Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rungwe ataja sababu kumng’oa Mwalimu Chaumma

Muktasari:

  • Rungwe amesema ofisi ya Katibu Mkuu ina watendaji wengi, lakini hatua ya kwanza ilikuwa kumuondoa kiongozi mkuu wa ofisi hiyo, endapo uchunguzi utabaini kuwapo kwa viongozi au watendaji wengine waliohusika na tuhuma hizo, watachukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Hashimu Rungwe, ametoa tamko rasmi la kumtengua aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Salumu Mwalimu huku akimtangaza Naibu Katibu Mkuu wa Chaumma Bara, Benson Kigaila kuwa Kaimu Katibu Mkuu hadi uchaguzi mwingine utakapofanyika.

Rungwe amesema uamuzi huo umetokana na tuhuma mbalimbali zinazomkabili Mwalimu, ikiwemo kupoka mamlaka ya Mwenyekiti na kujifanya msemaji wa chama bila idhini, kutokuwa muwazi katika shughuli za uendeshaji wa chama, pamoja na kubadili uamuzi halali uliopitishwa na chama na kuyabadili kwa msimamo wake binafsi.

Akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya Chaumma, Rungwe amesema uamuzi huo ulifikiwa na wajumbe wa Halmashauri Kuu katika kikao kilichofanyika jana Juni 30, 2026, baada ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na Katibu Mkuu huyo.

Kabla ya kung'olewa, mapema asubuhi ya jana Jumanne, Mwalimu aliwasilisha barua kwa Mwenyekiti, akiomba kuundwe timu ya kuchunguza tuhuma zinazomkabili na akisema yupo tayari kuwa nje ya ofisi kupisha uchunguzi huo.

Hata hivyo, leo Rungwe amesema: "Mwalimu alikuwa akipoka mamlaka ya Mwenyekiti bila idhini yangu. Amekuwa akibadilisha misimamo halali ya chama na kuwasilisha misimamo yake binafsi kana kwamba ndiyo ya chama. Kutokana na makosa hayo ametenguliwa, na nafasi yake itakaimiwa na Benson Kigaila hadi uchaguzi mwingine utakapofanyika."

Rungwe amesema ofisi ya Katibu Mkuu ina watendaji wengi, lakini hatua ya kwanza ilikuwa kumuondoa kiongozi mkuu wa ofisi hiyo, endapo uchunguzi utabaini kuwapo kwa viongozi au watendaji wengine waliohusika na tuhuma hizo, watachukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa katiba ya chama.

"Chama hiki kinahitaji uwazi katika utendaji wake. Mimi kama Mwenyekiti sina jambo la kuficha ndani ya chama. Ninataka kila jambo lifanyike kwa uwazi kwa sababu shughuli za chama si mali binafsi ya mtu. Kinachotakiwa ni kufuata taratibu na katiba ya chama," amesema.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu Benson Kigaila amesema Mwalimu ameondolewa madarakani baada ya kujadiliwa na Kamati Kuu kufuatia tuhuma zilizokuwa zikimkabili, ambapo alipewa nafasi ya kujitetea.

"Mwalimu mwenyewe alikiri mbele ya Kamati Kuu na hata akaomba kujiuzulu. Hivyo, alikuwa anafahamu tuhuma hizo zilimhusu yeye binafsi. Uchunguzi ulianzishwa na Sekretarieti ya chama ambayo amekuwa akiifanyia kazi akiwa Katibu Mkuu," amesema Kigaila.

Amesema kama kungekuwa na ushahidi wa kuwapo kwa watu wengine waliohusika, Sekretarieti ingewajumuisha katika uchunguzi huo.

"Kama alivyosema Mwenyekiti, endapo itabainika kuwa kuna mtu mwingine aliyeshiriki matendo hayo, naye atachukuliwa hatua kwa mujibu wa katiba ya chama. Kwa sasa tumemwondoa kwanza aliyebainika kuwa na makosa," amesema.

Kigaila amesema baada ya kutenguliwa, Mwalimu ataendelea kuwa mwanachama wa kawaida wa Chaumma na hatahusika tena katika vikao vya uamuzi vya chama vinavyohitaji mtu mwenye wadhifa wa uongozi.

"Baada ya kutenguliwa, Mwalimu atabaki kuwa mwanachama wa kawaida. Atashiriki shughuli za chama katika ngazi ya tawi lake, kwa kuwa kila mwanachama ni mjumbe wa mkutano mkuu wa tawi," amesema.

Aidha, Kigaila amesema baada ya kukamilisha suala hilo, chama kinaendelea na utekelezaji wa mipango yake, ikiwemo kufanya kikao maalumu cha kutafuta rasilimali za kukiendesha chama.

"Ingawa wadau wanatuchangia, hatuwezi kutegemea misaada yao pekee. Tunahitaji kila mwanachama achangie ili chama kiweze kupiga hatua. Baada ya mkutano huu tunaelekea kupanga mikakati hiyo," amesema.

Pia amesema kuanzia kesho Alhamisi Julai 2, 2026 chama kinatarajia kuanza mchakato wa kusajili Bodi ya Wadhamini, ambapo hatua iliyobaki ni kukamilisha muhtasari wa nyaraka kabla ya kuwasilishwa kwa mamlaka husika ili kutimiza matakwa ya kisheria.

Amesema Halmashauri Kuu imeidhinisha mchakato wa kuboresha katiba ya chama, ambapo hatua za awali zimekamilika na waraka umepelekwa katika ngazi za mikoa. Kwa mujibu wake, makatibu wa mikoa wameelekezwa kusimamia ukusanyaji wa maoni yatakayosaidia kukamilisha marekebisho ya katiba.