CCK yawachongea watumishi Pwani

Muktasari:

  • Chama Cha Kijamii (CCK) kimetaka kufanyika uchunguzi wa kina na kuchukua hatua za kinidhamu na kisheria dhi ya watumishi wasio waaminifu ambao wamekuwa sababu ya migogoro ya ardhi maeneo mbalimbali nchini.

Kibaha. Chama Cha Kijamii (CCK) kimetaka kufanyika uchunguzi wa kina na kuchukua hatua za kinidhamu na kisheria dhi ya watumishi wasio waaminifu ambao wamekuwa sababu ya migogoro ya ardhi maeneo mbalimbali nchini.

Wito huo umetolewa Novemba 3, 2023; na viongozi wakuu wa chama hicho katika mahojiano maalum na Mwananchi Digital, muda muda mfupi baada ya kumalizika kwa mkutano wa viongozi wa Mkoa wa Pwani uliofanyika Mjini Kibaha.

Katika mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na Mkurugenzi wa Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mabhare Matinyi, viongozi wa chama hicho walikuwa miongoni mwa waalikwa.

"Migogoro ya ardhi imeendelea kuibuka kila kukicha, ukifuatilia utaambiwa baadhi ya watendaji wa Serikali katika kuanzi ngazi za mitaa na vitongoji mpaka kwenye halmashauri, ambao wanadaiwa kuhusika, hivyo ni vema sasa dawa hiyo ikafanyika ili kukomesha hilo," amesema Dk Gabriel Mziwanda Katibu Mkuu CCK.

Dk Mziwanda anaonekana kuumizwa na migogoro hiyo na kusema: “Hii migogoro imekuwa ikichangia kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi kwa kujikuta wanaacha shughuli za kiuchumi na kufutilia haki zao kwenye mahakama na mabaraza ya ardhi jambo ambalo ni hatari.”

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa chama hicho, Jesca Rutahuila, amesema kuwa wakati umefika ambao Serikali inapaswa kutumia nguvu ya ziada ili kukabiliana na migogoro ya ardhi na kubwa ni kuwamulika wahusika ambao baadhi yao ni watumishi wa Serikali ngazi za Halmashauri.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge katika mkutano huo, amesema kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakijiingiza kwenye migogoro kwa kutokuwa na uelewa wa maswala ya kisheria.

“Tumekuwa tukishughulikia migogoro ya ardhi kwa njia mbalimbali ikiwemo ya mashauriano na pande mbili na wanapofikia makubaliano basi tunayamaliza lakini njia zingine ni kupitia hatua za kisheria," amesema Kunenge.

Kwa mujibu wa RC huyo wa Pwani, kazi yake kubwa ni kusikiliza kero na malalamiko, kisha kuunda timu ya kufanya uchunguzi na inapobainika mwenye haki, jambo linalofuata ni kuzikutanisha pande zote kísha kueleza ukweli na uhalisia na kutoa ushauri wa namna ya kusuluhisha.

Aidha, Kunege amewataka wakazi mkoani humo, kutovamia maeneo ya ardhi na kujenga au kuuza kwani kufanya hivyo ni kuvunja sheria za nchi.

"Nawaomba hata nyinyi waandishi wa habari msisite kutoa elimu kwa wananchi watambue sheria na namna ya kumiliki ardhi kihalali," amesema.

Baadhi ya migogorp ya ardhi mikubwa mkoani Pwani ni pamoja na ule wa Mitamba, Kikongo na Razaba na katika maeneo ya kambi za Jeshi katika wilaya za Kisarawe, Mafia, Kibiti na Chalinze mtawalia.

Kwa upande wake, Matinyi amesema kuwa Serikali imeendelea kuwatumikia wananchi wake ikiwemo kuboresha miundombinu na kuwasogezea huduma muhimu.

Aidha katika taarifa za utekelezaji shughuli za maendeleo zilizowasilishwa na wakurugenzi wa Halmashauri za mkoani huo, imeonyesha kuwepo kwa ongezeko la fedha za miradi ya maendeleo.

Hii inatokana na wasilisho la Mhandisi wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), mkoani Pwani, Leopold Runji ambapo amesema kwa miaka mitatu 2021/2023 tayari wameepokea Sh84 bilioni zilizowekezwa katika ujenzi wa kilometa 95.6 za barabara kwa za kiwango cha lami, huku zile za kiwango cha changarawe zikiwa ni kilometa 1,600 za changarawe kati ya km 5,140 zilizopo chini ya wakala huo.