Prime
Fedha za vyama zinavyowang’oa vigogo upinzani
Katibu Mkuu Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu
Muktasari:
- Katika miaka ya karibuni, baadhi ya vyama vilivyowahi kushuhudia viongozi wakiondolewa kutokana na madai yanayohusishwa na usimamizi wa fedha ni pamoja na Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992, usimamizi wa fedha ndani ya vyama vya siasa, hususan vya upinzani, umeendelea kuwa moja ya maeneo yanayozua migogoro, mifarakano na hali ya kutokuaminiana kati ya viongozi na wanachama.
Fedha hizo, ambazo mara nyingi hutolewa na wadau mbalimbali kwa lengo la kusaidia shughuli za kisiasa, hususan maandalizi ya uchaguzi wa ndani na uchaguzi mkuu, zimekuwa zikitarajiwa kuimarisha uhai na maendeleo ya vyama.
Hata hivyo, katika baadhi ya nyakati, zimegeuka kuwa chanzo cha migogoro badala ya kuwa nyenzo ya kujenga taasisi hizo.
Miongoni mwa sababu zinazotajwa ni madai kwamba wakati mwingine fedha hizo hutolewa nje ya mifumo rasmi ya kifedha ya vyama, hali inayotoa mwanya kwa baadhi ya viongozi wasiokuwa waaminifu kuzitumia kwa manufaa binafsi badala ya kuelekezwa katika shughuli zilizokusudiwa.
Matokeo yake, baadhi ya vyama vimejikuta vikikumbwa na migongano kati ya viongozi na wanachama, huku wengine wakiondolewa madarakani au kupoteza ushawishi wao kisiasa kutokana na tuhuma za matumizi mabaya ya fedha au kujinufaisha nazo.
Katika miaka ya karibuni, baadhi ya vyama vilivyowahi kushuhudia viongozi wakiondolewa kutokana na madai yanayohusishwa na usimamizi wa fedha ni pamoja na Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imekuwa ikieleza kuwa usimamizi wa fedha unaendelea kuwa miongoni mwa changamoto zinazoibua migogoro ndani ya vyama vya siasa, licha ya maboresho ya sheria na kanuni yanayofanyika mara kwa mara.
Kwa upande mwingine, baadhi ya wachambuzi wa siasa wanasema chanzo kikuu cha migogoro hiyo ni kukosekana kwa mifumo madhubuti ya usimamizi wa fedha inayoweza kuhakikisha mapato na matumizi ya vyama yanasimamiwa kwa uwazi, uwajibikaji na kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.
Kisa cha Chaumma
Mfano wa karibuni ni ndani ya Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), ambako aliyekuwa Katibu Mkuu, Salum Mwalimu, aliondolewa madarakani baada ya kukabiliwa na tuhuma mbalimbali, ikiwamo matumizi mabaya ya ofisi na madai ya ubadhirifu wa fedha alizodaiwa kupokea kutoka kwa wadau kwa ajili ya shughuli za chama.
Kwa mujibu wa taarifa za chama hicho, tuhuma hizo ziliwasilishwa na baadhi ya wajumbe wa Sekretarieti katika kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika Juni 29, 2026, makao makuu ya chama, kufuatia kuwasilishwa kwa waraka wa kutokuwa na imani naye.
Katika kikao hicho, Mwalimu alipewa nafasi ya kujitetea. Kwa mujibu wa vyanzo vya ndani ya chama, alikiri baadhi ya tuhuma zilizokuwa zikimkabili na kuomba kujiuzulu.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Katiba ya Chaumma, Kamati Kuu ilipaswa kupiga kura ili kuamua kama bado ilikuwa na imani naye. Wajumbe wote walipiga kura ya kutokuwa na imani naye.
Uamuzi huo uliwasilishwa katika kikao cha Halmashauri Kuu kilichofanyika Juni 30, 2026, ambapo wajumbe waliridhia kwa kauli moja kumwondoa katika nafasi ya Katibu Mkuu.
Baada ya uamuzi huo, Mwenyekiti wa Chaumma, Hashimu Rungwe, alitangaza kumvua Salum Mwalimu wadhifa huo na kumteua Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, Benson Kigaila, kuwa Kaimu Katibu Mkuu hadi uchaguzi mkuu wa chama utakapofanyika.
Kwa mujibu wa Rungwe, Mwalimu ataendelea kubaki mwanachama wa kawaida na kushiriki shughuli za chama kupitia tawi lake.
Wachambuzi wamulika chanzo cha migogoro
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (Suza), Dk Abdallah Mkumbukwa anasema vyama vingi vya siasa, hususan vya upinzani, vinaendelea kukabiliwa na migogoro kutokana na kukosekana kwa mifumo madhubuti ya usimamizi wa fedha.
Anasema migogoro hiyo hujitokeza zaidi baada ya uchaguzi, ambapo masuala ya fedha huwa chanzo kikuu cha sintofahamu kati ya viongozi na wanachama.
“Vyama vingi vimekuwa vikikumbwa na migogoro baada ya uchaguzi, na kichocheo kikubwa ni fedha. Kumekuwa na usiri mkubwa katika eneo hilo, na migogoro inapoanza mara nyingi hukosekana mifumo au watu wenye uwezo wa kuisimamia na kuifikisha kwenye suluhu,” anasema.
Kwa mujibu wa Dk Mkumbukwa, changamoto nyingi zinazovikabili vyama vya siasa huanzia katika namna fedha zinavyopokelewa, kusimamiwa na kutumika.
Hata hivyo, anasema baadhi ya vyama vikubwa vimefanikiwa kupunguza migogoro ya aina hiyo kwa kuanzisha vyombo maalumu vinavyosimamia fedha na kuhakikisha kunakuwa na uwajibikaji.
Baraza la Vyama lasisitiza uadilifu
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ali Khatibu, anasema ukosefu wa uadilifu na uaminifu miongoni mwa baadhi ya viongozi ni miongoni mwa changamoto zinazochangia migogoro ndani ya vyama vya siasa.
Anasema baadhi ya viongozi wamekuwa wakipokea fedha kutoka kwa wadau moja kwa moja, kinyume na taratibu za kifedha za vyama.
“Fedha za chama zinapaswa kupitishwa katika mifumo rasmi ya chama, ikiwamo kuwekwa kwenye akaunti za chama. Vilevile, fedha hizo zinapotakiwa kutumika, lazima ziidhinishwe na vikao halali vya chama,” anasema.
Kwa mujibu wa Khatibu, baadhi ya viongozi hupokea fedha mikononi na wakati mwingine hushindwa kuziwasilisha kwa chama. Hata wanapofanya hivyo, hawazipeleki katika idara husika, hususan kitengo cha fedha, hali inayodhoofisha mifumo ya uwajibikaji na kuwafanya baadhi ya viongozi kujihusisha na majukumu yasiyowahusu.
Wito wa kuimarisha uwajibikaji
Kwa upande wake, Profesa George Kahangwa anashauri kila chama cha siasa kuanzisha kitengo cha kudhibiti rushwa ili kuimarisha uwajibikaji, hususan katika vipindi vya uchaguzi ambavyo matumizi ya fedha huongezeka na huweza kutoa mianya ya vitendo vya rushwa.
“Mapambano dhidi ya rushwa yanapaswa kuanzia ndani ya vyama vya siasa. Kuanzishwa kwa vitengo maalumu vya kudhibiti rushwa kutasaidia kuzuia matumizi mabaya ya fedha na kuongeza uwazi katika uendeshaji wa shughuli za vyama,” anasema.
Profesa Kahangwa anasema vyama vya siasa ni taasisi za umma, hivyo vinapaswa kusimamia fedha zake kwa uwazi na kuwajibika kwa wanachama na umma kwa ujumla.
Anasema kumekuwapo hofu kwamba baadhi ya fedha zinazotolewa na wadau hulenga kushawishi misimamo ya vyama, huku nyingine zikidaiwa kutumika katika vitendo vya utakatishaji fedha.
“Ni muhimu kuwe na mifumo madhubuti ya ufuatiliaji wa fedha. Kama taasisi nyingine zinavyowasilisha taarifa za matumizi ya fedha kwa umma, hata vyama vya siasa vinapaswa kufanya hivyo ili kuongeza uwazi na kuimarisha imani ya wananchi,” anasema.
Profesa Kahangwa anasema changamoto nyingine ni uwepo wa baadhi ya watu wanaojiunga na vyama vya siasa kwa lengo la kujinufaisha binafsi badala ya kulitumikia Taifa.
“Wapo wanaoingia kwenye siasa kwa maslahi binafsi badala ya dhamira ya kulitumikia Taifa. Watu wa aina hiyo ni rahisi kushawishika na wakati mwingine hugeuza vyama kuwa sehemu ya kutafuta manufaa binafsi,” anasema.
Kwa mujibu wake, viongozi wenye malengo ya kujitajirisha huathiri maendeleo ya vyama kwa kuwa hutanguliza maslahi yao badala ya kuweka mikakati ya muda mrefu ya kukijenga chama.
Aidha, anasema wakati mwingine viongozi wamekuwa wakigawa au kutumia fedha nje ya utaratibu, huku migogoro inayozuka baadaye isimaanishe kuwa wanaolalamika ni waadilifu zaidi, bali mara nyingine hutokana na kutoridhishwa na namna fedha hizo zilivyogawanywa.
Profesa Kahangwa anaeleza kuwa migogoro ya kuwaondoa wenyeviti na makatibu wa vyama imekuwepo kwa muda mrefu tangu baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995. Kwa maoni yake, migogoro mingi huibuka baada ya uchaguzi kutokana na kutofautiana kuhusu usimamizi na matumizi ya fedha zinazopokelewa kutoka kwa wadau.
“Palipo na mzoga ndipo tai hukusanyika,” anasema, akimaanisha kuwa penye maslahi makubwa ndipo migogoro na makundi ya kugombea maslahi hujitokeza kwa urahisi zaidi.
Ofisi ya Msajili yakiri
Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, anakiri kuwa usimamizi wa fedha unaendelea kuwa miongoni mwa changamoto zinazosababisha migogoro katika vyama vya siasa nchini, ikiwamo Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma).
Anasema changamoto za usimamizi wa fedha si za vyama vya siasa pekee, bali zinajitokeza hata katika taasisi nyingine na familia, jambo ambalo limeifanya Serikali kuendelea kuboresha sheria na kanuni ili kuimarisha uwazi na uwajibikaji.
“Eneo la fedha lina changamoto si kwa vyama vya siasa pekee, hata katika familia. Ndiyo maana Bunge limekuwa likifanya maboresho ya sheria mara kwa mara ili kuimarisha usimamizi wa fedha. Hata Sheria ya Fedha ya mwaka 2009 imeendelea kuboreshwa ili kuhakikisha mapato ya vyama yanakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),” anasema.
Kwa mujibu wa Nyahoza, awali vyama vya siasa vilikuwa vinakaguliwa na wakaguzi wao wa ndani.
Hata hivyo, ilibainika kuwa katika baadhi ya matukio kulikuwa na udhaifu katika utoaji wa taarifa za kifedha, hali iliyoibua haja ya kuimarisha mfumo wa ukaguzi. Anasema kutokana na changamoto hizo, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ilipendekeza kufanyika kwa marekebisho ya sheria ili kumpa CAG mamlaka ya kukagua hesabu za vyama vya siasa.
“Hatua hiyo ililenga kuimarisha usimamizi wa fedha. Baadaye, mwaka 2019, zilitungwa Kanuni za Fedha za Vyama vya Siasa (Political Parties Financial Regulations) ili kuongeza uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha za vyama,” anasema.
Nyahoza anaeleza kuwa mwaka 2024 yalifanyika tena maboresho ya sheria na kanuni kwa lengo la kuhakikisha kila chama kinakuwa na maofisa wanaosimamia fedha pamoja na mifumo madhubuti ya ukaguzi wa ndani.
“Kwa sasa kila chama kinapaswa kuwa na kanuni za usimamizi wa fedha. Marekebisho ya mwaka 2024 yalilenga kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika eneo hilo. Sambamba na hilo, kila mwaka tunatoa mafunzo kwa makatibu wakuu, waweka hazina na maofisa ununuzi wa vyama vya siasa,” anasema.
Anasema sheria pia inazitaka fedha zote za vyama kupitishwa katika akaunti rasmi za chama, huku Ofisi ya Msajili ikiendelea kufuatilia utekelezaji wa matakwa hayo kupitia mafunzo na uhakiki wa kila mwaka. “Tunafanya uhakiki wa vyama kila mwaka ili kuona kama vinazingatia sheria na masharti yaliyowekwa. Chama kinachobainika kukiuka hatua huchukuliwa. Mfano, mwaka 2017 tuliwasitishia ruzuku kwa kipindi cha mwaka mmoja ACT-Wazalendo baada ya kushindwa kuwasilisha taarifa za fedha zilizopaswa kukaguliwa na CAG,” anasema.
Kwa mujibu wa Nyahoza, mifumo ya usimamizi wa fedha inaendelea kuimarishwa sambamba na utoaji wa elimu kwa viongozi wa vyama vya siasa. Hata hivyo, anasisitiza kuwa mafanikio ya hatua hizo yanategemea pia uadilifu, busara na utayari wa viongozi kuzingatia sheria na kanuni zilizopo.
“Mambo mengine yanahitaji busara, hekima na maadili. Viongozi wanapaswa kuwa wazi kwa sababu eneo la fedha ndilo linalochochea migogoro mingi ndani ya vyama vya siasa,” anasema.
Nyahoza anasema tangu Ofisi ya Msajili ilipoanza kutoa mafunzo kwa viongozi wa vyama, migogoro inayohusishwa na masuala ya fedha imepungua kwa kiwango kikubwa. Aidha, anasema hata idadi ya vyama vinavyopata hati zenye mashaka kupitia ripoti za CAG imeendelea kupungua.
“Tatizo halijaisha kabisa, kama inavyoonekana katika mgogoro wa Chaumma, lakini linaendelea kupungua. Kama wasimamizi hatuwezi kuacha kutoa elimu, kuboresha sheria na kuchukua hatua za kinidhamu ili kuhakikisha eneo la fedha linasimamiwa kwa kuzingatia sheria na viongozi wa vyama wanawajibika ipasavyo,” anasema.