Prime
Sababu za Chaumma kumng’oa Mwalimu
Muktasari:
- Mwalimu aliondolewa kwenye wadhifa huo, juzi baada ya kura ya kutokuwa na imani naye iliyopigwa na wajumbe wa halmashauri kuu na hatimaye, mwenyekiti Hashim Rungwe, maarufu Mzee wa Ubwabwa akatengua uteuzi wake
Dar es Salaam. Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), kimesema uamuzi wake wa kumuondoa Salum Mwalimu kuwa katibu mkuu wake, umetokana na madai mbalimbali ikiwamo kupoka mamlaka ya mwenyekiti.
Mwalimu aliondolewa kwenye wadhifa huo, juzi baada ya kura ya kutokuwa na imani naye iliyopigwa na wajumbe wa halmashauri kuu na hatimaye, mwenyekiti Hashim Rungwe, maarufu Mzee wa Ubwabwa akatengua uteuzi wake.
Badala yake, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Bara, Benson Kigaila ameteuliwa kukaimu nafasi hiyo hadi hapo uchaguzi utakapofanyika.
Kabla ya kung'olewa, mapema asubuhi ya juzi, Mwalimu aliwasilisha barua kwa mwenyekiti, akiomba kuundwe timu ya kuchunguza tuhuma zinazomkabili, akisema yupo tayari kuwa nje ya ofisi kupisha uchunguzi huo.
Mwalimu aliukwaa wadhifa huo Mei 19, mwaka jana, siku ambayo ndiyo alijiunga rasmi na chama hicho, baada ya kuondoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Akizungumza baada ya uamuzi huo mbele ya waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe amedai kulikuwa na tuhuma mbalimbali zinazomkabili Mwalimu, ikiwamo kupoka mamlaka ya mwenyekiti.
Tuhuma nyingine, Rungwe amedai Mwalimu alijifanya msemaji wa chama bila idhini, kutokuwa muwazi katika shughuli za uendeshaji wa chama na kubadili uamuzi halali uliopitishwa na chama na kuwa na msimamo wake binafsi.
"Mwalimu alikuwa akipoka mamlaka ya mwenyekiti bila idhini yangu. Amekuwa akibadilisha misimamo halali ya chama na kuwasilisha misimamo yake binafsi kana kwamba ndiyo ya chama,” amedai.
Rungwe amesema ofisi ya katibu mkuu ina watendaji wengi, lakini hatua ya kwanza ilikuwa kumuondoa kiongozi mkuu, endapo uchunguzi utabaini kuwapo kwa viongozi au watendaji wengine waliohusika na tuhuma hizo, watachukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa katiba ya chama.
"Chama hiki kinahitaji uwazi katika utendaji wake. mimi kama mwenyekiti, sina jambo la kuficha ndani ya chama. Ninataka kila jambo lifanyike kwa uwazi kwa sababu shughuli za chama si mali binafsi ya mtu. Kinachotakiwa ni kufuata taratibu na katiba ya chama," amesema.
Kaimu Katibu Mkuu Benson Kigaila, amedai kuwa, Mwalimu ameondolewa madarakani baada ya kujadiliwa na Kamati Kuu kufuatia tuhuma zilizokuwa zikimkabili na alipewa nafasi ya kujitetea.
"Mwalimu mwenyewe alikiri mbele ya Kamati Kuu na hata akaomba kujiuzulu. Hivyo, alikuwa anafahamu tuhuma hizo zilimhusu yeye binafsi. Uchunguzi ulianzishwa na Sekretarieti ya chama ambayo amekuwa akiifanyia kazi akiwa katibu mkuu," amesema.
Amesema kama kungekuwa na ushahidi wa kuwapo kwa watu wengine waliohusika, Sekretarieti ingewajumuisha katika uchunguzi huo.
"Kama alivyosema mwenyekiti, endapo itabainika kuna mtu mwingine aliyeshiriki matendo hayo, naye atachukuliwa hatua kwa mujibu wa katiba ya chama. Kwa sasa tumemwondoa kwanza aliyebainika kuwa na makosa," amesema.
Kigaila amesema baada ya kutenguliwa, Mwalimu ataendelea kuwa mwanachama wa kawaida wa Chaumma na hatahusika tena katika vikao vya uamuzi vinavyohitaji mtu mwenye wadhifa wa uongozi.
"Baada ya kutenguliwa, Mwalimu atabaki kuwa mwanachama wa kawaida. Atashiriki shughuli za chama katika ngazi ya tawi lake, kwa kuwa kila mwanachama ni mjumbe wa mkutano mkuu wa tawi," amesema.
Aidha, Kigaila amesema baada ya kukamilisha suala hilo, chama kinaendelea na utekelezaji wa mipango yake, ikiwamo kufanya kikao maalumu cha kutafuta rasilimali za kukiendesha chama.
"Ingawa wadau wanatuchangia, hatuwezi kutegemea misaada yao pekee. Tunahitaji kila mwanachama achangie ili chama kiweze kupiga hatua. Baada ya mkutano huu tunaelekea kupanga mikakati hiyo," amesema.
Pia, amesema kuanzia leo Alhamisi Julai 2, 2026 chama kinatarajia kuanza mchakato wa kusajili Bodi ya Wadhamini na hatua iliyobaki ni kukamilisha muhtasari wa nyaraka kabla ya kuwasilishwa kwa mamlaka husika ili kutimiza matakwa ya kisheria.
Amesema Halmashauri Kuu imeidhinisha mchakato wa kuboresha katiba ya chama, hatua za awali zimekamilika na waraka umepelekwa katika ngazi za mikoa.
Ameeleza makatibu wa mikoa wameelekezwa kusimamia ukusanyaji wa maoni yatakayosaidia kukamilisha marekebisho ya katiba.
Alipotafutwa kuzungumzia tuhuma hizo, Mwalimu alijibu yuko hospitali kumtembelea mgonjwa, hivyo atafutwe baadaye.
Hata alipotafutwa baadaye, simu yake iliita bila kupokewa.
Maoni ya uchambuzi
Mchambuzi wa masuala ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Mohammed Bakari amesema migogoro inayojitokeza ndani ya vyama vya siasa ni jambo la kawaida.
Amesema lakini, kwa upande wa Chaumma, hali hiyo ilitarajiwa kutokana na sintofahamu iliyokuwepo wakati baadhi ya viongozi wake walipohamia chama hicho wakitokea Chadema.
Amesema Mwalimu na wenzake waliingia Chaumma kwa kishindo kutoka Chadema na baadaye wakawa na ushawishi ndani ya chama, jambo lililoonesha uzito wao kisiasa ndio maana akapata nguvu ya kupoka mamlaka ya mwenyekiti.
"Kwa mtazamo wangu, Mwalimu alifanikiwa kuchukua mamlaka makubwa ya mwenyekiti kutokana na nguvu aliyoingia nayo kutoka Chadema, ikiwamo uwezo wa kifedha.
“Kiashiria cha hilo ni namna mikutano waliyokuwa wakiifanya ilivyokuwa na maandalizi yaliyovutia na kuibua maswali kuhusu chanzo cha fedha hizo, kwani ilikuwa wazi hazikutokana na Chaumma pekee," amesema Profesa Bakari.
Amesema usimamizi wa fedha umekuwa changamoto kwa vyama vingi vya siasa nchini, hususan vya upinzani, hivyo vinapaswa vijitathmini na kuweka mifumo madhubuti.
"Katika kila jambo zuri linalotokea, mara nyingi huwa pia kuna athari hasi. Hilo ni jambo la kawaida na halipaswi kushangaza, hasa katika masuala ya kisiasa," amesema.
Mchambuzi mwingine wa siasa, kutoka Chuo Kikuu cha Zanzibar (Suza), Dk Abdallah Mkumbukwa amesema vyama vingi vya siasa, hususan vya upinzani, hukumbwa na migogoro mikubwa pindi inapofika suala la usimamizi wa fedha.
"Tangu baada ya uchaguzi mkuu kulikuwa na migogoro ya kifedha iliyokuwa ikiendelea chini kwa chini, lakini haikuwekwa wazi. Pia, ukosefu wa watu wenye uwezo wa kutatua migogoro hiyo na kufikia suluhu ndiyo unaochangia matatizo yanayoikumba Chaumma pamoja na vyama vingine," amesema.
Dk Mkumbukwa amesema changamoto nyingi ndani ya vyama vya siasa huanzia kwenye matumizi na usimamizi wa fedha mara nyingi vyama vikubwa vina vyombo maalumu vinavyosimamia masuala ya fedha, jambo linalosaidia kupunguza migogoro ya aina hiyo.