CAG ang’amua makato makubwa ya mishahara
Muktasari:
CAG pia ameshauri Serikali iandae motisha kwa wafanyakazi kutokana na makato makubwa katika mishahara
Dar es Salaam. Kama Serikali itafuata ushauri wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), itakuwa ahueni kwa wafanyakazi wanaokatwa mishahara kulipa deni la mkopo wa elimu ya juu.
CAG pia ameshauri Serikali iandae motisha kwa wafanyakazi kutokana na makato makubwa katika mishahara yao yaliyosababishwa na utekelezaji wa Sheria ya Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na marekebisho ya mwaka 2004.
Hii ni baada ya CAG, Profesa Mussa Assad kubaini katika ukaguzi wake wa mwaka 2016/17 kuwa kuna wafanyakazi wanaopata chini ya theluthi moja ya mishahara yao baada ya marekebisho ya kiwango cha marejesho ya mikopo hiyo kutoka asilimia nane hadi asilimia 15 kufuatia kupitishwa kwa mabadiliko ya sheria hiyo katika Bunge mwaka 2016.
Katika ripoti ya ukaguzi wa hesabu za Serikali za Mitaa, CAG anasema watumishi 4,830 wa halmashauri 58 alizozikagua mwaka 2016/17 wanapata mishahara chini ya theluthi moja kinyume cha Sheria namba 7 ya mwaka 1970.
Pia, sheria hiyo imesisitizwa na waraka wa Novemba 28, 2012 wenye kumbukumbu namba CE.26/46/01/1/66 unaoelekeza makato katika mishahara ya watumishi yasizidi theluthi mbili ya mishahara yao ghafi.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa katika marekebisho ya sheria mpya ya HESLB ya mwaka 2016, Serikali iliamua kuanza kutumia makato ya asilimia 15 kwa ajili ya kupunguza mkopo bila kujali kiasi cha mshahara wa mtumishi kitakachosalia.
Katika ukaguzi huo, CAG anasema makato mengi kwenye mishahara ya watumishi yanaweza kuathiri utendaji na ustawi wao, hivyo kuathiri utoaji wa huduma za mamlaka za Serikali za Mitaa.
“Kiasi kikubwa cha makato ya mshahara kinaweza kusababisha mtumishi wa umma kuingia kwenye majaribu kwa urahisi na kushiriki katika matumizi mabaya ya fedha za umma; zaidi, huweza kusababisha matumizi mabaya ya ofisi kwa faida binafsi,” anasema Profesa Assad katika ripoti hiyo.
“Ninapendekeza kuwa katika siku zijazo marekebisho yoyote ya sheria yanapaswa kuzingatia mikataba iliyokuwapo awali ili kuzuia madhara kwa pande zinazohusika.
“Ilikuwa ni matarajio yangu kwamba makato mengi yangepungua kwa kipindi kirefu kutokana na kuanzishwa kwa udhibiti kwa kutumia mfumo wa Lawson serikalini, lakini hali imekuwa sivyo.”
Anasema utekelezaji wa sheria hiyo uliongeza idadi ya watumishi wanaopata mshahara chini ya theluthi moja hadi kufikia 4,830 wa halmashauri 58 ikilinganishwa na mwaka 2015/16 walipokuwa 625 kutoka halmashauri 33 na mwaka 2014/15 walipokuwa 789 wa halmashauri 16.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, msemaji wa Wizara ya Fedha, Benny Mwaipaja alisema: “Majibu ya hoja alizozitoa CAG, tutayatoa ila kwa sasa siwezi kuzungumzia hilo.”
Ushauri wa CAG umeungwa mkono na rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Tumaini Nyamhokya ambaye alisema sheria hiyo mpya ilipaswa kuanza na wanufaika wapya na si watumishi waliokuwa na mikataba ya kulipa asilimia nane ambao walikuwa wakiendelea kukatwa.
“Serikali ndiyo ilifanya makosa na inaendeleza makosa hayo. CAG ameyaona na ni kweli inavunja morali kwa watumishi,” alisema Nyamhokya.
“Mtumishi aliyekuwa akikatwa na kubakiwa na Sh500,000, leo akibaki na Sh300,000 atakuwa katika hali gani katika utendaji kazi?” alihoji Nyamhokya.
Akizungumzia pendekezo la CAG la kutoa motisha, Nyamhpokya alisema kwa hali ilivyo ya kimapato ya Serikali za Mitaa, itakuwa vigumu kutoa motisha kwa kuwa vyanzo vingi vya mapato vimechukuliwa na Serikali Kuu.
Ripoti ya CAG aliyoiwasilisha bungeni Aprili 11, inaonyesha kuwa katika majalada binafsi ya wafanyakazi wa halmashauri 19 aliyopitia, nyaraka zinazohusu madai, mahojiano na maofisa rasilimali watu alibaini kuwapo kwa madai yanayofikia Sh9.86 bilioni ambayo hayakulipwa.
“Ninatambua juhudi zilizofanywa na Serikali kumaliza tatizo la madai ya watumishi ya muda mrefu. Hata hivyo, wasiwasi wangu ni ucheleweshaji wa kulipa madai ya mfanyakazi pale yanapotakiwa kulipwa,” anasema.
“Madai yasiyolipwa kwa muda mrefu yanaongeza madeni kwa mamlaka za serikali za mitaa na yanaweza kudhoofisha morali wa watumishi katika kutoa huduma bora na kwa ufanisi kwa umma.
“Ninapendekeza kwa halmashauri na Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa kushirikiana na Hazina kuhakikisha kuwa fedha za kutosha zinatengwa kwa ajili ya kulipa madai ya wafanyakazi kwa wakati,” anasema.
Akijibu hoja zilizoibuliwa na CAG alipozungumza na waandishi wa habari bungeni mjini Dodoma jana, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alisema makusanyo ya bodi yamepanda kutoka Sh28 bilioni hadi Sh116 bilioni kwa mwaka unaoishia 2017 na mpaka Machi 2018 walishakusanya Sh132.3 bilioni.
Alisema pia wadaiwa sugu kwa mwaka huu wa fedha waliotambuliwa ni 147,231 na kati yao 42,213 wameanza kulipa mikopo yao.
Profesa Ndalichako alisema Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA) inakikagua kitengo cha ununuzi cha wizara hiyo kubaini sababu za upungufu.
Serikali pia imesema inafanya uhakiki ili kujua uhalali wa ongezeko la deni la gharama za matibabu la Sh17 bilioni kwa muda wa miezi sita lililoibuliwa katika ripoti hiyo ya CAG. Katika ripoti yake, CAG anasema deni hilo liliongezeka kutoka Sh28.60 bilioni Juni 30 mwaka 2017 hadi kufikia Sh47.73 bilioni Desemba 2017.
Jana, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu aliwaambia waandishi wa habari kuwa tathmini inafanywa na madaktari bingwa kujua gharama na aina ya matibabu kama inaendana na mkataba.
“Tumewaelekeza wataalamu wafanye tathmini ni wagonjwa wangapi walikwenda kutibiwa na kuanzia lini na walikwenda kutibiwa wapi na nini walikuwa wanatibiwa,” alisema Ummy.
Alisema tathmini hiyo inalenga katika kubaini gharama halisi za matibabu, dawa na gharama nyingine nje ya matibabu.
Ummy alisema ongezeko la asilimia 60.71 linahitaji Serikali kulifuatilia kwa makini ili kupunguza mzigo wa madeni na kuhakikisha hospitali zinalipwa kwa wakati.
“Inawezekana kuwa wengine labda walitakiwa kwenda kutibiwa moyo wakafika huko wakasema wapandikiziwe mimba au cosmetic surgery (upasuaji wa kubadilisha mwonekano wa maumbile au sura) pia kuna kuchomekewa dawa, pia wataangalia,” alisema.
Ummy alisema sababu nyingine ya uhakiki ni rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi kupungua kutoka 554 Julai 2015 – Juni 2016, kwenda 357 Julai 2016-Juni 2017. Mpaka Machi mwaka huu zimeshatolewa rufaa 42.
“Kwa hiyo kuambiwa tu madeni hayo ni ya nyuma, lazima tujiridhishe vya kutosha na kazi hii inafanywa na wataalamu,” alisema.
Alisema Serikali imetenga Sh14 bilioni za kununulia mashine ya (Pet CT-Scan), ambayo inaweza kutambua saratani mwilini badala ya kuwapeleka India.
Kuhusu wizara kutolipa Sh61.4 bilioni katika Mfuko wa Kimataifa wa Kupambana na Malaria, Ukimwi na Kifua Kikuu (Global Fund) alisema linahakikiwa ili kujua gharama halisi.
Kuhusu Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), ambako CAG alibaini kuwa bidhaa kutoka nje zenye thamani ya Dola 1.94 milioni za Marekani ziliingizwa nchini kwa kutumia vibali vya kughushi, Waziri Ummy alisema hatua zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na kulifikisha suala hilo katika vyombo vya dola na kwamba, wahusika wameshatakiwa kulipa ada na tozo ambazo hawakulipa wakati wa uingizaji wa bidhaa hizo.