CAG abainisha hasara mashirika matano, mawili yarejesha ruzuku kama mapato

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kishere akikabidhi ripoti ya ukaguzi wa hesabu za Serikali kwa mwaka 2022/2023 kwa Rais Samia Suluhu Hassan

Muktasari:

  • Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali amebainisha mashirika matano ya umma ambayo yamepata hasara ya mabilioni ya shilingi kwa mwaka wa fedha 2022/23.

Dar es Salaam. Licha ya hatua zinazochukuliwa na Serikali kuboresha mashirika ya umma kwa kuyapa ruzuku na kuunda kamati za watalaamu kuyasimamia, ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2022/23 imebaini mashirika matano yamepata hasara ya mabilioni ya shilingi.

Mashirika hayo ni pamoja na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Kampuni ya Mawasiliano Tanzania (TTCL), Shirika la Reli Tanzania (TRC), Kampuni ya Uwekezaji (Tanoil) na Shirika la Posta Tanzania.

Akiwasilisha ripoti ya ukaguzi kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma leo Machi 28, 2024, CAG Charles Kichere amesema ATCL imepata hasara ya Sh56.64 bilioni mwaka wa fedha 2022/23.

Hasara hiyo imeongezeka kwa asilimia 61 kutoka hasara ya Sh35.24 bilioni iliyoripotiwa katika mwaka uliotangulia.

Amesema shirika hilo lililoundiwa timu ya wataalamu inayofanya tathmini ya kiufundi, kifedha na utendaji, limepata hasara licha ya kupewa ruzuku ya Sh31.55 bilioni kutoka serikalini.

CAG amesema licha ya hilo, shirika hilo limerejesha Sh9.71 bilioni ikiwa ni sehemu ya ruzuku hiyo, kama mapatio kwa mwaka 2022/23.

Mbali na shirika hilo, Kichere ameitaja TTCL kuwa nayo imepata hasara ya Sh894 milioni, ambayo imepungua ikilinganishwa na hasara ya Sh19.23 bilioni ya mwaka uliopita.

“Shirika hilo limetengeneza hasara licha ya kupewa ruzuku ya Sh4.55 bilioni kutoka Serikalini,” aliasema akibainisha kuwa shirika hilo pia “limerudisha Sh4.4 bilioni ikiwa ni sehemu ya ruzuku hiyo kama mapato yake kwa mwaka 2022/23.”

Amelitaja pia Shirika la Reli Tanzania (TRC) akisema kwa mwaka 2022/23 nalo limepata hasara ya Sh100.7 bilioni, ikiwa imepungua kwa asilimia 47.32 ikilinganishwa na hasara ya Sh190.01 bilioni yam waka uliotangulia.

Vilevile, hasara hiyo imetokea licha ya kupokea ruzuku ya Sh32.81 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida.

Nayo Kampuni ya Uwekezaji (Tanoil), imepata hasara ya Sh76.56 bilioni kwa mwaka 2022/23 ikiwa ni ongezeko la hasara ya Sh7.48 bilioni, kutoka ile iliyoripotiwa mwaka jana ya Sh68.72 bilioni.

“Hasara hiyo ilitokana na mafuta yaliyoaghizwa kutoka nje kuzuiwa kutokana na Tanoil kushindwa kuwalipa wauzaji na gharama kubwa ya kuyahifadhi kufikia Sh12.9 bilioni ikilinganishawa na Sh6.1 bilioni kwa mwaka jana.

“Pia, mapato ya kampuni kutokana na mauzo ya mafuta yalipungua kwa Sh296 bilioni sawa na asilimia 49. Pia, kuna kupungua kwa kiwango cha mafuta ilichouza. Tanoil iliuza lita milioni 112 ikilinganishwa na lita milioni 264 za mwaka uliotangulia,” amesema.

Kwa upande wa Shirika la Posta Tanzania, Kichere amesema limepata hasara ya Sh1.34 bilioni kwa mwaka wa fedha 2022/23 ikilinganishwa na Sh16.21 bilioni mwaka uliotagulia wa 2021/22.

“Lakini faida ya mwaka uliotangulia ilitokana na mauzo ya mali za shirika, sio biashara. Hasara ya mwaka huu ilichangiwa na kupungua kwa huduma za uendeshaji zilizobaki, sawa na mwaka uliopita,” amesema.

CAG ameshauri mamlaka za umma kuboresha ufanisi wa uendeshaji, kuongeza ukusanyaji wa mapato na kupunguza gharama, kuendeleza mkakati wa kugeuza mwelekeo wa uwekezaji usio na ufanisi.

Pia, ameshauri mashirika hayo kuendeshwa na wafanyakazi wenye weledi, ubunifu na wenye ufanisi kibiashara.

“Serikali inapaswa kuimarisha usimamizi kwa kuteua wajumbe wa bodi wenye utaalamu na maarifa katika sekta husika na ujuzi wa biashara,” amesema.