Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CCM yaitaka Tamisemi kufanya marekebisho walimu kurundikana mjini

Muktasari:

  • CCM yaitaka Tamisemi kuweka utarabu bora wa upangaji wa walimu katika maeneo ya vijijini badala ya kuwaacha kukaa maeneo ya mjini.

Morogoro. Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo ameishauri Serikali kutawanya walimu kwa uwiano sawa ili kukidhi haja wanafunzi kufundishwa kwa idadi kamili ya walimu badala ya kuwaacha kujirundika eneo moja hasa la mjini.

Katibu mkuu huyo amesema hatua hiyo pia itasaidia  walimu kufundisha wanafunzi kwa idadi ndogo na kurahisisha utoaji elimu  huduma bora kwa urahisi.

Chongolo ametoa ushauri huo, leo Jumamosi Januari 28, 2023 katika ziara yake ya kichama ya siku tisa aliyoanza mkoani Morogoro, akiambatana na viongozi wenzake akiwemo Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Sophia Mjema na Katibu wa Oganaizesheni, Issa Haji Ussi.

Ziara hiyo itakayofanyika katika wilaya mbalimbali za Mkoa wa Morogoro ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 46 ya CCM yanayotarajiwa kufikia kilele chake Februari 5 mwaka huu, sherehe zitakazofanyika mkoani hapa.

Katika maelezo yake, Chongolo aliitaka Ofisi ya Rais Tamisemi kufanya mapitio kwa kupeleka walimu katika maeneo yenye uhitaji hasa vijijini, badala ya kuwaacha kukaa sehemu moja.

Amesema maeneo yote ya nchi yanahitaji huduma zinazofanana kama ni walimu basi kuwepo kwa uwiano kote ili kukidhi huduma ya elimu itakayotolewa kwa usahihi na ulinganifu katika maeneo yote.

Amesema sio sahihi walimu kukaa maeneo ya mijini huku vijijini kukiwa hakuna.

"Hatua hii inasababisha tabaka na upungufu wa wasomi katika maeneo ya vijijini, shule za kata na Serikali zipo kila eneo la nchi, sasa lazima tuzifanye ziwe na ubora na kuwa kimbilio la wananchi kwa kupeleka watoto kuanzia ngazi ya msingi.

"Hili nitalisimamia na kuhakikisha Gairo inapata walimu wa kutosha, nimeambiwa hapa Morogoro kuna maeneo ya walimu wa ziada, tutapitia takwimu na kuiagiza Tamisemi iratibu mchakato huu kwa kuwaondoa na kuwapeleka vijijini," amesema Chongolo.

Chongolo amesema kiwango cha ufaulu kuanzia ngazi ya msingi na sekondari wilayani Gairo bado hakiridhishi tofauti na miaka miwili iliyopita, akiwataka viongozi wilaya na mkoa kutafakari na kubaini kilichojitokeza.

Chongolo ambaye ni mkuu wa wilaya wa zamani za Kinondoni na Longido amesema kama mtu umeajiriwa na Serikali lazima akubali kufanya kazi katika maeneo yoyote ili kuhakikisha huduma bora inapatikana kwa kuwawezesha wanafunzi kupata huduma bora ya elimu.

Kwa upande wake, Mjema amewasisitizia viongozi wa ngazi mbalimbali kusikiliza kero za wananchi wao kwa wakati badala ya kusubiri ujio wa viongozi wakuu katika maeneo yao.

"Unaposikiliza kero inatakiwa iishe siku hiyo hiyo au siku chache zijazo badala ya kuiacha iendelee... kila akija kiongozi mwingine kero ile ile," amesema Mjema.