CCM yaibukia kwenye mazishi ya kiongozi wa Chadema

Baadhi ya viongozi na wanachama wa CCM wakiwa kwenye foleni ya kuaga mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Chadema, Sylvester Masinde aliyefariki katika Hospitali ya Bugando. Picha na Mgongo Kaitira

Mwanza. "Siasa siyo Uadui," ndiyo kauli unayoweza kuitumia kuelezea kitendo cha wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakiongozwa na Mwenyekiti wa Umoja Vijana wa CCM Taifa, Mohammed Kawaida kuibuka katika Kanisa Katoliki la Watakatifu Petro na Paulo lililopo Mtaa wa Mwananchi jijini Mwanza kwa ajili ya kuaga mwili wa mwasisi wa Chadema, Sylvester Masinde.

Mzee Masinde ambaye enzi za uhai wake alikuwa ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema na Muasisi wa chama hicho alifariki Machi 15, 2023 katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando akipatiwa matibabu ya saratani ya tezi dume.

Akiongoza jopo la viongozi hao, Kawaida ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) ameambatana na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Sixbert Jichabu, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nyamagana, Peter Bega, Mjumbe wa NEC, Mwanaenzi Suluhu Hassan na wanachama wa CCM zaidi ya 20.

"Kwa niaba ya uongozi wa CCM tunatoa pole kwa Chadema kwa kumpoteza kiongozi aliyeshiriki kutengeneza maoni ya chama hiki. Tuko na Chadema katika kipindi hiki kigumu tunamuombea Mungu ampumzishe," amesema Kawaida ambaye amekaribishwa na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe mbali kuwashukuru viongozi na wanachama hao wa CCM kufika kuwafariji aliwataka kufikisha ujumbe wa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa ndoto ya Masinde ilikuwa kupata Katiba Mpya na Tume huru ya uchaguzi hivyo amuenzi kwa kutimiza ndoto hiyo.

"Baada ya kustaafu utumishi wake serikalini kwa hiari mwaka 1992, Mzee Masinde aliona bado kuna mapungufu katika mfumo wa demokrasia ya nchi yetu ambayo aliamini yataondolewa kwa kuwa na Katiba Mpya hivyo niwaomba mfikishe ujumbe huu kwa Rais Samia amuenzi Masinde kwa kutupatia Katiba Mpya," amesema Mbowe.

Mbowe amemuelezea Masinde enzi za uhai wake kama kiongozi anayependa haki, usawa na asiyependa uonevu hivyo akawataka wanachama wa Chadema kumuenzi kwa vitendo kwa kufanya hivyo.

Mwili wa Masinde ambao umefanyiwa maombi Maalum katika kanisa hilo unatarajiwa kuzikwa leo Saa 10:00 Alasiri katika makaburi ya eneo la Mwananchi kata ya Mahina jijini Mwanza.