Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bweni la wavulana sekondari ya Kalangalala lanusurika kuteketea

Bweni la wavulana katika Shule ya Sekondari Kalangalala, Manispaa ya Geita, lililonusurika kuteketea baada ya moto kuzuka leo wakati wanafunzi walipokuwa madarasani. Picha na Chubwa.

Muktasari:

  • Tukio hilo linatokea ikiwa ni siku kadhaa zimepita baada ya kituo cha mafuta cha Lake Oil, kilichopo mtaa wa Mwatulole,Manispaa ya Geita kuwaka moto Ijumaa Julai 10,2026 wakati gari aina ya Canter lililokuwa likijazwa mafuta kushika moto.

Geita. Bweni la wavulana katika Shule ya Sekondari Kalangalala, iliyopo Manispaa ya Geita, limenusurika kuteketea baada ya moto ambao chanzo chake bado hakijafahamika kuzuka na kuunguza kitanda kimoja pamoja na baadhi ya mali za wanafunzi.

Tukio hilo limetokea leo Julai 13, 2026 saa 6:30 mchana wakati wanafunzi walipokuwa wakiendelea na masomo darasani.

Moto huo ulibainika baada ya wanafunzi kuona moshi ukitoka katika bweni hilo linalokaliwa na wanafunzi 96.

Makamu Mkuu wa shule hiyo Antidius Deusdedit ameliambia Mwananchi kuwa walimu walipokea taarifa za moto huo kutoka kwa wanafunzi na kuchukua hatua za haraka huku wakiwasiliana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

"Tulikimbilia eneo la tukio na kuanza kupambana na moto kwa kutumia vizima moto pamoja na ndoo za mchanga kabla ya askari wa zimamoto kufika," amesema Deusdedit.

Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wakihamisha kitanda kilichoteketea kwa moto kutoka bweni la wavulana katika Shule ya Sekondari Kalangalala, Manispaa ya Geita, baada ya tukio la moto. Picha na Chubwa.

Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule hiyo, Yusuf Zacharia   amesema moto huo uligunduliwa na mwanafunzi aliyekuwa amekaa karibu na dirisha darasani.

"Tulikuwa darasani tunaendelea na masomo. Mwanafunzi aliyekuwa dirishani aliona moshi na kumjulisha mwalimu. Tulielekezwa kwenda kuuzima moto, tukachukua ndoo za mchanga na kuumwaga kwenye moto hadi ukazimika," amesema.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Geita, Keneth Mwakasitu amesema uchunguzi unaendelea kubaini chanzo halisi cha moto huo, huku dalili za awali zikionyesha huenda ulisababishwa na uzembe wa kibinadamu.

Amesema hakuna mtu aliyepoteza maisha wala kujeruhiwa kutokana na tukio hilo, kwa kuwa lilitokea wakati wanafunzi wote wakiwa madarasani.

"Madhara yaliyotokea ni madogo. godoro moja na chandarua kimoja vimeteketea. Pia baadhi ya madaftari ya wanafunzi, ndoo, vikombe, balbu zilizoharibiwa na joto pamoja na kioo cha dirisha vimeharibika," amesema Mwakasitu.

Amesema kiwango kidogo cha uharibifu kimetokana na mwitikio wa haraka wa walimu na wanafunzi pamoja na elimu ya kujikinga na majanga ya moto ambayo Jeshi la Zimamoto limekuwa likiitoa shuleni hapo.