 354 122

Advertisement