Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UCHAMBUZI WA MALOTO: Mwalimu anaondoshwa kwenye uongozi Chaumma, jina linalochafuka ni la Mbowe

New Content Item (1)



Utamu wa hadithi si pale inapoishia.  Simulizi ya Salum Mwalimu na wenzake, inaanzia Januari 22, 2025. Ilikuwa asubuhi mapema, pigo zito likatengeneza mwanzo wa hatima.

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwa miaka 22, aliangushwa kwenye uchaguzi na makamu wake, Tundu Lissu. Haukuwa uchaguzi, bali mapambano ya hatima. Nani atoke, yupi abaki.

Kampeni zilikuwa chafu. Pande mbili zilichagua kufanya siasa za kumalizana. Ama zao, ama zetu, ilikuwa ari ya kupasuana. Mbowe baada ya kushinda, akatoa wosia kwa viongozi wapya: “Mimi niliahidi kuwa kama ningeshinda ningeunda kamati ya ukweli na maridhiano ili watu wazungumze na kutibu majeraha yaliyoletwa na kampeni. Sasa, ikiwa mnaniheshimu kama baba, basi nawaagiza Lissu na viongozi wenzako wapya mlete maridhiano baada ya majeraha yaliyoletwa na kampeni.”

Zilikuwepo jitihada za kuunganisha watu. Lissu na Kamati Kuu ya Chadema, yote ilikwenda Bagamoyo kutibu nyufa. Haikuchukua muda, sauti zikaanza kutoka nje. Ilishindikana kuifanya Chadema kubaki moja. Kikazaliwa kikundi, kikaitwa G55. Ni wana-Chadema waliojipambanua kutoafikiana na misimamo ya viongozi wa chama. Mgogoro mkubwa ukawa ushiriki wa Chadema kwenye Uchaguzi Mkuu 2025.

Mikutano kadhaa na waandishi wa habari. Aliyekuwa Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, mara kwa mara alikuwa nyuma ya ‘maikrofoni’ za wana habari. Pembeni ya Mrema, ungemwona aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Chadema, Benson Kigaila. Zilikuwa zama za vuguvugu katikati ya harakati.

Jambo moja lilikuwa dhahiri. Viongozi waliojipambanua kuwa timu ya Mbowe. Kisha, wakawekwa kando baada ya Lissu kushika hatamu, walikuwa ndiyo vinara wa G55. Yaliyojiri baadaye yalikuwa na majibu kuwa zile vuguvugu za mwanzo, hazikuwa harakati za kuuasa uongozi kufanya mabadiliko ya misimamo yake, bali utunzi wa hadithi ya kisingizio cha kuondokea nyumbani.

Kikapita kipindi tambo na vijembe vilisikika. “Uongozi huu wa Chadema hautafikisha hata miezi mitatu, chama kitakuwa kimesambaratika.” Ulikuwa utabiri wa anguko la Chadema kwenye mikono ya Lissu. Ukafuata uvumi ulioenea kama moto nyikani. Kwamba, G55 na wengine waliokuwa timu ya Mbowe, wanahamia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma).

Jua lilichomoza, siku ikawa imeanza, likakaa utosini. Mchana tayari. Likazeeka, ni jioni hiyo. Usiku ukawadia. Ikafuata siku nyingine. Tangazo likatoka, kweli Chaumma ilivuna wana-Chadema. Tena viongozi.

Mwalimu, Mrema, Kigaila, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Kati, Devotha Minja, hiyo ni kutaja wachache. Minja Makamu Mwenyekiti Chaumma, Tanzania Bara. Mwalimu Katibu Mkuu mpya Chaumma. Kigaila Naibu Katibu Mkuu. Mrema Mkurugenzi wa Mawasiliano.

Uvumi kuwa Mbowe angegombea urais kupitia Chaumma, ulibaki kuwa uvumi. Mwalimu akachukua leseni ya chama, akaizunguka nchi akiahidi kuwa “rais wa masela,” mgombea mwenza alikuwa Minja.

Baada ya uchaguzi, hazikuonekana tena harakati za chama. Wenye matumaini wakasema, “tuvute Subira,” wapo waliotamba kuwa Chaumma ilikuwa ikijipanga kuchukua nafasi ya Chadema, na kuwa chama kikuu cha upinzani Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katikati ya viulizo na matumaini, uso wa jamii ukashitushwa na taarifa ya Mwalimu kuomba kujiweka kando kupisha uchunguzi dhidi yake.

Oooh, kumbe alikuwa akituhumiwa kwa mwenendo mbaya ndani ya Chaumma! Siku moja baada ya Mwalimu kuomba kujiweka pembeni, Mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe, akatokeza mbele ya waandishi wa habari na kutangaza uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Chaumma wa kumvua ukatibu mkuu Mwalimu.

Nazikumbuka zile shamrashamra za Mei 19, 2025. Mwalimu, Minja, Kigaila, Mrema, aliyekuwa Katibu wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Catherine Ruge, na wengine, wakiwa wamevaa fulana za Chaumma, wakionesha kadi zao za uanachama wa chama hicho. Picha nyingine ya utambulisho wao, katikati yao akiwa Rungwe.

Ilibeba tafsiri ya wanasiasa waliochagua malisho mema, kwa ajili ya kufanya siasa zenye uzani.

Unazungumzia mwaka mmoja, mwezi mmoja, na siku 12 tu. Hizo ndiyo tarakimu za muda ambao Mwalimu amekuwa Katibu Mkuu Chaumma.  Waliotabiri anguko la miezi mitatu Chadema kwenye mikono ya Lissu, wanakuwa wa kwanza kutia fora, kwa kufukuzana ndani ya miezi 13 na siku 12, tangu zile shamrashamra zao zao kuhamia chama na kukipa pumzi mpya.

Kigaila amesema, Mwalimu ni samaki aliyeoza, hivyo ameondolewa.  Maana yake, wao waliobaki wote ni safi. Wahenga waliokijenga Kiswahili na methali zake, walisema, samaki mmoja akioza wameoza wote. Na hapa ndipo palipo na wasiwasi kuhusu dhamira yao ya kuondoka Chadema. Je, nani anaweza kuwaamini leo kuwa walikuwa na haki ya kusema yote waliyosema, kuupinga uongozi mpya Chadema, kisha kuhamia Chaumma? Bila shaka, timu iliyohama Chadema na kutimkia Chaumma, ikiongozwa na Mwalimu, itapata wakati mgumu kujieleza kuwa wao hawakuwa wakorofi, isipokuwa Lissu na timu yake.

Mbowe ni mwanasiasa aliyejenga heshima yake tangu mwanzo wa vuguvugu la kuanzisha vyama vingi vya siasa. Akawa kijana zaidi kwenye timu iliyoasisi Chadema. Akawa kiongozi wa vijana wa Chadema, mbunge, Mwenyekiti wa Chadema, Kiongozi wa Upinzani Bungeni kwa mihula miwili. Mnapotembea na jina la mtu wa aina hiyo, mnapaswa kuchunga nyendo zenu. Mwendo wenu mzuri, utampa heshima. Mkienda vibaya mnamchafua. Iwe kwa ukweli au uzushi wao, walitakiwa kufahamu kwamba mwendo wowote wa hovyo, watu watageuka nyuma na kumtazama Mbowe. Hata hivyo, baada ya Mwalimu kufukuzwa uongozi Chaumma, na Kigaila kuonekana ni sehemu a waliobeba bango la kufukuzwa msafiri mwenzake kutoka Chadema, wapo watu wanaona kumbe ilikuwa sawa Mbowe kutoendelea na uenyekiti, maana wanaofukuzana Chaumma, ndiyo wangekuwa kwenye safu za juu za uongozi Chadema. Bila shaka, hata Mbowe mwenyewe baada ya kusikia mvurugano wa Mwalimu na wenzake Chaumma, atakuwa anakuna kichwa na kusikitika. Yeye ni kiongozi na mwalimu wao siasa. Inakuwaje wanafunzi wake wanagombana na kutimuana? Hawana uvumilivu au ipo tamaa ambayo imewafanya wasahau walipotoka? Kung’olewa kwa Mwalimu ni alama ya ushindi kwa viongozi wapya Chadema, ambao waliamua kuwaweka kando, kisha wao wakahama.

Hiyo ndiyo hadithi. Ilivyoanza ndivyo inavyotengeneza matukio katikati ya safari. Je, ni kweli Mwalimu alikuwa kirusi, kwa hiyo baada ya kumtimua sasa Chaumma itaamka na kutikisa siasa za nchi? Vipi kuondoka kwa Mwalimu itakuwa ndiyo mwisho wa jumla wa Chaumma? Muda ni hakimu wa kila kitu. Tuvute subira. Tuitazame Chaumma. Inaweza kufanya maajabu. Inawezekana pia yenyewe ndiyo ikawa maajabu.