CCM yajipanga kuvunja mwiko kwa kuitwaa Kata ya Nangwa

Hanang. CCM imejipanga kuhakikisha inashinda na kuongoza Kata ya Nangwa ambayo kwa takriban miaka 15 imekuwa mikononi mwa Chadema.

Katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015 mgombea wa Chadema alishinda kata hiyo kwa kupata kura 1,452; CCM kura 1,347; ACT Wazalendo kura nane na CUF kura sita.

Mgombea wa CCM katika uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata hiyo, Portajia Baynit akiomba kura akihutubia mkutano wa kampeni Kijiji cha Nangwa juzi, alisema hatawaangusha wananchi wa eneo hilo hivyo wampe kura nyingi.

“Tumepoteza kura zetu miaka iliyopita, hivyo huu ni wakati wetu sasa wa kuonyesha kuwa CCM inaweza kuongoza Nangwa,” alisema Baynit.

Alisema iwapo atapata ridhaa ya kuwaongoza, atahakikisha anashirikiana nao kufanikisha maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwamo elimu, afya, kilimo, mifugo na maji.

Mgombea huyo alisema hakuna sababu ya kuwapa kura wapinzani ambao muda mrefu wamekuwa wakirudisha nyuma maendeleo kwa kupenda kesi.

Wagombea udiwani wa kata hiyo watakaopambana kwenye kinyang’anyiro hicho Novemba 26 ni Baynit (CCM), Yohana Daffi (Chadema) na Lucy Sulle (CUF).

Naye mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Hanang, Mathew Darema alisema kwamba wamejipanga kuhakikisha wanatwaa kata hiyo.

Akihutubia kwenye mkutano huo wa kampeni, Darema aliwataka wananchi wa eneo hilo kutofanya makosa kuchagua upinzani katika uchaguzi huo mdogo wa udiwani.

Darema alisema mgombea wa CCM wa kata hiyo, Baynit atawaletea maendeleo kuliko wagombea wa vyama vya upinzani ambao alidai hawana sera.

Alisema wananchi watafanya makosa wasipomchagua mgombea wa CCM, ambaye ni mwanamke shupavu.

“Mgombea wetu tunamwamini, ni mpambanaji ambaye ni shupavu kuhakikisha anasimamia maendeleo, mnahitaji kuchagua mtu ambaye atasaidia kusimamia kasi ya mwenyekiti wetu,” alisema.

Mwenyekiti huyo alisema chama hicho kinajivunia uteuzi wa mgombea wake kwa sababu ana uwezo wa kupambana kuhakikisha maendeleo yanapatikana.