CCM Kilimanjaro ‘yacharuka’ uhujumu wa mradi wa maji
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi (katikati) akizungumza katika ziara hiyo
Muktasari:
- Serikali ya Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, imetakiwa kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria watu wote waliohusika na uhujumu wa miundombinu ya mradi wa maji katika Kata ya Kileo wilayani humo.
Mwanga. Serikali ya Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, imetakiwa kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria watu wote ambao wamehusika na uhujumu wa miundombinu ya mradi wa maji katika Kata ya Kileo wilayani humo.
Rai hiyo imetolewa leo Jumatatu Juni 12, 2023 na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi wakati kamati ya siasa ya chama hicho mkoa ilipotembelea mradi wa maji wa vijiji vya kivulini na Kileo ambao unatarajiwa kugharimu Sh1.3 bililion hadi kukamilika.
Boisafi emetoa kauli hiyo, kufuatia taarifa ya mabomba yenye urefu wa mita 400 kufukuliwa na baadhi ya wananchi katika Kata hiyo ya Kileo, ambapo amesema Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kutekeleza miradi hiyo na kwamba chama hakitaweza kuwavumilia watu wa namna hiyo.
"Mradi unajengwa na wanufaika ni nyinyi jambo ambalo limejitokeza kwamba mita 400 za mabomba ya miundombinu ya maji imefukuliwa, waliohusika ni wananchi wa hapa, hakuna aliyetoka nje, ni ninyi wenyewe kwa sababu ya tamaa zenu ambazo hazijengi"
"Niwaombe tuwe wazalendo na hofu ya Mungu, kazi hizi haziwezi kufanyika kirahisi hivyo, kwani unapoona fedha zimekuja zinatekeleza mradi halafu kuna baadhi ya watu wanakuja kuhujumu, hao ni watu wabaya,”ameongeza.
Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Abdallah Mwaipaya amesema katika utekekezaji wa mradi huo wa maji zipo changamoto mbalimbali ikiwemo baadhi ya wananchi kuhujumu miiundombinu kwa kufukua mabomba yenye urefu wa mita 400.
"Miradi hii ya maji inakabiliwa na changamoto nyingi hasa za wakazi wa eneo hili, baadhi ya wananchi wamefukua mabomba yaliyowekwa mita 400, na tayari wapo ambao tumewakamata,"amesema.
Akizungumza Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema zaidi ya Sh2bilioni zimetolewa na serikali kwa ajili ya utekekezaji wa miradi ya maji Kata ya Kileo na kuwataka wananchi kuilinda miundombini ya maji ili miradi hiyo iweze kuwa endelevu.
"Wananchi tunapaswa kulinda miundombinu ya maji, hakuna mtu ambaye yuko juu ya sheria, ukifanya kosa unachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria, lakini pia niwaombe vijana, kunapotokea utekelezaji wa miradi kama hii, mjitokeze kushiriki,”amesema.