Bwana harusi alivyofariki kwa ugonjwa wa ajabu

Muktasari:

  • Mmoja kati ya watu watano waliofariki dunia kwa ugonjwa wa ajabu katika Kata ya Maruku na Kanyangereko Bukoba vijijini, mkoani Kagera alikuwa bwana harusi mtarajiwa.

Kagera. Mmoja kati ya watu watano waliofariki dunia kwa ugonjwa wa ajabu katika Kata ya Maruku na Kanyangereko Bukoba vijijini, mkoani Kagera alikuwa bwana harusi mtarajiwa.

Watu hao waliofariki dunia ni kati ya saba walioripotiwa kuwa na ugonjwa huo huku wakiwa na dalili za homa, kutapika, kutokwa damu maeneo mbalimbali ya mwili na figo kushindwa kufanya kazi.

Taarifa ambazo gazeti hili limezipata kutoka kwa ndugu wa karibu ni kwamba kati ya waliofariki ambao tayari miili yao imezikwa alitarajiwa kufunga ndoa Aprili mwaka huu.

Bwana harusi huyo mtarajiwa, Benson Rutabingwa alifikwa na mauti Machi 15 baada ya kuugua ugonjwa huo unaosemekana aliupata kwa ndugu zake watatu ambao ni miongoni mwa watano walioripotiwa kufariki dunia.

“Mazishi yake yalifanyika shambani kwao Bulinda na yalihudhuriwa na mkewe mtarajiwa, kaka yake na watu wa afya. Majirani na ndugu wengine hawakuruhusiwa kushiriki.

“Mwili wa bwana harusi mtarajiwa ulitoka hospitalini ukiwa umeshaandaliwa hata nyumbani haukufika, ulipelekwa moja kwa moja shambani kuzikwa,” kilieleza chanzo chetu cha habari.

Reskipius Rutabingwa, kaka wa marehemu Benson alisema mdogo wake aliyekuwa mjasiriamali wa duka la nafaka na vyakula alikuwa akiishi kijiji kimoja na mchumba wake ambao walikuwa kwenye mipango ya kufunga ndoa.

“Mdogo wangu alianza kunyong’onyea tukampeleka hospitali ya Serikali ndipo alifariki dunia,” alisema

Alisema awali vipimo vilionyesha ana Malaria na UTI, hivyo alipewa dawa za magojwa hayo lakini hakupata nafuu ndipo walipoamua kumpeleka hospitalini.

“Mchumba wake anaendelea vizuri na ameshaondoka na familia yake muda si mrefu,” alisema.

Kuhusu uhusiano wa watu watatu waliofariki dunia na ugonjwa huo ambao hakutaka kuwataja majina, alisema si wa familia moja kama taarifa zinavyosambaa.

“Hatukuwa familia moja japo ni wa vijiji majirani,” alisema.

Mwingine aliyezikwa siku hiyo ni aliyekuwa mhudumu wa afya kituo cha Maruku upande wa maabara, Amos Kashumuni aliyeacha mke na watoto watatu.

Mkazi wa Kijiji cha Bulinda, Nyangoma Kulwa alisema shuguli katika kijiji hicho zinaendelea kama kawaida huku tahadhari zikiendelea kuchukuliwa ikiwemo kutosalimiana kwa kushikana mikono.

Akizungumza na waandishi wa habari na baadhi ya wahudumu wa afya katika ukumbi wa mkutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera juzi, Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel alisema majibu ya sampuli za watu hao waliofariki kwa ugonjwa huo bado hayajatoka na yakiwa tayari taarifa zitatolewa kwa umma.

“Naomba wananchi waendelee kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa yasiyojulikana na wawe wavumilivu wakati madaktari wa Serikali wakichunguza kuona sampuli za wenzetu waliofariki vifo vyao vilisababishwa na nini,” alisema Dk Mollel.

Aliwataka wananchi kutoa taarifa kwa viongozi wa eneo lao pindi wanapobaini mtu mwenye dalili za ugonjwa usiojulikana au wamripoti mgonjwa zahanati, kituo cha afya na hospitali itakayokuwa karibu nao.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila aliwasisitiza wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa mbalimbali.