Caspian yafungua kesi kuimiliki Tancoal kwa miaka miwili

Muktasari:

  • Nyaraka ambazo Mwananchi limeziona zinaonyesha kesi hiyo ilifunguliwa Agosti 15 katika Mahakama Kuu (kitengo cha biashara) ikitaka kuiweka Tancoal chini ya uangalizi kutokana na mgogoro wa malipo ya deni la Dola 6 milioni za Marekani.

Dar es Salaam. Kampuni ya Caspian imefungua kesi ikiomba kuishikilia kwa miaka miwili kampuni ya Tancoal inayoendesha mgodi wa makaa ya mawe Ngaka mkoani Ruvuma.

Nyaraka ambazo Mwananchi limeziona zinaonyesha kesi hiyo ilifunguliwa Agosti 15 katika Mahakama Kuu (kitengo cha biashara) ikitaka kuiweka Tancoal chini ya uangalizi kutokana na mgogoro wa malipo ya deni la Dola 6 milioni za Marekani.

Taarifa ambazo gazeti hili limezipata zinasema Caspian imefungua kesi namba 198 ya mwaka 2018 ili kuiweka chini ya uangalizi kampuni hiyo kufidia deni hilo. Kesi hiyo inatarajiwa kusikilizwa Septemba 21.

“Licha ya kwenda mahakamani, kwa sasa Caspian bado wanaendelea na uchimbaji wa makaa ya mawe. Tancoal inajipanga kujibu madai hayo ambayo inasema haiwezi kulipa kwa sababu (Caspian) walidanganya uwezo wao kwa maelezo kwamba walichelewa kuanza uzalishaji na walikiuka mkataba kwa kuzalisha kiwango kidogo ndani ya saa 300 za makubaliano kila mwezi,” kilieleza chanzo cha kuaminika.

Serikali kupitia Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) inamiliki asilimia 30 ya hisa za Tancoal na asilimia 70 zilizobaki zikiwa mali ya kampuni ya Intra Energy Corporation (IEC). Endapo maombi ya Caspian yatapata kibali cha mahakama itamaanisha kuvunjwa kwa bodi ya wakurugenzi wa Tancoal na menejimenti kwa miaka miwili na majukumu yao kuwa chini ya Caspian.

Mgogoro

Machi 8, Wizara ya Viwanda na Biashara ilitoa agizo kwa kampuni ya Tancoal kuongeza uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya soko hasa kwa viwanda vya saruji nchini.

Wakati Serikali inatoa agizo hilo la siku nne, uongozi wa Tancoal ulikuwa na mkataba na Caspian tangu mwanzoni mwa mwaka jana unaoitaka Caspian kufanya kazi kwa saa 300 kila mwezi.

Kutokana na mkataba huo Caspian ilitoa mitambo ya uchimbaji ambayo inaelezwa kuwa haikukidhi matarajio ya Tancoal, hivyo kuishawishi kufanya majadiliano mapya ya kurekebisha mkataba, lakini Caspian haikuwa tayari kufanya hivyo.

Hata hivyo vyanzo vya ndani vinaeleza kuwa makubaliano ya mkataba huo yaliingiza Tancoal kwenye gharama kubwa za uendeshaji kutokana na madai ya uwezo mdogo wa Caspian.

“Ni mkataba mbovu, ndiyo maana Tancoal iliomba kuurejea upya lakini Caspian walikataa. Tancoal ilisitisha malipo ya deni ililonalo ikitaka mabadiliko ya mkataba,” kilisema chanzo hicho.

Taarifa zinasema Caspian imeikodisha Tancoal mitambo ambayo baadhi imeshatumika kwa zaidi ya miaka 19, jambo linaloifanya iwe na ufanisi mdogo huku ikitumia mafuta mara mbili ya gharama za kawaida kiasi cha kuomba iwe inazimwa kila baada ya saa 300 ili kupunguza gharama hizo.